The chat will start when you send the first message.
1Ole wao wateremkao kwenda Misri wapate msaada, na kutegemea farasi; watumainio magari kwa kuwa ni mengi, na wapanda farasi kwa kuwa ni hodari sana; lakini hawamwangalii Mtakatifu wa Israeli, wala hawamtafuti BWANA![#Kum 28:68; Eze 17:15; Hos 11:8; Zab 20:7; Dan 9:13; Hos 7:7]
2Lakini yeye naye ana akili, naye ataleta uovu, wala hatayatangua maneno yake; bali ataondoka juu ya nyumba yao watendao mabaya, na juu ya msaada wa hao watendao maovu.
3Basi Wamisri ni wanadamu wala si Mungu, na farasi wao ni nyama wala si roho; na BWANA atakaponyosha mkono wake, yeye asaidiaye atajikwaa, na yeye asaidiwaye ataanguka, nao wataangamia wote pamoja.[#Zab 9:20; Eze 28:9]
4Maana BWANA aniambia hivi, Kama vile ilivyo simba angurumapo na mwanasimba juu ya mawindo yake, wachungaji wengi wakiitwa ili kumpiga, lakini hatiwi hofu na sauti zao, wala kufanya woga kwa sababu ya mshindo wao; ndivyo BWANA wa majeshi atakavyoshuka ili kufanya vita juu ya mlima Sayuni, na juu ya kilima chake.
5Kama ndege warukao, BWANA wa majeshi ataulinda Yerusalemu; ataulinda na kuuokoa, atapita juu yake na kuuhifadhi.[#Kum 32:11; Zab 91:4]
6Mwelekeeni yeye mliyemwasi sana, enyi wana wa Israeli.[#Hos 9:9]
7Maana katika siku hiyo kila mtu atatupa sanamu zake za fedha, na sanamu zake za dhahabu, ambazo mikono yenu imezifanya, zikawa dhambi kwenu.[#1 Fal 12:30]
8Ndipo huyo Mwashuri ataanguka kwa upanga ambao si wa mtu; na upanga usio upanga wa mtu utamwangamiza; naye ataukimbia upanga, na vijana wake watatoa kodi.[#2 Fal 19:35]
9Na mwamba wake utatoweka kwa sababu ya hofu, nao wakuu wake wataionea bendera hofu kuu, asema BWANA, ambaye moto wake u katika Sayuni, na tanuri yake katika Yerusalemu.[#Law 6:13]