1 Mambo 20

1 Mambo 20

Mji wa Raba na Waamoni unatekwa.

(1-3: 2 Sam. 11:1; 12:26-31.)

1Ikawa, mwaka ulipopita, siku hizo, wafalme wanapozoea kwenda vitani, Yoabu akavipeleka vikosi vya askari, akaiangamiza nchi ya wana wa Amoni, akaja, akausonga mji wa Raba kwa kuuzinga, lakini Dawidi alikuwa anakaa Yerusalemu. Yoabu akaupiga Raba, akaubomoa.

2Ndipo, Dawidi alipoliondoa taji la mfalme wao kichwani pake, akaliona uzito wake kuwa frasila tatu za dhahabu, nalo lilikuwa limepambwa kwa vito vyenye kima; hilo Dawidi akavikwa kichwani. Namo mjini akatoa mateka mengi sana.

3Nao watu waliokuwamo akawatoa, akawakatakata kwa misumeno na kwa magari ya chuma ya kupuria na kwa mashoka. Hivyo Dawidi akaifanyizia miji yote ya wana wa Amoni. Kisha Dawidi akarudi Yerusalemu pamoja na watu wote.

Mapigano matatu ya Wafilisti.

(4-8: 2 Sam. 21:18-22.)

4Ikawa, hayo yalipokwisha, yakatokea mapigano na wafilisti kule Gezeri; huko ndiko, Sibekai wa Husa alikompiga Sipai aliyekuwa mmoja wao yale Majitu marefu; ndivyo, walivyoshindwa.[#1 Mambo 27:11.]

5Kisha yakawa tena mapigano na Wafilisti; ndipo, Elihanani, mwana wa Yairi, alipompiga Lahami, nduguye Goliati wa Gati aliyekuwa na mkuki wenye uti kama majiti ya wafuma nguo.

6Kisha yakawa mapigano tena kule Gati; huko kulikuwa na mtu mrefu sana mwenye vidole sita sita mikononi na miguuni, vyote pamoja ni 24, naye alikuwa mmoja wao yale Majitu marefu.

7Alipowatukana Waisiraeli, Yonatani, mwana wa Simea, kaka yake Dawidi, akampiga.

8Hao walikuwa wamezaliwa katika mlango wa Majitu marefu huko Gati, wakauawa kwa mikono ya Dawidi na kwa mikono ya watumishi wake.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania