The chat will start when you send the first message.
1Waisiraeli wote wakamkusanyikia Dawidi huko Heburoni kumwambia: Tazama, sisi na wewe tu mifupa ya mmoja, nazo nyama za miili yetu ni za mmoja.[#1 Mose 29:14.]
2Napo hapo kale, Sauli alipokuwa mfalme bado, aliyewaongoza Waisiraeli kwenda na kurudi vitani ni wewe, naye Bwana Mungu wako alikuambia: Wewe utawachunga walio ukoo wangu wa Waisiraeli, nawe wewe utawatawala hao walio ukoo wangu wa Waisiraeli.
3Wazee wote wa Waisiraeli wakamjia mfalme huko Heburoni, Dawidi akafanya agano nao huko Heburoni mbele ya Bwana, wakampaka Dawidi mafuta, awe mfalme wao Waisiraeli, kama Bwana alivyosema kinywani mwa Samweli.[#1 Sam. 16:1,3,12.]
4Kisha Dawidi na Waisiraeli wote wakaenda Yerusalemu, ndio Yebusi, nao Wayebusi hapo walikuwa bado wenyeji wa nchi hiyo.
5Nao waliokaa Yebusi wakamwambia Dawidi: Humu hutaingia kabisa! Lakini Dawidi akaliteka boma la Sioni, ndio mji wa Dawidi.
6Dawidi akasema: Ye yote atakayekuwa wa kwanza wa kuwapiga Wayebusi atakuwa mkuu wa kwanza wa vikosi. Ndipo, Yoabu, mwana wa Seruya, alipopanda wa kwanza, akawa mkuu.
7Dawidi akakaa mle bomani, kwa hiyo likaitwa mji wa Dawidi.
8Akaujenga huo mji pande zote za kuuzunguka toka Milo; naye Yoabu akaujenga huo mji kuwa mpya pengine po pote.
9Dawidi akaendelea kuwa mkuu, kwa sababu Bwana Mwenye vikosi alikuwa naye.
10Hawa ndio wakuu wao mafundi wa vita, Dawidi aliokuwa nao, waliomsaidia kwa nguvu zao, apate ufalme; nao Waisiraeli wote walikuwa upande wao, walipomfanya kuwa mfalme, kama Bwana alivyowaambia Waisiraeli.
11Hii ndiyo hesabu yao mafundi wa vita, Dawidi aliokuwa nao: Yasobamu, mwana wa Hakemoni, mkuu wa thelathini; yeye aliuchezesha mkuki wake juu ya watu 300 waliouawa naye kwa mara moja.[#1 Mambo 27:2.]
12Aliyemfuata ni Elazari, mwana wa Dodo, wa Ahohi, huyu alikuwa mmoja wao wale mafundi wa vita watatu.[#1 Mambo 27:4.]
13Huyu alikuwa pamoja na Dawidi huko Pasi-Damimu, Wafilisti walipokusanyika huko kupigana naye. Huko kulikuwa na kipande cha shamba lenye mawele; hapo, watu walipowakimbia Wafilisti,
14ndipo, hawa walipokuja kusimama katikati ya hicho kipande cha shamba, wakakiponya wakiwapiga wafilisti; ndivyo, Bwana alivyowaokoa na kuwapatia wokovu mkubwa.
15Wakashuka wakuu watatu waliomo miongoni mwao wakuu wa thelathini, wafike gengeni kwa Dawidi penye pango la Adulamu; nayo makambi ya Wafilisti yalikuwa Bondeni kwa Majitu.[#1 Sam. 22:1.]
16Naye Dawidi siku zile alikuwa ngomeni, nacho kikosi cha walinzi wa Wafilisti kilikuwamo Beti-Lehemu.
17Hapo Dawidi akaingiwa na tamaa, akasema: Yuko nani atakayeninywesha maji ya kisima cha Beti-Lehemu, kilichoko langoni?
18Ndipo, wale watatu walipojipenyeza makambini mwa Wafilisti, wakachota maji katika kisima cha Beti-Lehemu kilichoko langoni, wakayachukua, wakamletea Dawidi, lakini Dawidi hakutaka kuyanywa, akammwagia Bwana kuwa kinywaji cha tambiko,
19akasema: Mungu wangu na anizuie, nisifanye kama hayo! Je? Ninywe damu za waume hawa waliojitoa wenyewe kwa ajili yao haya? Kwani wameyaleta haya kwa kujitoa wenyewe; kwa hiyo hakutaka kuyanywa. Hayo waliyafanya wale mafundi wa vita watatu.
20Naye Abisai, ndugu yake Yoabu, alikuwa mkuu miongoni mwa watu watatu; yeye ndiye aliyeuchezesha mkuki wake juu ya watu 300, ndio, aliowaua naye; akawa mwenye macheo kwa hao watatu.
21Kwao hao watatu aliheshimiwa kuliko wenzake wawili, akawa mkuu wao, lakini wale watatu wa kwanza hakuwa sawa nao.
22Benaya, mwana wa Yoyada, mwana wa mtu mwenye nguvu, alifanya matendo makuu, nako kwao kulikuwa Kabuseli. Yeye aliwaua wana wawili wa Arieli wa Moabu, tena siku moja, theluji ilipokuwa imeanguka, akashuka shimoni, akaua simba mlemle.
23Naye ndiye aliyemwua mtu wa Misri mwenye urefu wa mikono mitano aliyeshika mkononi mwake mkuki uliokuwa mzito kama majiti ya wafumaji; lakini akamshukia na kushika fimbo tu, akampokonya yule Misri mkuki mkononi mwake, akamwua kwa huo mkuki wake.[#1 Sam. 17:7,40,51.]
24Hayo aliyafanya Benaya, mwana wa Yoyada; kwa hiyo alipata macheo kwa hao mafundi wa vita watatu.[#1 Mambo 27:5-6.]
25Kwao hao thelathini aliheshimiwa yeye kuliko wenziwe, lakini wale watatu wa kwanza hakuwa sawa nao. Naye Dawidi akamweka kuwa mkuu wa walinzi wake.
26Mafundi wa vita wenye nguvu walikuwa hawa: Asaheli, ndugu yake Yoabu; Elihanani, mwana wa Dodo na Beti-Lehemu;
27Samoti wa Harori, Helesi wa Puloni,[#1 Mambo 27:8,10.]
28Ira, mwana wa Ikesi, wa Tekoa, Abiezeri wa Anatoti,
29Sibekai wa Husa, Ilai wa Ahohi,
30Maharai wa Netofa, Heledi, mwana wa Baana, wa Netofa,
31Itai, mwana wa Ribai, wa Gibea wa wana wa Benyamini, Benaya wa Paratoni,
32Hurai wa Nahale-Gasi, Abieli wa Araba,
33Azimaweti wa Bahurimu, Eliaba wa Salaboni,
34wana wa Hasemu wa Gizoni, Yonatani, mwana wa Sage, wa Harari,
35Ahiamu, mwana wa Sakari, wa Harari, Elifali, mwana wa Uri,
36Heferi wa Mekera, Ahia wa Puloni,
37Hesero wa Karmeli, Narai, mwana wa Ezibai,
38Yoeli, ndugu yake Natani, Mibuhari, mwana wa Hagri,
39Mwamoni Seleki, Naharai wa Beroti aliyekuwa mchukua mata wa Yoabu, mwana wa Seruya,
40Mwitiri Ira, Mwitiri Garebu,
41Mhiti Uria, Zabadi, mwana wa Alai,[#2 Sam. 11:3.]
42Adina, mwana wa Siza, wa Rubeni, aliyekuwa mkuu wao Warubeni mwenye watu 30,
43Hanani, mwana wa Maka, na Yosafati wa Meteni,
44Uzia wa Astera, Sama na Yieli, wana wa Hotamu wa Aroeri,
45Yediaeli, mwana wa Simuri, na nduguye Yoha wa Tisi,
46Mmahawimu Elieli na Yeribai na Yosawia, wana wa Elinamu, na Mmoabu Itima,
47Elieli na Obedi na Yasieli wa Soba.