The chat will start when you send the first message.
1Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu, na kusema,
2Je! Huu wingi wa maneno usijibiwe?
Na mtu aliyejaa maneno, je! Ahesabiwe kuwa na haki?
3Je! Majivuno yako yawanyamazishe watu wawe kimya?
Nawe hapo ufanyapo dhihaka, je! Hapana mtu atakayekutahayarisha?
4Kwa kuwa wewe wasema, Mafunzo yangu ni safi,[#Ayu 6:10; 1 Pet 3:15]
Nami ni safi machoni pako.
5Lakini, laiti Mungu angenena,
Na kuifunua midomo yake juu yako;
6Tena akuonyeshe hizo siri za hekima,[#Omb 3:22]
Ya kuwa hufanikiwa katika kuyatimiza makusudi yake!
Ujue basi ya kuwa Mungu akuachilia katika uovu wako.
7Je! Wewe waweza kuuvumbua ukuu wa Mungu?[#Ayu 5:9; Mhu 3:11; Isa 40:28; Mt 11:27; Rum 11:33; Efe 3:8]
Waweza kuufikia upeo wa huyo Mwenyezi?
8Ni juu mno kama mbingu; waweza kufanya nini wewe?
Ni wenye kina kuliko kuzimuni; waweza kujua nini wewe?
9Cheo chake ni kirefu kuliko dunia,
Ni kipana zaidi ya bahari.
10Yeye akipita, na kufunga watu,
Na kuwaita hukumuni, ni nani basi awezaye kumzuia?
11Kwa kuwa yeye awajua watu baradhuli;[#Zab 10:11]
Anapouona uovu, je; hatauangalia?
12Lakini mpumbavu aweza kupata ufahamu,
Ingawa mwanadamu huzaliwa kama mtoto wa punda mwitu.
13Wewe ukiuweka moyo wako kwa uelekevu,[#1 Sam 7:3; Zab 78:8; 143:6]
Na kumnyoshea mikono yako;
14Ikiwa una uovu mkononi mwako, uweke mbali nawe,
Wala usikubali upuzi kukaa hemani mwako;
15Hakika ndipo utakapopata kuinua uso pasipo ila;[#Mwa 4:5; Ayu 22:26; Zab 119:6; 1 Tim 2:8; 1 Yoh 3:21]
Naam, utathibitika, wala hutakuwa na hofu;
16Kwa kuwa utasahau mateso yako;
Utayakumbuka kama maji yaliyokwisha pita;
17Na maisha yako yatakuwa meupe kuliko adhuhuri;
Giza lake litakuwa kama alfajiri.
18Nawe utakuwa salama, kwa sababu kuna matumaini;
Naam, utatafutatafuta kando yako, na kupumzika salama.
19Tena utalala, wala hapana atakayekutia hofu;
Naam, wengi watakutafuta uso wako.
20Lakini macho ya waovu yataingia kiwi,
Nao hawatakuwa na njia ya kukimbilia,
Na matumaini yao yatakuwa ni kutoa roho.