1 Wafalme 16

1 Wafalme 16

Kufa kwake Basa.

1Neno la Bwana likamjia Yehu, mwana wa Hanani, kwa ajili ya Basa kwamba:[#1 Fal. 16:7.]

2Nilikukweza na kukutoa uvumbini, nikakupa kuwatawala walio ukoo wangu wa Waisiraeli, lakini umeendelea kuishika njia ya Yeroboamu, ukawakosesha walio ukoo wangu wa Waisiraeli, upate kunichafua kwa makosa yao.[#1 Fal. 14:7.]

3Kwa hiyo utaniona, nikimzoa Basa pamoja na mlango wake, nikiutoa mlango wako, uwe kama mlango wa Yeroboamu, mwana wa Nebati.[#1 Fal. 15:29.]

4Wao wa Basa watakaokufa mjini mbwa watawala; nao watakaokufa shambani madege wa angani watawala.[#1 Fal. 14:11.]

5Mambo mengine ya Basa nayo, aliyoyafanya, nayo matendo yake ya vitani yenye nguvu hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli?

6Basa akaja kulala na baba zake, akazikwa Tirsa, naye mwanawe Ela akawa mfalme mahali pake.

7Neno lile, Bwana alilolitoa kinywani mwa mfumbuaji Yehu, mwana wa Hanani, la mambo yatakayompata Basa na mlango wake, alilisema kwa ajili ya mabaya yote, aliyoyafanya machoni pa Bwana, amchafue kwa matendo ya mikono yake, akiwa kama wao wa mlango wa Yeroboamu, tena kwa kuwa aliwaua wao wa mlango wake.[#1 Fal. 16:1.]

Mfalme Ela wa Waisiraeli.

8Katika mwaka wa 26 wa Asa, mfalme wa Wayuda, Ela, mwana wa Basa, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli huko Tirsa miaka 2.[#1 Fal. 16:6.]

9Ndipo, mtumishi wake Zimuri, mkuu wa nusu ya magari, alipomlia njama; naye alikaa Tirsa. Siku moja alipokunywa na kulewa nyumbani mwa Arsa aliyekuwa mkuu wa nyumbani huko Tirsa,[#1 Fal. 15:27.]

10Zimuri akaingia, akampiga na kumwua katika mwaka wa 27 wa Asa, mfalme wa Wayuda, kisha akawa mfalme mahali pake.[#2 Fal. 9:31; 15:10,14,25,30.]

11Alipokwisha kuwa mfalme na kukaa katika kiti chake cha kifalme, akawaua wote waliokuwa wa mlango wa Basa, hakusaza wa kiume hata mmoja, wala ndugu zake, wala rafiki zake.

12Ndivyo, Zimuri alivyouangamiza mlango wa Basa, kama Bwana alivyosema kinywani mwa mfumbuaji Yehu yatakayompata Basa[#1 Fal. 16:1-4.]

13kwa ajili ya makosa yote ya Basa na kwa ajili ya makosa ya mwanawe Ela, waliyoyakosa na kuwakosesha Waisiraeli, wamchafue Bwana Mungu wa Isiraeli kwa mambo yao yasiyokuwa na maana.

14Mambo mengine ya Ela nayo yote, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli?

Mfalme Zimuri wa Waisiraeli.

15Katika mwaka wa 27 wa Asa, mfalme wa Wayuda, Zimuri akapata kuwa mfalme huko Tirsa siku 7; nao watu walikuwa wakiuzinga Gibetoni ulioko kwa Wafilisti.[#1 Fal. 15:27.]

16Wale watu waliouzinga huo mji waliposikia kwamba: Zimuri amemlia mfalme njama, akamwua, siku hiyo Waisiraeli wote waliokuwa huko makambini wakamfanya Omuri, mkuu wa vikosi, kuwa mfalme wa Waisiraeli.[#1 Fal. 16:9-10.]

17Kisha Omuri pamoja na Waisiraeli wote wakatoka Gibetoni, wakapanda, wausonge Tirsa kwa kuuzinga.

18Zimuri alipoona, ya kuwa mji umetekwa, akaingia ngomeni nyumbani mwa mfalme, akaichoma moto hiyo nyumba ya mfalme, alimokuwa, akafa hivyo

19kwa ajili ya makosa yake, aliyoyakosa na kuyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana akiendelea kuishika njia ya Yeroboamu na kuyafuata makosa yake, aliyoyafanya ya kuwakosesha Waisiraeli.

20Mambo mengine ya Zimuri nayo njama yake, aliyomlia mfalme, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli?

Mfalme Omuri wa Waisiraeli.

21Siku zile wao walio ukoo wa Waisiraeli wakagawanyika kuwa pande mbili: nusu ya watu ikawa upande wa Tibuni, mwana wa Ginati, wamfanye kuwa mfalme, nusu yao ikawa upande wa Omuri.

22Lakini watu waliokuwa upande wa Omuri wakapata nguvu kuliko wale waliokuwa upande wa Tibuni, mwana wa Ginati. Tibuni alipokufa, Omuri akaupata ufalme.

23Katika mwaka wa 31 wa Asa, mfalme wa Wayuda, Omuri akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli miaka 12. Alipoushika ufalme mle Tirsa miaka sita

24akaununua mlima wa Samaria kwa Semeri na kumlipa vipande viwili vya fedha, ndio shilingi 24000, kisha akajenga mji huko mlimani; nao huo mji, alioujenga, akauita Samaria kwa jina la Semeri aliyekuwa mwenye huo mlima.

25Omuri akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, naye akafanya mabaya zaidi kuliko wote waliokuwa mbele yake.[#Mika 6:16.]

26Akaendelea kuzishika njia zote za Yeroboamu, mwana wa Nebati, na kuyafanya makosa yake yaliyowakosesha Waisiraeli, wamchafue Bwana Mungu wa Isiraeli kwa mambo yao yasiyokuwa na maana.[#1 Fal. 12:30.]

27Mambo mengine ya Omuri, aliyoyafanya, nayo matendo yake ya vitani yenye nguvu, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli?

28Omuri akaja kulala na baba zake, akazikwa mle Samaria, naye mwanawe Ahabu akawa mfalme mahali pake.

Makosa ya mfalme Ahabu.

29Ahabu, mwana wa Omuri, akapata kuwa mfalme wa Waisiraeli katika mwaka wa 38 wa Asa, mfalme wa Wayuda. Naye Ahabu, mwana wa Omuri, akawa mfalme wa Waisiraeli mle Samaria miaka 22.

30Ahabu, mwana wa Omuri, akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana kuliko wote waliokuwa mbele yake.

31Tena haikumtoshea kuendelea kuyafanya makosa ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, akamwoa naye Izebeli, binti Etibaali, mfalme wa Sidoni, kisha akaenda kumtumikia Baali na kumwangukia.[#1 Fal. 16:26.]

32Akampatia Baali pa kumtambikia katika nyumba ya Baali, aliyoijenga Samaria.[#2 Fal. 3:2; 10:27-28.]

33Kisha Ahabu akatengeneza hata kinyago cha Ashera; ndivyo, Ahabu alivyozidisha kufanya mambo ya kumchafua Bwana Mungu wa Isiraeli kuliko wafalme wote wa Waisiraeli waliokuwa mbele yake.

34Hizo siku zake Hieli wa Beteli akaujenga tena mji wa Yeriko. Alipoiweka misingi yake, Abiramu, mwanawe wa kwanza, akafa, tena alipoyatia malango, akafa mwanawe mdogo Segubu, kama Bwana alivyosema kinywani mwa Yosua, mwana wa Nuni.[#Yos. 6:26.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania