The chat will start when you send the first message.
1Mbona nyakati zisiwekwe na Mwenyezi?[#Mdo 1:7]
Na hao wamjuao mbona hawazioni siku zake?
2Wako waziondoao alama za mipaka;[#Kum 19:14]
Huyachukua makundi na kuyalisha.
3Huwanyang'anya yatima punda wao,[#Kum 24:6,10,12,17]
Humtwaa rehani ng'ombe wake mwanamke mjane.
4Humgeuza mhitaji aiache njia;[#Mit 28:28]
Maskini wa nchi hujificha pamoja.
5Tazama, kama punda mwitu jangwani
Wao hutoka kwenda kazini mwao, wakitafuta chakula kwa bidii;
Jangwa huwapa chakula cha watoto wao.
6Hukata nafaka zao mashambani;
Na kuokota zabibu za waovu.
7Hujilaza usiku kucha uchi bila nguo,[#Kut 22:26; Kum 24:12; Isa 58:7]
Wala hawana cha kujifunika baridi.
8Hutota kwa manyunyu ya milimani,[#Omb 4:5]
Na kugandamania kwa jabali ili kujikinga,
9Wako wamwondoao matitini kwa nguvu huyo asiye na baba,
Na kutwaa rehani kwa maskini;
10Hata wazunguke uchi bila mavazi,
Nao wakiwa na njaa huchukua miganda;
11Hushindika mafuta ndani ya kuta za watu hao;
Wakanyaga mashinikizo, nao wana kiu.
12Watu huugua toka mji ulio na watu wengi,[#Mhu 8:11]
Na roho yake aliyejeruhiwa hupiga ukelele;
Wala Mungu hauangalii upumbavu.
13Hawa ni katika hao waliouasi mwanga;
Hawazijui njia zake,
Wala hawakai katika mapito yake.
14Mwuaji huamka asubuhi kukipambazuka, huwaua maskini na wahitaji;
Tena wakati wa usiku yu kama mwizi.
15Tena jicho lake mzinifu hungojea wakati wa gizagiza,
Akisema, Hapana jicho litakaloniona;
Naye huuficha uso wake.
16Wao hutoboa nyumba gizani;[#Yn 3:20]
Hujifungia ndani wakati wa mchana;
Hawaujui mwanga.
17Maana asubuhi kwao wote ni kama giza tupu;
Maana wao wavijua vitisho vya hiyo giza tupu.
18Mwasema, Yeye ni mwepesi juu ya uso wa gharika;
Sehemu yao inalaaniwa duniani;
Hageuki kwenda njia ya mizabibuni.
19Ukame na joto hukausha maji ya theluji;
Kama kuzimu kuwafanyavyo watenda dhambi.
20Tumbo lililomzaa litamsahau; buu litamla na kuona tamu;[#Mit 10:7]
Hatakumbukwa tena;
Na udhalimu utavunjwa kama mti.
21Naam, yeye huwala walio tasa wasiozaa;
Wala hamtendei mema mwanamke mjane.
22Lakini Mungu huwadumisha wenye uwezo kwa nguvu zake;
Huinuka, wasiokuwa na tumaini la kuishi.
23Huwapa usalama, nao wapumzika kwao;
Na macho yake yako juu ya njia zao.
24Wao wametukuzwa; lakini kitambo kidogo hutoweka;[#Zab 37:35,36]
Naam, hushushwa, na kuondolewa njiani kama wengine wote,
Nao hukatwa kama vile masuke ya ngano.
25Na kama sivyo sasa, ni nani atakayenihukumu mimi kuwa ni mwongo,
Na kuyafanya maneno yangu kuwa si kitu?