The chat will start when you send the first message.
1Hapo ndipo mwenye haki atakaposimama kwa ujasiri mwingi mbele ya nyuso zao waliomtesa, na wale waliozidharau kazi zake.
2Nao wayaonapo hayo watafadhaishwa kwa hofu ya kutisha, na kuishangaa ajabu ya wokovu wa Mungu.
3Ndipo watakaposema nafsini mwao, kwa kutubu na kuugua kwa sababu ya dhiki ya roho zao,
4Huyu ndiye yule tuliyemcheka sana zamani, kumfanya mithali ya kushutumu; sisi tulio wajinga tukahesabu ya kuwa maisha yake ni wazimu, na kikomo chake aibu.
5Amepataje huyu kuhesabiwa pamoja na wana wa Mungu, na sehemu yake pamoja na watakatifu?
6Hakika tulikengeuka katika njia ya kweli; wala nuru ya haki haikutuangaza, wala jua lake halikutuchomozea.
7Tukashiba njia za uasi na uharibifu, tukapitia majangwani pasina njia, tusiifahamu njia ya BWANA.
8Basi kiburi chetu kimetufaa nini? Au tumepata faida gani kwa utajiri na majivuno?
9Hayo yote yalipita kama kivuli, mfano wa tarishi aendaye mbio;
10kama jahazi ikatayo mawimbi yaumkayo, nayo ikiisha kupita dalili yake haionekani, wala mwendo wa mkuku wake mawimbini;
11kama vile ndege arukavyo angani, wala haionekani alama ya njia yake, ila hewa nyepesi yapenyeka ikipigwapigwa kwa mbawa zake, na kupasuliwa kwa nguvu ya kuruka kwake, na kwa kutikiswa kwa manyoya yake, isionekane baadaye alama yoyote ya kupita kwake;
12kama na mshale wa mpiga shabaha, panapo hewa hupasuliwa ikafumbika tena mara, hata watu wasitambue ulipopita.
13Vivyo hivyo na sisi mara tulipozaliwa tulitoweka; tusiweze kuonesha hata dalili moja ya wema, lakini katika uovu wetu tukaangamizwa kabisa.
14Kwa kuwa matumaini yake mtu mwovu huwa kama makapi yapeperushwayo na upepo, na kama tandabui laini ichukuliwayo mbele ya tufani; hutawanyika kama moshi urushwao kwa upepo, kama ukumbusho wa mgeni ashindaye siku moja tu.
15Bali wenye haki waishi milele, na thawabu yao i katika BWANA, na kutunzwa kwao kumekuwa kwake Yeye Aliye Juu.
16Kwa hiyo watapokea mkononi mwa BWANA taji la kifalme na kilemba cha uzuri; kwa maana yeye atawafunika kwa mkono wa kuume, na kwa mkono wake hodari atawalinda kama kwa ngao.
17Ghera yake ataifanya kuwa zana za vita, na jamii ya viumbe kuwa silaha zake, ajilipize kisasi juu ya adui zake.[#Efe 6:11-17]
18Atavaa haki kama deraya, na kujivika hukumu isiyo na unafiki mfano wa chapeo;
19utakatifu utamwia ngao imara,
20naye atanoa hasira kali kuwa upanga. Na ulimwengu wote pia utaondoka pamoja naye kupigana na adui zake wasio na akili.
21Kutoka mawingu, kama kutoka kwa upinde uliopindwa sawasawa, umeme utaruka moja kwa moja kupiga shabaha;
22mvua ya mawe imejaa ghadhabu itatupwa kwa nguvu kama kutoka kwa manati ya vita; maji ya bahari yatafurika kwa hasira juu yao, na mito itawaangamiza bila huruma;
23kinyamkera kitawakuta na kuwapeperusha mithili ya kimbunga. Hivyo uasi utafanya nchi yote kuwa ukiwa, na udhalimu wao utavipindua hata vita vya enzi vya wafalme.