1 Mambo 28

1 Mambo 28

Dawidi anamweka Salomo, ampokee ufalme.

1Dawidi akawakusanya Yerusalemu wakuu wote wa Waisiraeli, wakuu wa mashina na wakuu wa mafungu yaliyomtumikia mfalme na wakuu wa maelfu na wakuu wa mamia na wakuu wa mali na wa mapato yote ya mfalme na wanawe pamoja na watumishi wa nyumbani na mafundi wa vita nao wote waliokuwa waume wenye nguvu.

2Ndipo, mfalme Dawidi alipoinuka, asimame kwa miguu yake, akasema: Nisikilizeni, ninyi ndugu zangu nanyi mlio wa ukoo wangu! Mimi naliwaza moyoni mwangu kujenga nyumba, ndimo Sanduku la Agano la Bwana lipate kutulia, iwe mahali, Mungu wetu awekee miguu yake, nikaitengeneza mijengo.[#1 Mambo 22:7-10.]

3Lakini Mungu akaniambia: Hutalijengea Jina langu nyumba, kwani wewe ni mtu wa kupiga vita, ukamwaga damu.[#2 Sam. 7:5.]

4Lakini Bwana Mungu wa Isiraeli alinichagua katika mlango wote wa baba yangu, niwe mfalme wa Waisiraeli kale na kale, kwani alimchagua Yuda, awe mkubwa, namo mlangoni mwa Yuda akauchagua mlango wa baba yangu, namo katika wana wa baba yangu akapendezwa kunifanya mfalme wa Waisiraeli wote.[#1 Mose 49:10; 1 Sam. 16:1,12.]

5Kisha katika wanangu wote, kwani Bwana akanipa wana wengi, akamchagua mwanangu Salomo, akae katika kiti cha ufalme wa Bwana na kuwatawala Waisiraeli.

6Akaniambia: Mwanao Salomo ndiye atakayeijenga nyumba yangu na nyua zangu, kwani nimemchagua, awe mwanangu, mimi nami nitakuwa baba yake.[#1 Mambo 17:11-14.]

7Nao ufalme wake nitaushikiza, uwe wa kale na kale, akijishupaza kuyafanya maagizo yangu na maamuzi yangu kama leo.

8Sasa machoni pao Waisiraeli wote walio mkutano wa Bwana namo masikioni pake Mungu wetu ninawaonya: Yaangalieni na kuyatafuta maagizo yote ya Bwana Mungu wenu, mpate kuishika nchi hii njema, iwe yenu, kisha mwiachie wana wenu watakaokuwa nyuma yenu, iwe fungu lao kale na kale!

Dawidi anampa salomo mfano wa nyumba ya Mungu na mijengo.

9Nawe mwanangu Salomo, mjue Mungu wa baba yako, umtumikie kwa moyo wote mzima na kwa roho ipendezwayo naye! Kwani Bwana huichungua mioyo yote na kuyatambua mawazo yote, iliyoyatunga. Utakapomtafuta, atakuonekea; lakini ukimwacha, atakutupa kale na kale.[#Sh. 7:10.]

10Sasa vitazame vema! Kwani Bwana amekuchagua, uijenge nyumba itakayokuwa Patakatifu! Jihimize kuyafanya!

11Kisha Dawidi akampa mwanawe salomo mfano wa ukumbi na wa nyumba zake na wa vyumba vyake vya vilimbiko na wa vyumba vya juu na wa vyumba vya ndani na wa nyumba ya kupatia upozi,[#2 Mose 25:9.]

12hata mfano wao yote, aliyokuwa ameyawaza rohoni mwake, wa nyua za nyumba ya Bwana na wa vyumba vyote vilivyozizunguka na wa vilimbiko vya nyumba ya Mungu na wa vilimbiko vitakatifu.

13Akamwambia nazo zamu za watambikaji na za Walawi na kazi zote za utumishi wa nyumbani mwa Bwana na vyombo vyote vya utumishi wa nyumbani mwa Bwana.

14Akampa nazo dhahabu zilizopimwa; kila chombo kimoja cha kila kazi ya utumishi kilikuwa na dhahabu yake, tena fedha zilizopimwa, kila chombo kimoja cha kila utumishi fedha yake.

15Hata vinara vilipimiwa dhahabu zao, nazo taa zao dhahabu zao kila kinara kimoja na kila taa moja ilipimiwa dhahabu zake, hata fedha za vinara na za taa zao zilipimiwa kila kinara kimoja, kama kilivyotumika.

16Akampa nazo dhahabu zilizopimiwa meza za mikate, aliyowekwa Bwana, kila meza dhahabu zake, hata fedha za meza za fedha.

17Akampa tena dhahabu tupu za nyuma na za vyano na za madumu na za vinyweo vya dahabu, kila kinyweo kimoja kilipimiwa dhahabu zake, navyo vinyweo vya fedha vilipimiwa kila kinyweo kimoja fedha zake.

18Akampa nazo dhahabu zilizong'azwa za meza ya kuvukizia uvumba, nazo zilipimwa. Kisha akampa mfano wa gari, ndio makerubi ya dhahabu yaliyokunjua mabawa, yalifunike Sanduku la Agano la Bwana,

19Akamwambia: Haya yote yamo katika mwandiko uliotoka mkononi mwa Bwana, nikaupata, unifundishe kazi zote za mfano huu.

20Kisha Dawidi akamwambia mwanawe Salomo: Jipe moyo, upate nguvu za kuyafanya! Usiogope, wala usiingiwe na vituko! Kwani Bwana Mungu aliye Mungu wangu atakuwa na wewe, hatakuacha, wala hatakuepuka, hata kazi zote za utumishi wa nyumba ya Bwana zimalizike.[#1 Mambo 22:13; 5 Mose 31:6.]

21Tazama! Yako mafungu ya watambikaji na ya Walawi wa kuufanya utumishi wote wa hiyo nyumba ya Mungu, tena unao mafundi wa kila kazi wanaotaka kukusaidia kwa moyo, nao huujua kweli huo utumishi wote, hata wakuu na watu wote watakutii yote, utakayowaambia.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania