1 Mambo 13

1 Mambo 13

Dawidi anakwenda kulichukua Sanduku la Agano.

(Taz. 2 Sam. 6:1-11.)

1Dawidi akafanya shauri nao wakuu wa maelfu na wakuu wa mamia na watawalaji wote,

2kisha Dawidi akauambia mkutano wote wa Waisiraeli: Mkiona kuwa vema, tena vikiwa vimetoka kwake Bwana Mungu wetu, na tutume pande zote po pote kwa ndugu zetu waliosalia katika nchi zote za Isiraeli, hata kwa watambikaji na kwa Walawi katika miji yao, wanamokaa, kuwaambia, wakusanyike kwetu,

3twende kulichukua Sanduku la Mungu wetu, tulirudishe kwetu, kwani siku za Sauli hatukulitafuta.

4Watu wote wa huo mkutano wakaitikia, wafanye hivyo, kwa kuwa neno hilo lilikuwa limenyoka machoni pao watu wote.

5Kwa hiyo Dawidi akawakusanya Waisiraeli wote toka Sihori katika Misri hata kufika Hamati, waje kulichukua Sanduku la Mungu huko Kiriati-Yearimu.

6Kisha Dawidi na Waisiraeli wote wakapanda kwenda Bala, ndio Kiriati-Yearimu ulio mji wa Yuda, kulichukua huko Sanduku la Mungu Bwana akaaye juu ya Makerubi, kwa maana hili liliitwa kwa Jina lake.[#Yos. 15:9.]

7Wakalipandisha Sanduku la Mungu katika gari jipya wakilitoa katika nyumba ya Abinadabu, nao Uza na Ayo wakaliendesha hilo gari.

8Dawidi mwenyewe na Waisiraeli wote wakalitangulia na kucheza mbele ya Mungu kwa nguvu zote na kumwimbia pamoja na kupiga mazeze na mapango na patu na matoazi na matarumbeta.

9Walipofika pa kupuria pake Kidoni, Uza akapeleka mkono, alishike Sanduku, kwa kuwa ng'ombe walijikwaa.

10Ndipo, makali ya Bwana yalipomwakia Uza, akampiga, kwa kuwa amelipelekea hilo Sanduku mkono wake, akafa papo hapo mbele ya Mungu.

11Hapo Dawidi akaingiwa na uchungu, ya kuwa Bwana amempiga Uza pigo kama hilo, wakapaita mahali pale Peresi-Uza (Pigo la Uza) mpaka siku hii ya leo.

12Siku hiyo Dawidi akashikwa na woga wa kumwogopa Mungu kwamba: Nitawezaje kuliingiza Sanduku la Mungu kwangu?

13Kwa hiyo Dawidi hakuliingiza Sanduku hilo kwake mjini kwa Dawidi, akashika njia nyingine, akaliweka nyumbani mwa Obedi-Edomu wa Gati.

14Humo nyumbani mwa Obedi-Edomu Sanduku la Mungu likakaa kwenye mlango wake miezi mitatu, naye Bwana akaubariki mlango wa Obedi-Edomu nayo yote yaliyokuwa yake.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania