Zaburi 12

Zaburi 12

Ombi la msaada wakati wa dhiki

1Tuokoe, ee BWANA, maana hamna tena amchaye Mungu[#Isa 57:1]

Maana waaminifu wametoweka katika wanadamu.

2Husemezana yasiyofaa kila mtu na mwenziwe,

Wenye midomo ya kujipendekeza;

Husemezana kwa mioyo ya unafiki;

3BWANA ataikata midomo yote ya kujipendekeza,

Na ulimi unenao maneno ya kiburi;

4Waliosema, Kwa ndimi zetu tutashinda;

Midomo yetu ni yetu wenyewe,

Ni nani aliye bwana juu yetu?

5Kwa ajili ya kuonewa kwao wanyonge,[#Kut 3:7,8]

Kwa ajili ya kuugua kwao wahitaji,

Sasa nitasimama, asema BWANA,

Nitamweka salama yeye wanayemfyonya.

6Maneno ya BWANA ni maneno safi,[#2 Sam 22:31; Zab 18:30; Mit 30:5]

Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi;

Iliyosafishwa mara saba.

7Wewe, BWANA, ndiwe utakayetuhifadhi,

Utatulinda na kizazi hiki milele.

8Wasio haki hutembea pande zote,

Huku ufisadi ukitukuka kati ya wanadamu.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania