Warumi 4

Warumi 4

Mfano wa Abrahamu

1Basi, tusemeje juu ya Abrahamu, baba yetu kwa jinsi ya mwili?

2Kwa maana ikiwa Abrahamu alihesabiwa haki kwa ajili ya matendo yake, analo la kujisifia; lakini si mbele za Mungu.

3Maana Maandiko yasemaje? Abrahamu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki.[#Mwa 15:6; Gal 3:6; Yak 2:23]

4Lakini kwa mtu afanyaye kazi, ujira wake hauhesabiwi kuwa ni neema, bali kuwa ni deni.[#Rum 11:6; Mt 20:7,14]

5Lakini kwa mtu asiyefanya kazi, bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtauwa, imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki.

6Kama vile Daudi ainenavyo heri yake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na haki pasipo matendo,[#Zab 32:1,2]

7Heri waliosamehewa makosa yao,[#Zab 32:1-2]

Na waliositiriwa dhambi zao.

8Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi.

9Basi je! Heri hiyo ni kwa hao waliotahiriwa, au kwa hao pia wasiotahiriwa? Kwa kuwa tunanena ya kwamba kwake Abrahamu imani yake ilihesabiwa kuwa ni haki.[#Mwa 15:6]

10Alihesabiwaje basi? Alipokwisha kutahiriwa, au kabla hajatahiriwa? Si baada ya kutahiriwa, bali kabla ya kutahiriwa.

11Naye aliipokea dalili hii ya kutahiriwa, mhuri wa ile haki ya imani aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa; apate kuwa baba yao wote waaminio, ijapokuwa hawakutahiriwa, ili na wao pia wahesabiwe haki;[#Mwa 17:10,11]

12tena awe baba wa kutahiriwa, kwa wale ambao si waliotahiriwa tu, bali pia wanazifuata nyayo za imani yake baba yetu Abrahamu aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa.[#Mt 3:9; 1 Pet 2:21; 2 Kor 12:18]

Ahadi ya Mungu yatimizwa kwa imani

13Kwa maana ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Abrahamu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa imani.[#Mwa 17:4-6; 22:17-18; Gal 3:29]

14Maana ikiwa wale wa sheria ndio warithi, imani imekuwa bure, na ahadi imebatilika.[#Gal 3:18]

15Kwa sababu sheria ndiyo ifanyayo hasira; maana pasipokuwapo sheria, hapana kosa.[#Rum 3:20; 5:13; 7:8,10]

16Kwa hiyo ilitoka katika imani, iwe kwa njia ya neema, ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazawa wote; si kwa wale wa torati tu, ila na kwa wale wa imani ya Abrahamu; aliye baba yetu sisi sote;[#Gal 3:7]

17(kama ilivyoandikwa, Nimekuweka kuwa baba wa mataifa mengi); mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako.[#Mwa 17:5; Isa 48:13]

18Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.[#Mwa 15:5]

19Yeye asiyekuwa dhaifu wa imani, alifikiri hali ya mwili wake uliokuwa umekwisha kufa, (akiwa amekwisha kupata umri wa kama miaka mia moja), na hali ya utasa wa tumbo lake Sara.[#Mwa 17:17; #4:19 Katika Kigiriki ni ‘hali ya kufa ya tumbo lake Sara’.]

20Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutoamini, bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza Mungu;[#Ebr 11:7,11,34]

21huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi.

22Kwa hiyo ilihesabiwa kwake kuwa ni haki.[#Mwa 15:6]

23Lakini haikuandikwa kwa ajili yake tu kwamba ilihesabiwa kwake;[#Rum 15:4]

24bali na kwa ajili yetu sisi mtakaohesabiwa vivyo hivyo, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu katika wafu;[#1 Pet 1:21]

25ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki.[#Isa 53:4-5; 1 Kor 15:17]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania