The chat will start when you send the first message.
1Hekima ilimlinda hata mwisho yule mtu wa kwanza, baba wa ulimwengu, aliyehulukiwa peke yake; akamponya katika kosa lake mwenyewe,[#Mwa 1:26-28]
2na kumpa uwezo wa kujipatia amri juu ya vitu vyote.
3Lakini yule mwenye hatia alipojitenga nayo katika hasira yake aliangamia mwenyewe katika ghadhabu, ambayo katika hiyo alimwua nduguye.[#Mwa 4:8-13]
4Na hapo kwa ajili yake dunia ilipokuwa ikifurikishwa na gharika, mara ya pili Hekima ilileta wokovu, kwa kumwongoza yule mtu wa haki katika njia yake kwa kipande dhaifu cha mti.[#Mwa 7:1–8:22]
5Aidha, mataifa walipoafikiana katika uovu, wakachafuliwa ndimi zao, Hekima ilimtambua yule mtu mwaminifu, na kumhifadhi katika unyofu wake mbele za Mungu, ikamthibitisha wakati ule moyo wake ulipomwonea shauku mwanawe.[#Mwa 11:1-9; 12:1-3; 22:1-19]
6Aidha, pindi walipokuwa wakiangamizwa wale wabaya, Hekima ilimponya yule mtu mwenye haki, ambaye alikimbia kutoka moto ulioshuka mbinguni juu ya ile miji mitano;[#Mwa 19:1-29]
7na hata sasa maganjo yatokayo moshi ni ushuhuda wa ubaya wao, pia na mimea inayozaa matunda mazuri yasiyoiva kamwe. Naam, hata na roho isiyoamini inalo kumbukumbu lake huko, yaani nguzo ya chumvi iliyoko leo.
8Maana hao walioiomba Hekima walidhoofika, hata wasiweze kuyatambua yaliyo mema; na zaidi ya hayo waliacha nyuma yao, kwa faida ya maisha ya kibinadamu, kumbukumbu la upumbavu wao; ili makusudi walivyokengeua wasikose kutambulikana.
9Walakini Hekima iliwaponya katika shida zao wale waliongoja kwa saburi.
10Aidha, hapo yule mwenye haki alipokimbia mbele ya hasira ya nduguye, Hekima ilimwongoza katika njia sawa; ikamwonesha ufalme wa Mungu, na kumjulisha mambo matakatifu; ikimfanikisha katika taabu zake, na kumzidishia mazao ya kazi zake;[#Mwa 27:43; 28:10-22; 32:24-30]
11tena, watu walipomwonelea kwa sababu ya ubahili wao, ikasimama upande wake na kumtajirisha;
12ikamlinda na adui zake, na kumhifadhi salama kati yao waliomwotea; mfano wa mwamuzi ikaangalia pigano lake kuu; ili afahamu ya kwamba utauwa una nguvu kupita mambo yote.
13Aidha, alipouzwa yule mwenye haki Hekima haikumwacha, ila ilimwokoa na kutenda dhambi;[#Mwa 37:12-36; 39:1-23; 41:37-44]
14ikateremka pamoja naye hata gerezani, wala vifungo havikumwondoka, hata ilipomletea fimbo ya enzi ya ufalme, na amri juu yao waliomdhulumu; ikaudhihirisha uongo wao waliomshitaki kwa dhihaka, na kumjalia yeye mwenyewe utukufu wa milele.
15Hekima nayo iliwaokoa watu watakatifu, wazao wasio na hatia, mikononi mwa lile taifa dhalimu.[#Kut 1:1–15:21]
16Ikaingia katika roho yake yule mtumishi wa BWANA, naye akawapinga wafalme wenye kutisha kwa maajabu na ishara.
17Ikawajazi wale watu watakatifu malipo ya kazi zao za taabu; ikawaongoza wapitie njia ya ajabu; ikawa kwao kifuniko wakati wa mchana, na mwako wa nyota wakati wa usiku.
18Ikawavusha penye Bahari ya Shamu, na kuwaongoza panapo maji mengi;
19lakini ikawatosa adui zao, na kuwatupa ufuoni kutoka chini ya vilindi.
20Kwa hiyo wenye haki waliwateka wasio haki wakaimba nyimbo za kulihimidi jina lako, BWANA, na kuutukuza kwa umoja mkono wako uliowapigania;
21kwa sababu Hekima ilikifumbua hata kinywa cha bubu, na kuzinenesha vizuri ndimi zao waliokuwa wachanga.