The chat will start when you send the first message.
1Haya ni maono ya Isaya, mwana wa Amozi aliyoyaona kuhusu Yuda na Yerusalemu, siku za Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda.[#Hes 12:6; 2 Fal 15:1-7; 15:32–16:20; 18:1–20:21; 2 Nya 26:1-23; 27:1-9; 28:1-27; 29:1–32:33]
2Sikieni, enyi mbingu, tega sikio, Ee nchi, kwa maana BWANA amenena;
Nimewalisha watoto na kuwalea, nao wameniasi.
3Ng'ombe amjua bwana wake,[#Yer 9:3,6]
Na punda ajua kibanda cha bwana wake;
Bali Israeli hajui, watu wangu hawafikiri.
4Ole wake, taifa lenye dhambi, watu wanaochukua mzigo wa uovu, wazao wa watenda mabaya, watoto wanaoharibu; wamemwacha BWANA, wamemdharau yeye aliye Mtakatifu wa Israeli, wamefarakana naye na kurudi nyuma.[#Isa 57:3,4]
5Mbona mnataka kupigwa, hata sasa, hata mkazidi kuasi? Kichwa chote ni kigonjwa, moyo wote umezimia.[#Isa 9:13; Yer 2:30]
6Toka wayo wa mguu hadi kichwani hamna uzima ndani yake; bali jeraha na machubuko na vidonda vitokavyo usaha; havikufungwa, havikuzongwazongwa, wala havikulainishwa kwa mafuta.[#Yer 8:22]
7Nchi yenu ni ukiwa; miji yenu imeteketezwa kwa moto; nchi yenu, wageni wameila mbele ya macho yenu; nayo ni ukiwa, kana kwamba imeangamizwa na wageni.[#Kum 28:51]
8Na binti Sayuni ameachwa kama kibanda katika shamba la mizabibu, kama kipenu katika shamba la matango, kama mji uliohusuriwa.
9Kama BWANA wa majeshi asingalituachia mabaki machache sana, tungalikuwa kama Sodoma, tungalifanana na Gomora.[#Mwa 19:24; Rum 9:29]
10Lisikieni neno la BWANA, enyi waamuzi wa Sodoma; tegeni masikio msikie sheria ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora.[#Eze 16:46]
11Huu wingi wa sadaka zenu mnazonitolea una faida gani? Asema BWANA. Nimejaa mafuta ya kafara za kondoo dume, na mafuta ya wanyama walionona; nami siifurahii damu ya ng'ombe wala ya wana-kondoo wala ya mbuzi dume.[#Amo 5:21-22; Zab 50:8]
12Mjapo ili kuonekana mbele zangu, ni nani aliyetaka neno hili mikononi mwenu, kuzikanyaga nyua zangu?
13Msilete tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mwandamo na sabato, kuita makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada.
14Sikukuu zenu za mwezi mpya na karamu zenu zilizoamriwa, nafsi yangu yazichukia; mambo hayo yanilemea; nimechoka kuyachukua.
15Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu.[#Ayu 27:9; 1 Tim 2:8]
16Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya;[#Yer 4:14; Rum 12:9]
17jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane.[#Mik 6:8]
18Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama damu, zitakuwa kama sufu.[#1 Sam 12:7; Mik 6:2; Isa 41:21; 44:22; Zab 51:7; Mik 7:18; Efe 1:6-8]
19Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi;[#Kum 28:1]
20bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha BWANA kimenena haya.[#Tit 1:2]
21Mji huu uliokuwa mwaminifu umekuwaje kahaba! Yeye aliyejaa hukumu ya haki; haki ilikaa ndani yake, bali sasa wauaji!
22Fedha yako imekuwa takataka, divai yako imechanganywa na maji.
23Wakuu wako ni waasi, na rafiki za wezi; kila mtu hupenda rushwa, hufuata malipo; hawampatii yatima haki yake, wala maneno ya mjane hayawafikii.[#2 Nya 36:14; Yer 5:5; Dan 9:5; Hos 9:15]
24Kwa hiyo, asema Bwana, BWANA wa majeshi, Mwenye enzi, wa Israeli, Nitapata faraja kwa hao wanipingao, nitalipiza kisasi kwa adui zangu;[#Kum 28:63]
25nami nitakuelekezea wewe mkono wangu, na kukutakasa takataka zako kabisa, na kukuondolea bati lako lote;[#Ufu 3:19]
26nami nitawarejesha tena waamuzi wako kama walivyokuwa hapo kwanza, na washauri wako kama hapo mwanzo; baada ya hayo utaitwa, Mji wa haki, mji mwaminifu.
27Sayuni itakombolewa kwa hukumu, na waongofu wake kwa haki.
28Lakini waasi na wenye dhambi wote wataangamizwa pamoja, nao wamwachao BWANA watateketezwa.
29Kwa maana watatahayarika kwa sababu ya mialoni mliyoitamani, nanyi mtaaibishwa kwa sababu ya bustani mlizozichagua.[#Isa 57:5; 65:3]
30Maana mtakuwa kama mwaloni ambao majani yake yakauka, na kama bustani isiyo na maji.
31Na mtu hodari atakuwa kama makumbi, na kazi yake kama cheche ya moto; nao watawaka pamoja, wala hapana atakayewazima.