Zekaria 13

Zekaria 13

1Katika siku hiyo watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, watafunguliwa chemchemi ya kuwatakasa dhambi na unajisi.[#Isa 1:16,17; Yn 1:29; 1 Kor 6:11; Ebr 9:14; 1 Pet 1:19; 1 Yoh 1:7; Ufu 1:5]

Kuabudu sanamu kwakatiliwa mbali

2Kisha itakuwa katika siku hiyo, asema BWANA wa majeshi, nitakatilia mbali majina ya sanamu katika nchi, yasikumbukwe tena; pia nitawafukuza manabii, na roho ya uchafu, watoke katika nchi.[#Kut 23:13; 2 Pet 2:1]

3Tena itakuwa ya kwamba, mtu awaye yote atakapotoa unabii, basi baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia, Hutaishi; kwa maana unanena maneno ya uongo kwa jina la BWANA; na baba yake na mama yake waliomzaa watamtambua atoapo unabii.[#Kum 13:6]

4Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba manabii, kila mmoja wao, atayaonea haya maono yake atoapo unabii; wala hawatavaa joho la nywele ili kudanganya watu;

5bali atasema, Mimi si nabii kamwe; mimi ni mkulima wa nchi; kwa maana nilifanywa mtumwa tokea ujana wangu.

6Na mtu yeyote akimwuliza, Je! Majeraha haya yote uliyo nayo katikati ya mikono yako ni nini? Naye atajibu, Ni majeraha niliyotiwa katika nyumba ya rafiki zangu.

Mchungaji apigwa na kundi kutawanyika

7Amka, Ee upanga, juu ya mchungaji wangu, na juu ya mtu aliye mwenzangu, asema BWANA wa majeshi; mpige mchungaji, nao kondoo watatawanyika; nami nitaugeuza mkono wangu juu ya wadogo.[#Isa 40:11; 53:4-6; Ebr 13:20; Yn 10:30; 1:29; Lk 12:32; Mt 26:31; Mk 14:27]

8Hata itakuwa, ya kwamba katika nchi yote mafungu mawili yatakatiliwa mbali, nao watakufa, asema BWANA; lakini fungu la tatu litabaki humo.[#Rum 11:5]

9Nami nitalileta fungu lile la tatu na kulipitisha kati ya moto, nami nitawasafisha kama fedha isafishwavyo, nami nitawajaribu kama dhahabu ijaribiwavyo; wataliitia jina langu, nami nitawasikia; mimi nitasema, Watu hawa ndio wangu; nao watasema, BWANA ndiye Mungu wangu.[#Isa 48:10; Zab 66:10; Mal 3:4; 1 Pet 1:6,7; Ufu 2:10]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania