1 Mambo 16

1 Mambo 16

Dawidi anamshukuru Mungu.

(1-3,43; 2 Sam. 6:17-19.)

1Walipokwisha kuliingiza Sanduku la Mungu wakaliweka katikati ya lile hema, Dawidi alilolipigia, wakamtolea Mungu ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za kumshukuru.

2Dawidi alipokwisha kuzitoa hizo ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za shukrani akawabariki watu katika Jina la Bwana.

3Kisha akawagawia watu wote wa Isiraeli, waume kwa wake, kila mtu mkate wa sikukuu na kipande cha nyama na andazi la zabibu.

4Akaweka Walawi wengine, watumike hapo penye Sanduku la Bwana na kuwakumbusha watu, Bwana Mungu wa Isiraeli aliyoyafanya, wamshukuru na kumtukuza,

5ndio mkuu Asafu na Zakaria aliyekuwa mkuu wa pili, tena Yieli na Semiramoti na Yehieli na Matitia na Eliabu na Benaya na Obedi-Edomu na Yieli, wavishike vyombo vya kuimbia, mapango na mazeze, naye Asafu ayapige matoazi.

6Nao watambikaji Benaya na Yahazieli wapige matarumbeta siku zote mbele ya Sanduku la Agano la Mungu.

7Siku hiyo ndipo, Dawidi alipoagiza kwanza kumshukuru Bwana kwa msaada wa Asafu na wa ndugu zake:

(8-22: Sh. 105:1-15.)

8Mshukuruni Bwana, nalo Jina lake litambikieni!

Yajulisheni makabila ya watu matendo yake!

9Mpigieni shangwe za kumwimbia!

Mataajabu yake yote yatungieni tenzi!

10Lishangilieni Jina lake lililo takatifu!

Mioyo yao wamtafutao Bwana na ifurahi!

11Mchungulieni Bwana nazo nguvu zake!

Utafuteni uso wake siku zote!

12Yakumbukeni mataajabu yake, aliyoyafanya.

nayo maamuzi yake yashangazayo yakisemwa na kinywa chake!

13Ninyi mlio uzao wake Isiraeli aliyemtumikia,

nanyi wana wa Yakobo, yeye aliyemchagua!

14Yeye Bwana ni Mungu wetu, nchi zote anaziamua.

15Likumbukeni Agano lake kale na kale!

Aliowaagiza kulishika Neno lake ni vizazi elfu.

16Agano ni lile, alilomwekea Aburahamu,

nacho kiapo ni kile, alichomwapia Isaka.

17Mbele yake Yakobo naye akalisimamisha kuwa maongozi,

Agano la kale na kale liwe kwake Isiraeli

18kwamba: Wewe ndiwe, nitakayekupa nchi ya Kanaani.

iwe fungu lenu, nililowapimia.

19Vilikuwa hapo, walipokuwa kikundi cha watu wanaohesabika,

maana kule walikuwa wachache tu, tena wageni.

20Wakawaendea watu wa huko, taifa kwa taifa,

walipotoka kwa mfalme mmoja, wakawajia wenziwe.

21Lakini hakuna mtu, aliyempa ruhusa kuwakorofisha,

hata wafalme akawapatiliza kwa ajili yao kwamba:

22Niliowapaka mafuta msiwaguse tu,

wala wafumbuaji wangu msiwafanyizie mabaya!

(23-33: Sh. 96.)

23Mwimbieni Bwana, nchi zote!

Utangazeni wokovu wake siku kwa siku!

24Wasimulieni wamizimu utukufu wake,

nako kwenye makabila yote ya watu mataajabu yake!

25Kwani mkuu ni Bwana, apaswa na kutukuzwa sana,

naye anaogopesha kuliko miungu yote.

26Kwani miungu yote ya makabila ya watu ni ya bure tu,

lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu.

27Ukuu na urembo uko mbele yake,

uwezo na uchangamko upo hapo, alipo.

28Ninyi mlio wa ukoo wa watu, mpeni Bwana yaliyo yake!

Kwa kuwa ni mtukufu na mnguvu, mpeni Bwana yaliyo yake!

29Kwa kuwa Jina lake ni tukufu, mpeni Bwana yaliyo yake!

Chukueni vipaji vya tambiko, mje kumtokea!

Mtambikieni Bwana na kuvaa mapambo yapasayo Patakatifu!

30Mkimtokea, mastuko na yawaguie, ninyi wa nchi zote!

Yeye ndiye aliyeishikiza nchi, isije kuyumbayumba!

31Kwa hiyo mbingu na zifurahi, nchi nayo na ipige shangwe!

Nako kwa wamizimu na waseme: Bwana ni mfalme!

32Hata bahari nayo yote yajaayo ndani yake na yavume!

Mashamba nayo yote yaliyomo na yapige vigelegele!

33Itakuwa, nayo miti yote ya mwituni imshangilie Bwana,

kwani ndiye atakayekuja kuihukumu nchi.

(34-36: Sh. 106:1,47-48.)

34Mshukuruni Bwana, ya kuwa ni mwema!

Ya kuwa upole wake ni wa kale na kale!

35Semeni: Tuokoe, Mungu uliye wokovu wetu!

Tukusanye na kutuponya kwenye wamizimu,

tupate kulishukuru Jina lako takatifu,

tuzidishe kukusifu na kukushangilia!

36Na atukuzwe Bwana Mungu wa Isiraeli, tangu kale hata kale!

Watu wote wakaitika: Amin! Haleluya!

Malinganyo ya kumtumikia Mungu.

37Huko kwenye Sanduku la Agano la Bwana Dawidi akamwacha Asafu na ndugu zake, watumikie mbele ya hilo Sanduku pasipo kukoma wakifanya kazi ipasayo kila siku moja.

38Tena akamweka Obedi-Edomu pamoja na ndugu zake 68, huyu Obedi-Edomu, mwana wa Yedutuni, na Hosa wawe walinda malango.

39Naye mtambikaji Sadoki na watambikaji ndugu zake akawaacha mbele ya Kao la Bwana kule kilimani kwenye Gibeoni,[#1 Mambo 21:29.]

40wamtolee Bwana mezani pa kutambikia pasipo kukoma asubuhi na jioni ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na kuyafanya yote yaliyoandikwa katika Maonyo ya Bwana, aliyoyaagiza, Waisiraeli wayafanye.[#2 Mose 29:38-39.]

41Pamoja nao walikuwako Hemani na Yedutuni nao wengine wote waliochaguliwa na kuandikwa majina, waimbe:

Mshukuruni Bwana, ya kuwa upole wake ni wakale na kale!

42Akina Hemani na Yedutuni waliokuwa nao, wakapewa matarumbeta na matoazi ya kuwapa wenye kuyapiga na vyombo vyote vya kuimbia nyimbo za Mungu. Nao wana wa Yedutuni wakalinda langoni.

43Kisha watu wote wakaenda kila mtu nyumbani kwake, naye Dawidi akazunguka kuubariki mlango wake.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania