1 Mambo 26

1 Mambo 26

Walinda malango wa Kilawi.

1Mafungu ya walinda malango yalikuwa haya: kwao wa Kora alikuwa Meselemia, mwana wa kore, naye alikuwa mmoja wao wana wa Asafu.[#2 Mambo 8:14; 35:15.]

2Wana wa Meselemia walikuwa wa kwanza Zakaria, wa pili Yediaeli, wa tatu Zebadia, wa nne Yatinieli;

3wa tano Elamu, wa sita Yohana, wa saba Elihoenai.

4Wana wa Obedi-Edomu walikuwa wa kwanza Semaya, wa pili Yozabadi, wa tatu Yoa, wa nne Sakari, wa tano Netaneli;

5wa sita Amieli, wa saba Isakari, wa nane Peultai, kwani Mungu alimbariki.

6Naye mwanawe Semaya alikuwa amezaliwa wana walioitawala milango yao, kwani walikuwa waume wenye nguvu.

7Wana wa Semaya walikuwa Otini na Refaeli na Obedi, tena Elizabadi na ndugu zake Elihu na Semakia waliokuwa wenye nguvu.

8Hawa wote walikuwa miongoni mwao wana wa Obedi-Edomu, wao na wana wao na ndugu zao walikuwa watu wenye nguvu walioufalia huo utumishi; hao wa Obedi-Edomu walikuwa 62.

9Naye Meselemia alikuwa na wana na ndugu waliokuwa wenye nguvu, nao walikuwa 18.

10Naye Hosa aliyekuwa mmoja wao wana wa Merari alikuwa na wana, mkuu wao alikuwa Simuri, lakini siye wa kwanza, lakini baba yake alimweka kuwa mkuu;

11wa pili alikuwa Hilkia, wa tatu Tebalia, wa nne Zakaria. Wana wote wa Hosa pamoja na ndugu zake walikwua 13.

12Katika haya mafungu ya walinda malango wakuu wao walikuwa na zamu zao za kutumika nyumbani mwa Bwana sawasawa kama ndugu zao.

13Walipoipigia kura za lango kwa lango, waliwapigia wadogo sawasawa kama wakubwa.[#1 Mambo 25:8.]

14Hapo kura ya maawioni kwa jua ikamwangukia Selemia; hata mwanawe Zakaria aliyekuwa mwenye akili za kukata mashauri wakampigia kura, nayo kura yake ikaangukia kaskazini.

15Ya Obedi-Edomu ikaangukia kusini, nayo ya wanawe ikaiangukia nyumba ya vilimbiko.

16Ya Supimu na ya Hosa ikaangukia machweoni kwa jua penye lango la Saleketi, ngazi ya kupandia juu ilipo; hapo vilifuatana kilindo na kilindo.

17Upande wa maawioni kwa jua walikuwa kila siku Walawi sita, kaskazini kila siku wanne, kusini kila siku wanne, napo penye nyumba ya vilimbiko wawili wawili.

18Penye kijumba kilichojengwa kando upande wa machweoni kwa jua walikuwa wanne penye ngazi, tena wawili hapo penye chumba hicho.

19Haya ndiyo mafungu ya walinda malango waliokuwa wana wa Kora na wana wa Merari.

Watunza vilimbiko wa Kilawi.

20Kwao Walawi Ahia akawekwa kuviangalia vilimbiko vya nyumba ya Mungu na vilimbiko vitakatifu.

21Kwao wana wa Ladani ndio wana wa Gersoni, aliowazaa Ladani; waliokuwa wakuu wao hiyo milango ya Ladani, mwana wa Gersoni, ndio wa Yahieli.[#1 Mambo 23:8.]

22Wana wa Yehieli, Zetamu na nduguye Yoeli, wakawekwa kuviangalia vilimbiko vya nyumba ya Bwana.

23Kwao wa Amuramu na kwao wa Isihari na kwao wa Heburoni na kwao wa Azieli

24ndiko, Sebueli, mwana wa Gersomu, mwana wa Mose, alikokuwa mkuu wao walioviangalia vilimbiko.[#1 Mambo 23:16.]

25Tena kwao ndugu zake waliozaliwa na Eliezeri alikuwa mwanawe Rehabia, mwanawe alikuwa Yesaya, mwanawe alikuwa Yoramu, mwanawe alikuwa Zikiri, mwanawe alikuwa Selomiti.[#1 Mambo 23:17.]

26Huyu Selomiti na ndugu zake wakawekwa kuviangalia vilimbiko vitakatifu, alivyovitakasa mfalme Dawidi pamoja na wakuu wa milango na wakuu wa maelfu na wakuu wa mamia na wakuu wa vikosi.

27Walivitoa katika mateka ya vita, wakavitakasa kuziongeza mali za nyumba ya Bwana.

28Navyo vyote, alivyovitakasa mtazamaji Samweli na Sauli, mwana wa Kisi, na Abineri, mwana wa Neri, na Yoabu, mwana wa Seruya, vyote pia vikatiwa mikononi mwa Selomiti na ndugu zake.

Waamuzi wa Kilawi.

29Kwao wa Isihari waliwekwa Kenania na wanawe kufanya kazi za huko nje kwa Waisiraeli, wawe wenye amri na waamuzi wao.

30Kwao wa Heburoni waliwekwa Hasabia na ndugu zake, watu 1700 wenye nguvu, kuwaangalia Waisiraeli waliokuwako ng'ambo ya huku ya Yordani, upande wa machweoni kwa jua, wafanye kazi zote za Bwana, tena wamtumikie mfalme.

31Kwao wa Heburoni alikuwa naye Yeria aliyekuwa mkuu wao wa Heburoni kwa vizazi vyao na kwa milango yao; walipohesabiwa katika mwaka wa arobaini wa ufalme wa Dawidi, wakaonekana kwao mafundi wa vita wenye nguvu mle Yazeri wa Gileadi.

32Nao ndugu zake waliokuwa wenye nguvu, watu 2700, nao walikuwa wakuu wa milango. Hawa mfalme Dawidi aliwaweka kuwaangalia watu wa Rubeni na wa Gadi nao wa nusu ya shina la Manase, wafanye mambo yote ya Mungu na mambo ya mfalme yawapasayo.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania