The chat will start when you send the first message.
1Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nilimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu.[#1 Fal 22:19; Eze 10:1; Yn 12:41; Ufu 4:2; 2 Fal 15:7; 2 Nya 26:23]
2Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka.
3Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni BWANA wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake.[#Ufu 4:8]
4Na misingi ya vizingiti ikatikisika kwa sababu ya sauti yake aliyelia, nayo nyumba ikajaa moshi.[#Ufu 15:8]
5Ndipo niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, BWANA wa majeshi.
6Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu;[#Law 16:12; Ebr 13:10]
7akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa.
8Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi.[#Mwa 1:26]
9Naye akaniambia, Nenda, ukawaambie watu hawa, Endeleeni kusikia, lakini msifahamu; endeleeni kutazama, lakini msione.[#Mt 13:14-15; Mk 4:12; Lk 8:10; Yn 12:40; Mdo 28:26-27]
10Zifanye akili za watu hawa zipumbae, na uyatie uzito masikio yao, na uyafumbe macho yao; wasije wakaona kwa macho yao, na kusikia kwa masikio yao, na kufahamu kwa mioyo yao, na kurejea na kuponywa.
11Ndipo nilipouliza, Ee Bwana, hata lini? Naye akanijibu, Hadi miji itakapokuwa ukiwa, haina wenyeji, na nyumba zitakapokuwa hazina watu, na nchi hii itakapokuwa ganjo kabisa;
12hadi BWANA atakapowahamisha watu waende mbali sana, na mahame yatakapokuwa mengi ndani ya nchi.[#Kum 28:64]
13Na ijapokuwa imebaki sehemu moja katika sehemu kumi ndani yake, italiwa hii nayo; kama mvinje na kama mwaloni, ambao shina lake limebaki, ingawa imekatwa; kadhalika mbegu takatifu ndiyo shina lake.[#Rum 11:5]