1 Mambo 14

1 Mambo 14

Dawidi anajijengea nyumba. Wakeze na wanawe.

(1-16: 2 Sam. 5:11-25.)

1Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Dawidi na miti ya miangati na waashi na maseremala, wamjengee Dawidi nyumba.

2Ndipo, Dawidi alipojua, ya kuwa Bwana amemweka kweli kuwa mfalme wao Waisiraeli, kwani ufalme wake ukaja kutukuka zaidi kwa ajili ya ukoo wake wa Waisiraeli.

3Kisha Dawidi akachukua wanawake wengine mle Yerusalemu, Dawidi akazaa tena wana wa kiume na wa kike.

4Haya ndiyo majina ya wana, waliozaliwa Yerusalemu: Samua na Sobabu, Natani na Salomo,

5Ibuhari na Elisua na Elpeleti,

6na Noga na Nefegi na Yafia,

7na Elisama na Beliada na Elifeleti.

Dawidi anawashinda Wafilisti.

8Wafilisti waliposikia, ya kuwa Dawidi amepakwa mafuta, awe mfalme wao Waisiraeli wote, ndipo, Wafilisti wote walipopanda kumtafuta Dawidi. Dawidi alipovisikia akatoka kukutana nao.

9Wafilisti wakaja, wakajieneza Bondeni kwa Majitu.

10Dawidi akamwuliza Mungu kwamba: Nikipanda kupigana na Wafilisti, utawatia mkononi mwangu? Bwana akamwambia: Panda! Nitawatia mkononi mwako.

11Ndipo, walipopanda Baali-Perasimu; Dawidi alipowapiga huko, akasema yeye Dawidi: Mungu amewaatua adui zangu kwa nguvu ya mkono wangu, kama maji yanavyoatua ukingo. Kwa sababu hii wakapaita mahali pale Baali-Perasimu (Maatuko).

12Kwa kuwa wale waliiacha huko miungu yao, Dawidi akaagiza iteketezwe kwa moto.[#5 Mose 7:5,25.]

13Lakini Wafilisti wakapanda tena na kujieneza bondeni kulekuke.

14Naye Dawidi alipomwuliza Mungu tena, Mungu akamwambia: Usipande kuwafuata, ila uzunguke hapo, walipo, upate kuwajia ukitoka juu, misandarusi iliko.

15Hapo, utakaposikia vileleni kwa misandarusi shindo kama ya watu wapitao, basi, hapo watokee kupigana nao! Kwani ndipo, Mungu atakapotokea, akutangulie kuyapiga majeshi ya Wafilisti.

16Dawidi akafanya, kama Mungu alivyomwagiza, wakayapiga majeshi ya Wafilisti toka Gibeoni hata Gezeri.

17Jina lake Dawidi likaenea katika nchi zote, Bwana akawatia wamizimu wote woga wa kumwogopa.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania