The chat will start when you send the first message.
1Neno la BWANA lililomjia Yoeli, mwana wa Pethueli.[#Ebr 1:1; 2 Pet 1:21]
2Sikilizeni haya, enyi wazee;[#Kum 4:32; Isa 7:17; Dan 12:1; Yoe 2:2; Mt 24:21]
Sikilizeni, enyi wenyeji wote wa nchi.
Je! Mambo haya yamekuwako katika siku zenu,
Au katika siku za baba zenu?
3Waambieni watoto wenu habari yake,[#Zab 78:4]
Watoto wenu wakawaambie watoto wao,
Na watoto wao wakakiambie kizazi kingine.
4Yaliyosazwa na tunutu yameliwa na nzige; na yaliyosazwa na nzige yameliwa na parare; na yaliyosazwa na parare yameliwa na madumadu.
5Levukeni, enyi walevi, mkalie;[#Isa 32:10]
Pigeni yowe, ninyi nyote mnywao divai;
Kwa sababu ya divai mpya;
Maana umekatiliwa mbali na vinywa vyenu.
6Maana taifa limepanda juu ya nchi yangu,[#Mit 30:25; Ufu 9:8]
Lenye nguvu, tena halina hesabu;
Meno yake ni kama meno ya simba,
Naye ana magego ya simba mkubwa.
7Ameuharibu mzabibu wangu; ameuvunja mtini wangu; ameyaambua magamba yake kabisa; ameuangusha chini; matawi yake yamefanywa kuwa meupe.[#Isa 5:6]
8Omboleza kama mwanamwali avaaye magunia[#Isa 22:12; Mit 2:17]
Kwa ajili ya mume wa ujana wake.
9Sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji[#Yoe 2:14]
Zimekatiliwa mbali na nyumba ya BWANA;
Hao makuhani, wahudumu wa BWANA, wanaomboleza.
10Shamba limeharibika, nchi inaomboleza; maana nafaka imeharibika, divai mpya imekauka, mafuta yamepunguka.[#Yer 12:11; Isa 24:7]
11Tahayarini, enyi wakulima;[#Yer 14:3]
Pigeni yowe, enyi watunzaji wa mizabibu;
Kwa ajili ya ngano na shayiri,
Maana mavuno ya mashamba yamepotea.
12Mzabibu umesinyaa, mtini nao umevia;[#Isa 9:3; Yer 48:33; Hos 9:1,2]
Nao mkomamanga na mtende na mtofaa;
Naam, miti yote ya mashamba imekauka;
Maana furaha imetoweka kwa wanadamu.
13Jikazeni mkaomboleze, enyi makuhani;[#Yer 4:8]
Pigeni yowe, enyi wahudumu wa madhabahu;
Njooni mlale usiku kucha katika magunia,
Enyi wahudumu wa Mungu wangu;
Kwa kuwa sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji
Zimezuiwa katika nyumba ya Mungu wenu.
14Takaseni saumu, iteni kusanyiko la dini,[#2 Nya 20:3,13]
Wazee na wakusanye wenyeji wote wa nchi;
Waende nyumbani kwa BWANA, Mungu wenu,
Na kumlilia BWANA,
15Ole wake siku hii![#Yer 30:7; Yoe 2:3; Amo 5:16-18; Isa 13:6]
Kwa maana siku ya BWANA inakaribia, nayo itakuja kama maangamizi yatokayo kwake aliye Mwenyezi.
16Je! Chakula hakikukatiliwa mbali mbele ya macho yetu? Naam, furaha na kicheko mbali na nyumba ya Mungu wetu?[#Kum 12:7,12; 16:11]
17Mbegu zinaoza chini ya udongo wake; mabohari yameachwa ukiwa; ghala zimeharibika; kwa maana nafaka imekauka.
18Jinsi wanyama wanavyougua! Makundi ya ng'ombe yamefadhaika, kwa sababu hawana malisho; naam, makundi ya kondoo yamehangaika.[#1 Fal 18:5; Hos 4:3]
19Ee BWANA, nakulilia wewe;
Kwa maana moto umeyala malisho ya nyikani,
Na miali ya moto imeteketeza miti yote ya mashamba.
20Naam, hata wanyama pori wanakulilia wewe;[#Ayu 38:41; Zab 104:31; 1 Fal 17:7]
Kwa maana vijito vya maji vimekauka,
Na moto umeyateketeza malisho ya nyikani.