1 Mambo 12

1 Mambo 12

Wapiga vita wa Dawidi.

1Hawa ndio waliomjia Dawidi huko Siklagi, alipokuwa amefukuzwa, asimtokee Sauli, mwana wa Kisi. Nao hao ndio mafundi wa vita waliomsaidia kupigana.[#1 Sam. 27:6.]

2Walishika pindi, nao walijua kutupa mawe kuumeni na kushotoni na kupiga mishale kwa pindi zao; nao walikuwa ndugu zake Sauli, maana ni Wabenyamini.[#1 Mambo 8:40.]

3Mkuu Ahiezeri na Yoasi, wana wa Hasemaa wa Gibea; na Yezieli na Peleti, wana wa Azimaweti, na Beraka na Yehu wa Anatoti,

4na Isimaya wa Gibeoni, ni mmoja wao wale mafundi wa vita thelathini, tena ni mkuu wao hao thelathini, na Yeremia na Yahazieli na Yohana na Yozabadi wa Gedera,

5Eliuzai na Yerimoti na Balia na Semaria na Sefatia wa Harifu;

6Elkana na Isia na Azareli na Yoezeri na Yasobamu waliokuwa Wakora;[#1 Mambo 25:18.]

7na Yoela na Zebadia, wana wa Yerohamu wa Gedori.

8Kwao Wagadi nako walikuwako waliojitenga kumjia Dawidi kule gengeni nyikani; nao walikuwa mafundi wa vita wenye nguvu, waume waliozoea kupigana, walishika ngao na mikuki, nyuso zao zilikuwa kama nyuso za simba, wakapiga mbio kama paa milimani.[#2 Sam. 2:18.]

9Mkuu Ezeri, wa pili Obadia, wa tatu Eliabu,

10wa nne Misimana, wa tano Yeremia,

11wa sita Atai, wa saba Elieli,

12wa nane Yohana, wa tisa Elizabadi,

13wa kumi Yeremia, wa kumi na moja Makibanai.

14Hawa Wagadi walikuwa wakuu wa vikosi, aliyekuwa mdogo kwao aliweza kushinda mia, naye mkubwa elfu.

15Hawa ndio waliovuka Yordani katika mwezi wa kwanza, mto ulipojaa na kuzifurikia kingo zake zote mbili, wakawafukuza wote waliokaa huko mabondeni upande wa maawioni kwa jua na machweoni kwa jua.

16Watu wengine wa Benyamini na wa Yuda walipomjia Dawidi pale gengeni pake,

17Dawidi akawatokea, akaanza kusema nao akiwaambia: Kama mnakuja kwangu kwa kunitakia mema, mnisaidie, basi, moyo wangu utafanya bia nanyi, tupatane; lakini kama mnataka kunichongea kwao wanaonisonga, ingawa ukorofi haumo mikononi mwangu, Mungu wa baba zetu na ayatazame, awapatilize!

18Ndipo, roho ilipomwingia Amasai aliyekuwa mkuu wa thelathini, akasema: Tu watu wako, Dawidi; tuko pamoja na wewe, mwana wa Isai. Tengemana, tengemana! Naye atakayekusaidia na atengemane! Kwani Mungu wako anakusaidia. Ndipo, Dawidi alipowapokea, akawapa kuwa wakuu wa vikosi.

19Hata kwa Wamanase walikuwako waliourudia upande wa Dawidi, alipomjia Sauli pamoja na Wafilisti kupigana naye, lakini hawakuwasaidia; kwani wakuu wa Wafilisti walikuwa wamefanya shauri, kwa hiyo walikuwa wamempa ruhusa kwa kumwazia kwamba: Atarudi kwa bwana wake Sauli na kumtolea vichwa vyetu.[#1 Sam. 29:4.]

20Kisha alipokwenda Siklagi, Wamanase hawa wakarudi upande wake: Adina na Yozabadi na Yediaeli na Mikaeli na Yozabadi na Elihu na Siltai, ndio wakuu wa vikosi vyenye watu elfu kwao Wamanase.

21Hawa wakamsaidia Dawidi kushindana na askari za adui, kwani wao wote walikuwa mafundi wa vita wenye nguvu, wakawa wakuu wa vikosi.

22Kwani siku hizo watu wakaja kwa Dawidi siku kwa siku, wamsaidie, mpaka wakiwa jeshi kubwa kama jeshi la Mungu.

23Hii ndiyo hesabu ya wakuu wao wapiga vita waliomjia Dawidi huko Heburoni wakishika mata yao, wampe ufalme wakiuondoa kwake Sauli, kama Bwana alivyosema:

24wana wa Yuda waliochukua ngao na mikuki, watu 6800 wenye mata ya kupigia vita.

25Wana wa Simeoni, mafundi wa vita wenye nguvu wajuao kupiga vita, watu 7100.

26Wana wa Lawi watu 4600,

27naye Yoyada, mkuu wao wa Haroni, tena pamoja naye watu 3700,

28naye Sadoki aliyekuwa kijana mwenye nguvu ya kupiga vita, namo mlangoni mwa baba yake wakatoka wakuu 22.[#1 Mambo 6:8; 2 Sam. 15:24.]

29Wana wa Benyamini waliokuwa ndugu zake Sauli, watu 3000; kwani mpaka hapo wengi wao walikuwa upande wa mlango wa Sauli na kuulindia.

30Wana wa Efuraimu, mafundi wa vita wenye nguvu, watu 20800, ni watu waliokuwa wenye macheo katika milango yao.

31Katika nusu ya shina la Manase wakatoka watu 18000 waliokuwa wameandikwa majina yao, waje, wamfanye Dawidi kuwa mfalme.

32Wana wa Isakari waliojua kuitambua maana ya siku walijua nayo yaliyowapasa Waisiraeli kufanya, kwa hiyo wakaja wakuu wao 200 nao ndugu zao wote kwa kuagizwa nao.

33Kwa Zebuluni vikatoka vikosi vya watu waliokuwa tayari kupiga vita kwa kushika vyombo vyote vya vitani, watu 50000 waliozoea kujipanga pasipo kupitana mioyo.

34Kwa Nafutali wakatoka wakuu 1000, tena pamoja nao watu 37000 wenye ngao na mikuki.

35Kwa Dani wakatoka waliokuwa tayari kupiga vita, watu 28600.

36Kwa Aseri watu wakatoka vikosi vizima kwa kuwa tayari kupiga vita, watu 40000.

37Ng'ambo ya Yordani kwa Rubeni na kwa Gadi na katika nusu ya shina la Manase vikatoka vikosi vyenye vyombo vyote vya vitani, watu 120000.

38Watu hawa wote wa vita waliojua kujipanga vema vitani wakaja Heburoni, mioyo yao ikiwa mmoja kabisa, wakataka kumfanya Dawidi kuwa mfalme wa Waisiraeli wote; nao Waisiraeli wote waliosalia kwao mioyo yao ilikuwa mmoja tu wakitaka kumfanya Dawidi kuwa mfalme.

39Wakawa huko pamoja na Dawidi wakila, wakinywa siku tatu, kwani ndugu zao waliwaandalia.

40Nao waliokaa karibu kwao kuzifikia nchi za Isakari na za Zebuluni na za Nafutali waliwaletea vyakula vikichukuliwa na punda na ngamia na nyumbu na ng'ombe, vilikuwa vilaji vya unga na maandazi ya kuyu na ya zabibu na mvinyo na mafuta na ng'ombe na mbuzi na kondoo wengi, kwa kuwa ilikuwako furaha kwao Waisiraeli.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania