Ayubu 36

Ayubu 36

Elihu asifia wema wa Mungu

1Tena Elihu akaendelea na kusema,

2Ningojee kidogo nami nitakueleza;

Kwa kuwa ningali na maneno kwa ajili ya Mungu.

3Nitayaleta maarifa yangu kutoka mbali,

Nami nitampa haki Muumba wangu.

4Maana hakika maneno yangu si ya uongo;

Aliyekamilika katika maarifa yu pamoja nawe.

5Tazama, Mungu ni hodari, wala hamdharau mtu yeyote;

Ana uweza katika nguvu za fahamu.

6Hauhifadhi uhai wa waovu;

Lakini huwapa wateswao haki yao.

7Yeye hawaondolei macho yake wenye haki;[#Zab 113:8]

Lakini pamoja na wafalme huwaweka

Katika viti vya enzi milele, nao hutukuzwa.

8Nao wakifungwa kwa pingu,[#Zab 107:10]

Wakitwaliwa kwa kamba za mateso;

9Ndipo huwaonesha matendo yao,

Na makosa yao, ya kuwa wametenda kwa kujivuna.

10Yeye huyafunua masikio yao, wasikie maonyo,

Na kuwaagiza warudi kuuacha uovu.

11Kama wakisikia na kumtumikia,[#Ayu 11:13-19; Isa 1:19; 1 Tim 4:8; Yak 5:5]

Watapisha siku zao katika kufanikiwa,

Na miaka yao katika furaha.

12Lakini wasiposikia, wataangamia kwa upanga,

Nao watakufa pasipo maarifa.

13Lakini hao wasiomcha Mungu mioyoni hujiwekea hasira

Hawalilii msaada hapo awafungapo.

14Wao hufa wakingali vijana,

Na uhai wao huangamia katikati ya wachafu.

15Yeye humponya aliyetaabika kwa njia ya taabu yake,

Na kuyafunua masikio yao kwa maonevu.

16Naam, yeye angekuongoza utoke katika msiba

Hata mahali penye nafasi, ambapo hapana kizuizi;

Na kilichowekwa mezani pako kingejaa mafuta.

17Lakini umejaa hukumu ya waovu;

Hukumu na haki hukushika.

18Basi ujitunze, isije hasira ikakuvuta hata ukafanya mzaha;

Wala usikubali ukuu wa ukombozi ukugeuze.

19Je! Mali yako itatosha, hata usiwe katika taabu,

Au uwezo wote wa nguvu zako?

20Usiutamani usiku,

Wakati watu wakatwapo katika mahali pao.

21Jitunze, usiutazame uovu;[#Ebr 11:25]

Kwani umeuchagua huo zaidi ya taabu.

22Tazama, Mungu hutenda makuu kwa uweza wake;[#Isa 40:13; Rum 11:34; 1 Kor 2:16]

Ni nani afundishaye kama yeye?

23Ni nani aliyemwagiza njia yake?[#Kum 32:4]

Au ni nani awezaye kusema, Wewe umetenda yasiyo haki?

Elihu atangaza ukuu wa Mungu

24Kumbuka kuitukuza kazi yake,[#Zab 33:4; Dan 4:37; Yer 9:24; 1 Kor 1:31; 2 Kor 10:17; Ufu 15:3]

Watu waliyoiimbia.

25Wanadamu wote wameitazama;[#Rum 1:19]

Watu huiangalia kwa mbali.

26Tazama, Mungu ni mkuu, nasi hatumjui;[#1 Kor 13:12; Zab 90:2; Ebr 1:12]

Hesabu ya miaka yake haichunguziki.

27Maana yeye huvuta juu matone ya maji,

Yamwagikayo katika mvua kutoka ukungu wake;

28Ambayo mawingu yainyesha

Na kudondoza juu ya wanadamu kwa wingi.

29Naam, mtu aweza kuelewa matandazo ya mawingu,

Ngurumo za makao yake?

30Tazama, yeye huutandaza mwanga wake, umzunguke;

Naye hufunika vilindi vya bahari.

31Kwani huwahukumu makabila ya watu kwa njia hizi;

Hutoa chakula kwa ukarimu.

32Yeye huifunika mikono yake kwa umeme;

Na kuuagiza shabaha utakayopiga.

33Mshindo wake hutoa habari zake,

Anayewaka hasira juu ya uovu.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania