Mwanzo 20

Mwanzo 20

Abrahamu na Sara wakiwa Gerari

1Abrahamu akaondoka huko kwenda nchi ya kusini, akakaa kati ya Kadeshi na Shuri, naye akatembea katika Gerari.[#Mwa 18:1; 26:6]

2Abrahamu akanena juu ya Sara mkewe, “Huyu ni dada yangu”. Basi Abimeleki mfalme wa Gerari akatuma watu wakamtwaa Sara.[#Mwa 12:11-15; 26:7]

3Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mke wa mtu.[#Zab 105:14; Ayu 4:12; 33:15; Mwa 19:7]

4Basi Abimeleki alikuwa hakumkaribia, akasema, Ee Bwana, Je! Utaua hata taifa lenye haki?[#Mwa 18:23-25]

5Je! Hukuniambia mwenyewe, “Huyu ni dada yangu?” Na mwanamke mwenyewe naye akasema, “Huyu ni kaka yangu”. Kwa ukamilifu wa moyo wangu, na kwa kutojua kwangu, nimefanya hivi.

6Mungu akamwambia katika ndoto, Nami nimejua ya kwamba kwa ukamilifu wa moyo wako umefanya hivi, ndipo nami nikakuzuia usinitendee dhambi, kwa hiyo sikukuacha umguse.[#Mwa 35:5; Kut 34:4; 1 Sam 25:26,34]

7Basi sasa umrudishe mwanamke kwa mtu huyo, maana yeye ni nabii, naye atakuombea, upate kuishi. Bali usipomrudisha, fahamu ya kwamba kwa hakika utakufa wewe na watu wote ulio nao.[#1 Sam 7:5; 2 Fal 5:11; Ayu 42:8; Yak 5:14-16; 1 Yoh 5:16]

8Abimeleki akaamka asubuhi na mapema, akawaita watumwa wake wote, akawaambia maneno hayo yote, nao watu hao wakaogopa sana.

9Kisha Abimeleki akamwita Abrahamu, akamwambia, Umetutenda nini? Nimekukosa nini, hata ukaleta juu yangu na juu ya ufalme wangu dhambi kuu? Umenitenda matendo yasiyotendeka.[#Mwa 39:9; Yos 7:25]

10Abimeleki akamwambia Abrahamu, Umeona nini hata ukatenda jambo hili?

11Abrahamu akasema, Kwa kuwa niliona, hakika hapana hofu ya Mungu mahali hapa, nao wataniua kwa ajili ya mke wangu.[#Mwa 42:18; Neh 5:15; Mit 16:6]

12Hata hivyo, kwa kweli yeye ni dada yangu, yaani binti wa baba yangu na wala sio binti wa mama yangu; ndipo akawa mke wangu.[#Mwa 11:29]

13Ikawa hapo Mungu aliponisafirisha kutoka nyumba ya baba yangu, nikamwambia, Hii ndiyo fadhili yako, utakayonifanyia. Kila mahali tuingiapo, useme, Huyu ni kaka yangu.[#Mwa 12:1,9,10,13]

14Basi Abimeleki akatwaa kondoo, na ng'ombe, na watumwa, na wajakazi, akampa Abrahamu, akamrudishia Sara mkewe.[#Mwa 12:16]

15Abimeleki akasema, Nchi yangu iko mbele yako, ishi upendapo.[#Mwa 13:9; 47:6]

16Naye akamwambia Sara, Tazama! Nimempa ndugu yako fedha elfu moja, itakuwa kifunika macho kwako mbele ya wote walio pamoja nawe, nawe utakuwa na haki mbele ya watu wote.[#Mwa 20:5]

17Abrahamu akamwomba Mungu, Mungu akamponya Abimeleki, na mkewe, na wajakazi wake, nao wakazaa wana.[#Ayu 42:8; Yak 5:16]

18Maana BWANA alikuwa ameyafunga matumbo ya watu wa nyumbani mwa Abimeleki, wasizae, kwa ajili ya Sara mkewe Abrahamu.[#Mwa 12:17]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania