1 Mambo 23

1 Mambo 23

Hesabu na Kazi za Walawi.

1Dawidi alipokuwa mzee mwenye kushiba siku za kuwapo, akampa mwanawe Salomo ufalme wa Waisiraeli,[#1 Fal. 1:28-40.]

2akawakusanya wakuu wote wa Waisiraeli na watambikaji na Walawi.

3Hapo Walawi waliomaliza miaka thelathini na zaidi walipohesabiwa, ikawa hesabu yao ya vichwa vya waume 38000.

4Katika hawa wakapewa watu 24000 kuziangalia kazi za nyumba ya Bwana, watu 6000 kuwa wenye amri na waamuzi,

5watu 4000 kuwa walinda malango, tena watu 4000 kumtukuza Bwana kwa vyombo, Dawidi alivyovitengeneza vya kumtukuza Bwana.

6Kisha Dawidi akawagawanya kuwa mafungu yao wana wa Lawi, ndio Gersoni, Kehati na Merari.[#1 Mambo 6:1,16,17.]

7Wagersoni ni Ladani na Simei.[#1 Mambo 26:21.]

8Wana wa Ladani walikuwa watatu: mkubwa Yehieli, tena Zetamu na Yoeli.

9Wana wa simei walikuwa watatu: Selomiti na Hazieli na Harani. Hawa ndio wakubwa wa mlango wa Ladani.

10Wana wa Simei walikuwa: Yahati na Zina na Yeusi na Beria, hawa wanne walikuwa wana wa Simei.

11Naye Yahati alikuwa mkubwa, naye Ziza wa pili; lakini Yeusi na Beria hawakuwa na wana wengi, kwa hiyo walihesabiwa kuwa mlango mmoja.

12Wana wa Kehati walikuwa wanne: Amuramu, Isihari, Heburoni na Uzieli.[#1 Mambo 6:2-3.]

13Wana wa Amuramu walikuwa Haroni na Mose. Haroni akatengwa na kutakaswa, apatumikie Patakatifu Penyewe, yeye na wanawe kale na kale, wamvukizie Bwana kwa utumishi wao, tena wawabariki watu katika Jina lake kale na kale.[#1 Mambo 6:49; 5 Mose 10:8; Ebr. 5:4.]

14Naye Mose akawa mtu wa Mungu, wanawe wakatajwa majina yao penye shina la Lawi.[#5 Mose 33:1.]

15Wana wa Mose walikuwa Gersomu na Eliezeri.[#2 Mose 18:3-4.]

16Wana wa Gersomu mkubwa wao alikuwa Sebueli.[#1 Mambo 26:24.]

17Wana wa Eliezeri mkubwa wao alikuwa Rehabia; yeye Eliezeri hakuwa na wana wengine, lakini wana wa Rehabia walikuwa wengi zaidi.[#1 Mambo 24:21-30.]

18Wana wa Isahari mkubwa wao alikuwa Selomiti.

19Wana wa Heburoni mkubwa wao alikuwa Yeria, wa pili Amaria, wa tatu Yahazieli na wa nne Yekamamu.

20Wana wa Uzieli mkubwa wao alikuwa Mika, wa pili Isia.

21Wana wa Merari walikuwa Mahali na Musi, nao wana wa Mahali walikuwa Elazari na Kisi.[#1 Mambo 6:19.]

22Elazari akafa pasipo kupata wana wa kiume, alipata wa kike tu, nao wana wa Kisi wakawaoa hao ndugu zao.

23Wana wa Musi walikuwa watatu: Mahali na Ederi na Yeremoti.

24Hawa ndio wana wa Lawi kwa milango yao nao wakuu wa milango, kama walivyoandikwa kichwa kwa kichwa kwa hesabu ya majina yao, ndio waliofanyia nyumba ya Bwana kazi za utumishi, waliomaliza miaka ishirini na zaidi;

25kwani Dawidi alisema: Kwa kuwa Bwana Mungu wa Isiraeli ameupatia ukoo wake utulivu, tena kwa kuwa atakaa Yerusalemu kale na kale,[#Yoe. 3:21.]

26sasa Walawi hawana tena kazi za kulichukua hilo Kao na vyombo vyake vyote vya kulitumikia.

27Kwani kwa maagizo ya Dawidi ya mwisho wana wa Lawi walihesabiwa wao waliomaliza miaka ishirini na zaidi.

28Tangu hapo kazi zao zikawa kuwasaidia wana wa Haroni, wakiitumikia nyumba ya Bwana, waziangalie nyua na vyumba, wayasafishe matakatifu yote; hizi zikawa kazi zao za utumishi wa nyumba ya Mungu.

29Tena iliwapasa kuiandaa mikate, aliyowekewa Bwana, na unga uliopepetwa vema wa vilaji vya tambiko na wa maandazi membamba yasiyochachwa na wa vikate vilivyochomwa katika bati la chuma na wa vitumbua na kuviangalia vibaba na vipimo vyote pia.

30Tena iliwapasa kusimama siku kwa siku kulipokucha, wakimshukuru Bwana na kumtukuza, na vilevile kulipokuchwa.[#Sh. 92:3.]

31Tena iliwapasa kumtolea Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima za siku za mapumziko na za miandamo ya mwezi na za sikukuu kwa hesabu zao zilizowekwa za kumtolea Bwana pasipo kukoma.

32Hivyo walishika zamu ya Hema la Mkutano na zamu ya Patakatifu na zamu ya kuwasaidia ndugu zao wana wa Haroni wakitumikia nyumbani mwa Bwana.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania