The chat will start when you send the first message.
1Je! Mtu hana huduma ngumu juu ya nchi?[#Ayu 14:5,13,14; Zab 39:4; Mhu 3:1,2]
Na siku zake, je! Si kama siku za mwajiriwa?
2Kama mtumishi atamaniye sana kile kivuli,
Kama mwajiriwa anayetazamia mshahara wake;
3Hivyo basi nami nimepewa miezi ya ubatili iwe fungu langu,[#Zab 39:5; Mhu 1:14]
Nami nimeandikiwa mateso usiku hata usiku.
4Hapo nilalapo chini, nasema,
Nitaondoka lini? Lakini usiku huwa mrefu;
Nami nimejawa na kujitupa huku na huku hata kupambazuke.
5Mwili wangu unavikwa mabuu na madongoa ya udongo;[#Ayu 17:14; Zab 38:5-7; Isa 1:6]
Ngozi yangu hufumba, kisha ikatumbuka tena.
6Siku zangu hupita upesi kuliko chombo cha kufumia,
Nazo zapita pasipokuwa na matumaini.
7Kumbuka ya kwamba maisha yangu ni upepo;[#Zab 78:39; Yak 4:14]
Jicho langu halitaona mema tena.
8Jicho lake huyo anionaye halitaniangalia tena;[#Ayu 20:9]
Macho yako yatanielekea, lakini sitakuwapo.
9Kama vile wingu likomavyo na kutoweka,[#2 Sam 12:23; Zab 39:13]
Ndivyo alivyo huyo ashukaye kuzimuni, hatazuka tena kabisa.
10Hatarudi tena nyumbani kwake,
Wala mahali pake hapatamjua tena.
11Kwa hiyo sitakizuia kinywa changu;[#Zab 39:1,9]
Nitanena kwa mateso ya roho yangu;
Nitalia kwa uchungu wa nafsi yangu.
12Je! Mimi ni bahari, au je! Ni nyangumi?
Hata ukawaweka walinzi juu yangu?
13Hapo nisemapo, kitanda changu kitanituliza moyo,
Malazi yangu yatanipunguzia kuugua kwangu;
14Ndipo unitishapo kwa ndoto,
Na kunitia hofu kwa maono;
15Hata nafsi yangu huchagua kunyongwa,
Na kuchagua kifo kuliko maumivu yangu haya.
16Ninadhoofika; sitaishi siku zote;[#Mwa 27:46; Ayu 10:1; Zab 62:9; Mhu 6:11]
Usinisumbue, kwani siku zangu ni uvuvio.
17Je! Mtu ni kitu gani, hata ukamtukuza,[#Zab 8:4; 144:3; Ebr 2:6]
Na kumtia moyoni mwako,
18Na kumwangalia kila asubuhi,
Na kumjaribu kila dakika?
19Je! Hata lini hukomi kuniangalia;
Wala kunisumbua hata nimeze mate?
20Ikiwa nimefanya dhambi, nikufanyieje, Ee mlinda wanadamu?[#Zab 36:6]
Mbona umeniweka niwe shabaha yako,
Hata nimekuwa mzigo kwa nafsi yangu?
21Nawe, je! Mbona hunisamehe makosa yangu,
Na kuniondolea maovu yangu?
Kwa kuwa sasa nitalala mavumbini;
Nawe utanitafuta kwa bidii, lakini sitakuwapo.