Isaya 11

Isaya 11

Ufalme wa amani

1Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda.[#Isa 53:2; Zek 6:12; Mdo 13:23; Yer 23:5; Zek 3:8; Ufu 5:5; 22:16]

2Na Roho ya BWANA itakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha BWANA;[#Isa 42:1; Mt 3:16; Yn 1:32; Mdo 10:38]

3na furaha yake itakuwa katika kumcha BWANA; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake;

4bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya.[#Zab 72:2,4; Ufu 19:11; Mal 4:6; Ufu 2:16; 2 The 2:8]

5Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia.[#Efe 6:14]

6Mbwamwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwanasimba na ng'ombe wanono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza.[#Hos 2:18; Isa 65:25]

7Ng'ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng'ombe.

8Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa kunyonya atatia mkono wake katika pango la fira.

9Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua BWANA, kama vile maji yanavyoifunika bahari.[#Hab 2:14]

Kurudi kwa mabaki wa Israeli na Yuda

10Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa makabila ya watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu.[#Ebr 4:1; Rum 15:12]

11Na itakuwa katika siku hiyo, Bwana atapeleka mkono wake mara ya pili, ili ajipatie watu wake watakaosalia, kutoka Ashuru, na kutoka Misri, na kutoka Pathrosi, na kutoka Kushi, na kutoka Elamu, na kutoka Shinari, na kutoka Hamathi, na kutoka visiwa vya bahari.[#Zek 10:10]

12Naye atawatwekea mataifa bendera, atawakutanisha watu wa Israeli waliotupwa, atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika, kutoka ncha nne za dunia.[#Yn 7:35]

13Na wivu wa Efraimu utaondoka, na wale wanaomwudhi Yuda watakatiliwa mbali; Efraimu hatamhusudu Yuda, wala Yuda hatamwudhi Efraimu.[#Gal 3:28]

14Nao watashuka, watalirukia bega la Wafilisti upande wa magharibi; nao pamoja watawateka wana wa mashariki; watanyosha mkono juu ya Edomu na Moabu; na wana wa Amoni watawatii.

15Na BWANA atauangamiza kabisa ulimi wa bahari ya Misri; na kwa upepo wake uteketezao atatikisa mkono wake juu ya Mto, naye ataupiga, uwe vijito saba, na kuwavusha watu waliovaa viatu bila kulowa.[#Ufu 16:12]

16Itakuwako njia kuu kwa mabaki ya watu wake watakaobaki, watokao Ashuru, kama vile ilivyokuwako kwa Israeli, katika siku ile waliyotoka katika nchi ya Misri.[#Kut 14:29; Isa 51:10]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania