1 Wafalme 17

1 Wafalme 17

Mfumbuaji Elia anaitangaza njaa itakayokuja.

1Elia wa Tisibe aliyekaa ugenini huko Gileadi akamwambia Ahabu: Hivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli, ninayemtumikia, alivyo Mwenye uzima, miaka hii umande hautakuwako, wala mvua haitakunya, isipokuwa kwa neno la kinywa changu.[#Yak. 5:17; Ufu. 11:6.]

2Kisha neno la Bwana likamjia la kwamba:

3Ondoka hapa, ujiendee upande wa maawioni kwa jua kijificha kwenye kijito cha Kriti kinachoingia Yordani!

4Na unywe katika kijito hicho, tena nimeagiza makunguru, wakutunze kuko huko.

Elia kwenye kijito cha Kriti.

5Ndipo, alipokwenda, afanye, kama Bwana alivyomwagiza, akaenda kukaa kwenye kijito cha Kriti kinachoingia Yordani.

6Makunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, tena mkate na nyama jioni, akanywa maji ya hicho kijito.

7Ikawa, siku zilipopita, kijito kikakauka, kwani hakuna mvua katika nchi.

8*Ndipo, neno la Bwana lilipomjia la kwamba:

9Inuka, uende Sareputa katika nchi ya Sidoni, ukae huko! Utaona huko mwanamke mjane, niliyemwagiza, akutunze.[#Luk. 4:25-26.]

Elia anakaa Sareputa.

10Akainuka, akaenda Sareputa. Alipofika penya lango la mji akaona huko mwanamke mjane aliyeokota kuni, akamwita na kumwambia: Uniletee maji kidogo katika kata, ninywe!

11Alipokwenda kuyaleta, akamwita na kumwambia: Uniletee hata kipande kidogo cha mkate mkononi mwako.

12Akamjibu: Hivyo, Bwana Mungu wako alivyo Mwenye uzima, sinacho kilichochomwa! Nilivyo navyo ndio gao la unga katika kitungi na vifuta vichache katika kichupa. Tazama, ninaokota vikuni viwili, nije nijipikie mwenyewe na mwanangu, tule, kisha tufe.[#1 Fal. 18:10.]

13Elia akamwambia: Usiogope! Nenda, ufanye, kama ulivyosema! Lakini kwanza unitengenezee kiandazi kidogo, uniletee hapa nje! Kisha ujitengenezee wewe na mwanao!

14Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Unga hautaisha katika kitungi, wala kichupa hakitakosa mafuta mpaka siku ile, Bwana atakaponyesha mvua katika nchi.[#2 Fal. 4:2-4.]

15Yule mwanamke akenda, akafanya, kama Elia alivyosema, akala yeye, naye Elia aliyekuwamo nyumbani mwake siku kwa siku.

16Lakini unga haukuisha katika kitungi, wala kichupa hakikukosa mafuta, kama Bwana alivyosema kinywani mwa Elia.*

Elia anamfufua mwana wa mjane.

17Ikawa, hayo yalipokwisha kufanyika, mwanawe huyu mwanamke aliyekuwa mwenye nyumba akaugua, nao ugonjwa wake ukawa wenye nguvu sana, hata pumzi hasikusalia mwilini mwake.

18Ndipo, mwanamke alipomwambia Elia: Tuko na bia gani mimi na wewe, mtu wa Mungu? Umeingia mwangu kuyaumbua mabaya yangu, niliyoyafanya, umwue mwanangu.[#Luk. 5:8.]

19Elia akamwambia: Nipe mwanao! Akamchukua kifuani pake, akapanda naye darini, alimokuwa anakaa, akamlaza kitandani pake.

20Akamlilia Bwana kwamba: Bwana Mungu wangu, mbona umemfanyizia vibaya naye huyu mwanamke, ambaye nimefikia kwake, ukimwua mwanawe?

21Akamkumbatia mtoto mara tatu na kumlalia juu, akamlilia Bwana akisema: Bwana Mungu wangu, roho ya huyu mtoto na irudi mwake![#2 Fal. 4:34; Tume. 20:10.]

22Bwana akaiitikia sauti ya Elia, roho ya mtoto ikarudi mwilini mwake, akawa mzima tena.

23Ndipo, Elia alipomchukua mtoto, akashuka naye nyumbani kutoka darini, akampa mama yake yeye Elia akimwambia: Tazama, mwanao ni mzima![#Luk. 7:15; Ebr. 11:35.]

24Yule mwanamke akamwambia Elia: Sasa hivi nimetambua, ya kuwa wewe ndiwe mtu wa Mungu, nalo Neno la Mungu lililomo kinywani mwako ni la kweli.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania