1 Mambo 15

1 Mambo 15

Sanduku la Agano linapelekwa Yerusalemu.

1Dawidi akajijengea nyumba mjini mwake, nalo Sanduku la Mungu akalitengenezea mahali na kulipigia hema.

2Kisha Dawidi akasema: Sanduku la Mungu asilichukue mtu, wasipokuwa Walawi, kwani ndio, Bwana aliowachagua kulichukua Sanduku la Mungu na kumtumikia kale na kale.

3Dawidi akawakusanya Waisiraeli wote mle Yerusalemu, walipandishe Sanduku la Bwana na kuliweka mahali pake, alipolitengenezea.

4Dawidi akawakusanya wana wa Haroni na Walawi,

5kwao wana wa Kehati: mkuu Urieli na ndugu zake, watu 120;

6kwao wana wa Merari: mkuu Asaya na ndugu zake, watu 220;

7kwao wana wa Gersomu: mkuu Yoeli na ndugu zake, watu 130;

8kwao wana wa Elisafani: mkuu Semaya na ndugu zake, watu 200;

9kwao wana wa Heburoni: mkuu Elieli na ndugu zake, watu 80;

10kwao wana wa Uzieli: mkuu Aminadabu na ndugu zake, watu 112.

11Kisha Dawidi akawaita watambikaji Sadoki na Abiatari na Walawi Urieli, Asaya na Yoeli, Semaya na Elieli na Aminadabu,[#2 Sam. 15:29.]

12akawaambia: Ninyi m wakuu wa milango ya Walawi, jitakaseni ninyi na ndugu zenu! Kisha mtalipandisha Sanduku la Bwana Mungu wa Isiraeli na kuliweka mahali pake, nilipolitengenezea.

13Kwa kuwa mara ya kwanza hamkuwako. Bwana Mungu wetu akatupiga pigo, kwa kuwa hatukumtafuta kwa njia itupasayo.[#1 Mambo 13:9-10.]

14Watambikaji na Walawi wakajitakasa, wapate kulipandisha Sanduku la Bwana Mungu wa Isiraeli.

15Walawi wakalichukua Sanduku la Mungu kwa kuweka mipiko mabegani pao, kama Mose alivyoagiza kwa kuambiwa na Bwana.[#2 Mose 25:14; 4 Mose 4:15.]

16Kisha Dawidi akawaambia wakuu wa Walawi, wawapange ndugu zao waimbaji, wakivishika vyombo vyao vya kuimbia: mapango na mazeze na matoazi, wapige shangwe na kuzipaza sauti kwa furaha.

17Ndipo, Walawi walipowapanga: Hemani, mwana wa Yoeli, na kwa ndugu zake: Asafu, mwana wa Berekia, na kwa wana wa Merari walio ndugu zao: Etani, mwana wa Kusaya.

18Pamoja nao wakawapanga ndugu zao wa uzao wa pili: Zakaria, Beni na Yazieli, na Semiramoti na Yehieli na Uni, Eliabu na Benaya na Masea na Matitia na Elifelehu na Mikinea na Obedi-Edomu na Yieli waliokuwa walinda malango.

19nao waimbaji Hemani, Asafu na Etani walioshika matoazi ya shaba, wayavumishe,[#1 Mambo 6:33,39,44; 25:1.]

20na Zakaria na Azieli na Semiramoti na Yehieli na Uni na Eliabu na Masea na Benaya walioshika mapango, waimbe sauti za juu;

21na Matitia na Elifelehu na Mikinea na Obedi-Edomu na Yieli na Azazia walioshika mazeze, waimbe sauti za chini na kuwaongoza wengine.

22Kenania, mkuu wa Walawi, aliyewaimbisha akawasimamia, walipoimba, kwani aliijua kazi hiyo.

23Naye Berekia pamoja na Elkana wakayangoja malango penye Sanduku la Agano.

24Nao watambikaji Sebania na Yosafati na Netaneli na Amasai na Zakaria na Benaya na Eliezeri wakalitangulia Sanduku la Mungu na kupiga matarumbeta, nao Obedi-Edomu na Yehia wakayalinda malango penye sanduku hilo.

(25-29: 2 Sam. 6:12-16.)

25Ndivyo, Dawidi na wazee wa Waisiraeli na wakuu wa maelfu walivyokwenda kulipandisha Sanduku la Agano la Bwana wakilitoa nyumbani mwa Obedi-Edomu kwa furaha.

26Kwa sababu Mungu aliwasaidia Walawi waliolichukua Sanduku la Agano la Bwana, wakamtolea ng'ombe saba kuwa za tambiko pamoja na madume saba ya kondoo.

27Dawidi alikuwa amevaa kanzu ya bafta, hata Walawi wote waliolichukua hilo Sanduku na waimbaji na Kenania, mkuu wao waimbaji aliyewaimbisha, naye Dawidi alikuwa amevaa kisibau cheupe cha ukonge.

28Nao Waisiraeli wote wakalipandisha Sanduku la Agano la Bwana kwa kushangilia na kwa kupiga mabaragumu na matarumbeta na matoazi pamoja na kuyavumisha nayo mapango na mazeze.

29Ikawa, Sanduku la Agano la Bwana lilipoingia mjini kwa Dawidi, Mikali, binti Sauli, alichungulia dirishani, naye alipomwona mfalme Dawidi, jinsi alivyorukaruka na kuchezacheza, ndipo, alipombeza moyoni mwake.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania