The chat will start when you send the first message.
1Mwenye haki hupotea, wala hakuna atiaye hayo moyoni; na watu watauwa huondolewa, wala hakuna afikiriye ya kuwa mwenye haki ameondolewa asipatikane na mabaya.
2Yeye huingia katika amani; wao hustarehe katika vitanda vyao, kila mtu aendaye katika unyofu wake.
3Lakini ninyi karibuni hapa, enyi wana wa mwanamke mchawi, uzao wa mzinzi na kahaba.[#Mal 3:5]
4Mnafanya dhihaka yenu juu ya nani? Mmepanua vinywa vyenu, na kutoa ndimi zenu? Je, ninyi si wana wa uasi, uzao wa uongo;
5ninyi mnaowasha tamaa zenu kati ya mialoni, chini ya kila mti wenye majani mabichi; ninyi mnaoua watoto mabondeni, chini ya mianya ya majabali?
6Sehemu yako i katika makokoto ya bonde; hayo ndiyo kura yako; umeyamwagia hayo sadaka ya kinywaji, umeyatolea sadaka ya unga; je! Niwe radhi na mambo hayo?
7Umeweka kitanda chako juu ya mlima mrefu ulioinuka sana; ukaenda huko ili kutoa dhabihu.[#Eze 23:41]
8Na nyuma ya milango na miimo umeweka kumbukumbu lako; kwa maana umejifunua nafsi yako kwa ajili ya mwingine, si kwa ajili yangu, ukakwea juu; umekipanua kitanda chako, nawe umefanya maagano na hao; ulikipenda kitanda chao hapo ulipokiona.[#Eze 16:26]
9Ulimwendea mfalme na mafuta ya marhamu, ukaongeza manukato yako, ukawatuma wajumbe wako waende mbali, ukajidhili sana hadi kuzimu.
10Ulikuwa umechoka kwa ajili ya urefu wa njia yako; lakini hukusema, Hapana matumaini; ulipata kuhuishwa nguvu zako; kwa sababu hiyo hukuugua.
11Tena ni nani uliyemwogopa na kumhofu, hata ukasema uongo, wala hukunikumbuka mimi, wala kuweka hayo moyoni? Je! Mimi sikunyamaza tangu zamani, hata huniogopi?[#Zab 50:21]
12Mimi nitatangaza haki yako, na matendo yako hayatakufaa.
13Utakapolia, na wakuponye hao uliowakusanya; lakini upepo utawachukua; uvuvio tu utawachukulia mbali; lakini yeye anayenitumaini ataimiliki nchi, na kuurithi mlima wangu mtakatifu.[#Zab 37:3,9; Mt 5:5]
14Naye atasema,
Tutieni, tutieni,
Itengenezeni njia,
Ondoeni kila kizuizi
Katika njia ya watu wangu.
15Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu.[#Ayu 6:10; Lk 1:49; Zek 2:13; Zab 68:4; 34:18]
16Kwa kuwa sitashindana na watu siku zote, wala sitakuwa na hasira siku zote; maana roho ingezimia mbele zangu, na hizo nafsi nilizozifanya.[#Zab 78:38,39; Mik 7:18; Ebr 12:9]
17Kwa sababu ya uovu wa kutamani kwake niliona hasira, nikampiga; nilificha uso wangu, nikaona ghadhabu; naye akaendelea kwa ukaidi, kuifuata njia ya moyo wake mwenyewe.[#Eze 33:31]
18Nimeziona njia zake; nami nitamponya; nitamwongoza pia, nitamrudishia faraja zake, yeye na hao wanaomlilia.[#Zab 73:24]
19Mimi nayaumba matunda ya midomo; Amani, amani, kwake yeye aliye mbali, na kwake yeye aliye karibu; asema BWANA; nami nitamponya.[#Ebr 13:15; Mdo 2:39; Efe 2:17]
20Bali wabaya wanafanana na bahari iliyochafuka; maana haiwezi kutulia, na maji yake hutoa tope na takataka.
21Hapana amani kwa waovu; asema Mungu wangu.[#Isa 48:22]