The chat will start when you send the first message.
1Watu wasionitaka wanauliza habari zangu; nimeonekana na hao wasionitafuta; nililiambia taifa lisiloitwa kwa jina langu,[#Zab 22:27; Isa 2:2,3; Efe 2:12,13; Isa 63:19; Rum 10:20]
2Nitazameni, nitazameni. Mchana kutwa nimewanyoshea mikono yangu watu walioasi, watu waendao katika njia isiyo njema, wakifuata mawazo yao wenyewe;[#Kum 32:5; Zab 36:4; Rum 10:21]
3watu wanikasirishao mbele za uso wangu daima, wakitoa dhabihu katika bustani zao, na kufukiza uvumba juu ya matofali;[#Law 17:5; Isa 1:29]
4waketio kati ya makaburi, na kulala katika mahali pao pa siri; walao nyama ya nguruwe, na mchuzi wa vitu vinichukizavyo u katika vyombo vyao;[#Kum 18:11; Law 11:7]
5watu wasemao, Simama peke yako, usinikaribie mimi, kwa maana mimi ni mtakatifu kuliko wewe; watu hao ni moshi puani mwangu, moto uwakao mchana kutwa.[#Mt 9:11; Lk 5:30; Yud 1:19]
6Tazama, neno hili limeandikwa mbele zangu. Sitanyamaza, lakini nitalipa, naam, mimi nitawalipa ujira wao vifuani mwao;[#Kum 32:34; Mal 3:16]
7maovu yenu na maovu ya baba zenu pamoja, asema BWANA, ninyi mliofukiza uvumba juu ya milima, na kunitukana juu ya vilima; basi, kwa ajili ya hayo nitawapimia kwanza kazi yao vifuani mwao.[#Law 26:39; Zab 106:6; Dan 9:8; Mt 23:32]
8BWANA asema hivi, Kama vile divai mpya ipatikanavyo katika kichala, na mtu mmoja husema, Usikiharibu kwa maana mna baraka ndani yake; ndivyo nitakavyotenda kwa ajili ya watumishi wangu, ili nisiwaharibu wote.[#Yoe 2:14]
9Nami nitaleta uzao toka Yakobo, na mrithi wa milima yangu toka Yuda, na mteule wangu atairithi, na watumishi wangu watakaa huko.[#Mt 24:22]
10Na Sharoni itakuwa zizi la makundi ya kondoo, na bonde la Akori mahali pa kulala makundi ya ng'ombe, kwa ajili ya watu wangu walionitafuta.[#Hos 2:15; Yos 7:24-26]
11Bali ninyi mmwachao BWANA, na kuusahau mlima wangu mtakatifu, na kuandaa meza kwa ajili ya Bahati, na kuijazia Ajali vyombo vya divai iliyochanganyika;[#Eze 23:41; 1 Kor 10:21]
12mimi nitawaandikia kuuawa kwa upanga, na ninyi nyote mtainama ili kuchinjwa; kwa sababu nilipoita hamkuitika; niliponena, hamkusikia; bali mlitenda yaliyo mabaya machoni pangu, mlichagua mambo nisiyoyafurahia.[#Mit 1:24; Isa 66:4; Yer 7:13; Zek 7:7]
13Kwa hiyo Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, watumishi wangu watakula, bali ninyi mtaona njaa; tazama, watumishi wangu watakunywa, bali ninyi mtaona kiu; tazama, watumishi wangu watafurahi, bali ninyi mtatahayarika;
14tazama, watumishi wangu wataimba kwa furaha ya moyo, bali ninyi mtalia kwa huzuni ya moyo; mtapiga kelele kwa sababu ya uchungu wa roho zenu.
15Nanyi mtaliacha jina lenu kuwa laana kwa wateule wangu. Na Bwana MUNGU atakuua; naye atawaita watumishi wake kwa jina lingine.[#Mit 10:7; Mdo 11:26]
16Hata itakuwa yeye atakayejibariki duniani, atajibariki kwa Mungu wa kweli; naye atakayeapa duniani, ataapa kwa Mungu wa kweli. Kwa kuwa taabu za kwanza zimesahauliwa, na kwa kuwa zimefichwa machoni pangu.
17Maana, tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni.[#Isa 66:22; 2 Pet 3:13; Ufu 21:1]
18Lakini furahini, mkashangilie daima, kwa ajili ya hivi niviumbavyo; maana, tazama, naumba Yerusalemu uwe shangwe, na watu wake wawe furaha.
19Nami nitaufurahia Yerusalemu, nitawaonea shangwe watu wangu; sauti ya kulia haitasikika ndani yake tena, wala sauti ya kuomboleza.[#Ufu 21:4; 7:17]
20Hatakuwapo tena mtoto wa siku chache, wala mzee asiyetimia siku zake; kwa maana mtoto atakufa mwenye umri wa miaka mia; bali mtenda dhambi mwenye umri wa miaka mia atalaaniwa.[#Mhu 8:12]
21Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake.[#Law 26:16]
22Hawatajenga, kisha akakaa mtu mwingine ndani yake; hawatapanda, kisha akala mtu mwingine; maana kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, na wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi.
23Hawatajitaabisha kwa kazi bure, wala hawatazaa kwa taabu; kwa sababu wao ni wazao wa hao waliobarikiwa na BWANA, na watoto wao pamoja nao.[#Kum 28:41; Hos 9:12]
24Na itakuwa ya kwamba, kabla hawajaomba, nitajibu; na wakiwa bado wanena, nitasikia.[#Zab 32:5; Dan 9:21; Mt 6:8; Mdo 4:31]
25Mbwamwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja, na simba atakula majani kama ng'ombe; na mavumbi yatakuwa chakula cha nyoka. Hawatadhuru wala kuharibu katika mlima wangu mtakatifu wote, asema BWANA.[#Mwa 3:14; Rum 16:20; Isa 2:2; Dan 2:35; Ufu 14:1; Isa 11:6-9]