Isaya 21

Isaya 21

Utabiri juu ya Babeli, Edomu na Arabuni

1Ufunuo juu ya nyika kando ya bahari. Kama tufani za Negebu zikaribiavyo kwa kasi, inakuja kutoka nyikani, toka nchi itishayo.[#Zek 9:14; #21:1 tafsiri yake ni Nchi za kusini.]

2Nimeoneshwa maono magumu; atendaye hila anatenda hila, mharibu anaharibu. Panda juu, Ee Elamu; husuru, Ee Umedi; mimi ninakomesha maombolezo yake yote.[#1 Sam 24:13; Yer 49:34; Isa 24:16; 13:17]

3Kwa sababu hiyo viuno vyangu vimejaa maumivu, uchungu umenishika, kama uchungu wa mwanamke azaaye; ninaumwa sana, nisiweze kusikia; nimefadhaishwa kwa hofu, nisiweze kuona.

4Moyo wangu unapigapiga, utisho umenitaabisha, gizagiza la jioni nilipendalo limegeuka likanitetemesha.[#Kum 28:67]

5Wanaandaa meza, wanaweka ulinzi, wanakula, wanakunywa. Simameni, enyi wakuu, itieni ngao mafuta.[#Dan 5:5]

6Maana Bwana ameniambia hivi, Nenda, weka mlinzi; aonayo na ayatangaze.

7Naye akiona kundi la wapanda farasi, wakienda wawili wawili, na kundi la punda, na kundi la ngamia; na asikilize kwa makini, kwa makini sana.

8Ndipo akalia kama simba, Ee Bwana, mimi nasimama daima juu ya mnara wakati wa mchana, na kila usiku ninakaa katika zamu ya ulinzi wangu.[#Hab 2:1]

9Na, tazama, linakuja kundi la watu, wapanda farasi, wakienda wawili wawili. Akajibu na kusema, Babeli umeanguka, umeanguka; na sanamu zote za miungu yake zimevunjwa chini.[#Isa 13:19; Yer 50:2; Ufu 14:8; 18:2]

10Ewe wangu niliyekufikicha na kukupura; Hayo niliyoyasikia kwa BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, nayatangaza kwenu.[#Yer 51:33; Mik 4:13; Hab 3:12]

11Ufunuo juu ya Duma. Mtu ananililia toka Seiri, Ee mlinzi, habari gani za usiku? Ee mlinzi, habari gani za usiku?[#1 Nya 1:30; Eze 35:2; Oba 1:1]

12Mlinzi akasema, Mchana unakuja na usiku pia; mkitaka kuuliza, ulizeni; njoni tena.

13Ufunuo juu ya Arabuni.[#1 Nya 1:9]

Ndani ya msitu wa Arabuni mtalala,

Enyi misafara ya Wadedani.

14Waleteeni wenye kiu maji,[#Ayu 6:19]

Enyi wenyeji wa nchi ya Tema;

Nendeni kuwalaki wakimbiao na chakula chao.

15Kwa maana wanakimbia mbele ya panga,

Upanga uliofutwa, na upinde uliopindwa,

Na mbele ya ukali wa vita.

16Kwa sababu Bwana ameniambia hivi, Katika muda wa mwaka, kama miaka ya mtu mwenye kuajiriwa, utaangamia utukufu wote wa Kedari.[#Mwa 25:13; Zab 120:5; Wim 1:5; Isa 60:7]

17Na mabaki ya hesabu ya wavuta pinde, hao mashujaa wa Kedari watakuwa wachache; maana BWANA, Mungu wa Israeli, amenena neno hili.[#Hes 23:19; 1 Sam 15:29; Isa 1:20; Mt 24:35; Mk 13:31; Lk 21:33; 1 Pet 1:25]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania