Ayubu 5

Ayubu 5

Ayubu akosolewa na Mungu

1Haya, ita sasa; je! Yuko atakayekujibu?

Nawe utamwelekea yupi katika hao watakatifu?

2Kwani hasira humwua mtu mpumbavu,

Nao wivu humwua mjinga.

3Nimewaona wapumbavu wakishusha mizizi;

Lakini mara niliyalaani maskani yake.

4Watoto wake wako mbali na wokovu,

Nao wamesongwa langoni,

Wala hapana atakayewaponya.

5Mavuno yake wale wenye njaa huyala,

Na kuyatwaa hata kuyatoa miibani,

Nao wenye kiu huzitwetea mali zao.

6Kwani taabu haitoki mchangani,

Wala mashaka hayachipuki katika nchi;

7Lakini mwanadamu huzaliwa ili apate shida,

Kama cheche za moto zirukavyo juu.

8Lakini mimi ningemtafuta Mungu,[#Zab 50:15]

Ningemwekea Mungu kesi yangu;

9Yeye afanyaye mambo makuu, yasiyotambulikana;

Mambo ya ajabu yasiyo na hesabu;

10Yeye atoaye mvua inyeshe juu ya nchi,

Na kuyapeleka maji mashambani;

11Awainuaye juu hao walio chini;

Na hao waombolezao hukuzwa wawe salama.

12Yeye huitangua mipango ya wadanganyifu,

Mikono yao isipate kuyatimiza makusudi yao.

13Yeye huwanasa wenye hekima katika hila yao wenyewe;[#1 Kor 3:19]

Na mashauri ya washupavu yaharibika kwa haraka.

14Wao hupatwa na giza wakati wa mchana,

Hupapasa mchana vile vile kama usiku.

15Lakini yeye huokoa na upanga wa kinywa chao,

Hata kumwokoa mhitaji na mkono wake aliye hodari.

16Basi hivi huyo maskini ana matumaini,

Na uovu hufumba kinywa chake.

17Tazama, yu heri mtu yule Mungu amwadhibuye;[#Mit 3:11-12; Ebr 12:5-6; Zab 94:12; Yak 1:12]

Kwa hiyo usidharau kurudiwa na huyo Mwenyezi.

18Kwani yeye huumiza, lakini tena huuguza;[#Hos 6:1]

Yeye hutia jeraha, na mikono yake huponya.

19Yeye atakuokoa na mateso sita;[#Kut 12:46; Zab 34:19; Yn 19:36; Zab 91:10; Mit 1:33; 2 The 3:3; 2 Pet 2:9]

Naam, hata katika saba hapana uovu utakaokugusa.

20Wakati wa njaa atakukomboa na mauti;

Na vitani atakukomboa na nguvu za upanga.

21Utafichwa na mapigo ya ulimi;[#Zab 31:15]

Wala usiogope maangamizo yatakapokuja.

22Wewe utayacheka maangamizo na njaa;

Wala hutawaogopa wanyama wakali wa nchi.

23Kwani utakuwa na mapatano na mawe ya bara;[#Zab 91:12]

Nao wanyama wa bara watakuwa na amani kwako.

24Nawe utajua ya kwamba hema yako ni salama;

Na zizi lako utalikagua, wala usikose kitu.

25Tena utajua ya kwamba uzao wako utakuwa mwingi,

Na uzao wako utakuwa kama nyasi za nchi.

26Utafika kaburini mwenye umri mtimilifu,

Kama mganda wa ngano ulivyo wakati wake.

27Tazama, haya tumeyapeleleza, ndivyo yalivyo;

Yasikie, uyajue, ili upate mema.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania