Sira 5

Sira 5

Usiwe na majivuno

1Usitegemee mali zako,

wala usiseme, “Nina mali ya kutosha.”

2Usiongozwe na tamaa yako na nguvu yako,

katika kufuata tamaa za moyo wako.

3Usiseme, “Nani atanishinda?”

maana hakika Bwana atakuadhibu.

4Usiseme, “Nimetenda dhambi, lakini nimepata balaa gani?”

maana Bwana hakasiriki upesi.

5Usitegemee kupata msamaha,

hata kuongeza dhambi juu ya dhambi.

6Usiseme, “Huruma yake ni kubwa;

yeye atanisamehe dhambi zangu nyingi.”

Kumbuka, yeye ana huruma na ghadhabu,

na hasira yake huwakumba wenye dhambi.

7Usichelewe kumrudia Bwana,

wala usiahirishe kurudi siku hata siku.

Maana ghadhabu ya Bwana itakuwakia ghafla,

na wakati wa hukumu utaangamia.

8Usitegemee mali ya udanganyifu;

maana haitakufaa chochote siku ya balaa.

Uaminifu na kujitawala

9Usipepete nafaka kwa kila upepo,

wala kufuata asemacho mtu:

Hiyo ndiyo desturi ya mwenye dhambi mdanganyifu.

10Uwe na msimamo thabiti katika nia yako,

na usiwe kigeugeu katika maneno yako.

11Uwe mwepesi kusikiliza,

lakini uwe mwangalifu katika kutoa jibu.

12Kama unajua jambo hilo, mjibu jirani yako,

la hujui, basi usijibu.

13Sifa na aibu vyote hutokana na kusema.

ulimi wa mtu waweza kumwangamiza.

14Usikubali kujipatia sifa kwa kuteta,

usikubali kusema kitakachowahatarisha wengine.

Maana kama vile aibu humjia mwizi,

ndivyo hukumu kali itakavyompata mdanganyifu.

15Usikosee katika jambo lolote kubwa au dogo,

wala usiwe adui pale unapotakiwa kuwa rafiki.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania