The chat will start when you send the first message.
1Nyumba yake Salomo akaijenga miaka kumi na mitatu, mpaka akaimaliza hiyo nyumba yake yote.[#1 Fal. 9:10.]
2Kwanza akaijenga nyumba ya mwituni kwa Libanoni, urefu wake wa kwenda mbele ulikuwa mikono mia nao upana wake mikono hamsini nao urefu wake wa kwenda juu mikono thelathini; ilikuwa juu ya safu nne za nguzo za miangati, nazo boriti za miangati zilikuwa zimewekwa juu ya hizo nguzo.[#Yes. 22:8.]
3Vyumba vyake vilikuwa juu ya hizo nguzo, vikafunikwa juu penye dari kwa mbao za miangati, navyo vilikuwa arobaini na vitano, kila safu kumi na vitano.
4Nayo miamba ilikuwako safu tatu, hata madirisha yaliyoelekeana dirisha kwa dirisha, hivyo mara tatu.
5Milango yote na miimo yote ilikuwa ya nguzo zenye miraba, hata madirisha yaliyoelekeana dirisha kwa dirisha, hivyo mara tatu.
6Kisha akatengeneza ukumbi wenye nguzo, urefu wake wa kwenda mbele ulikuwa mikono hamsini, upana wake mikono thelathini; mbele yake kulikuwa na ukumbi mwingine wenye nguzo na kipago mbele yao.
7Kisha akatengeneza ukumbi wa kiti cha kifalme kuwa baraza ya shauri, atakamokatia mashauri ya watu; ukafunikwa mbao za miangati toka chini hata juu.
8Kisha akaijenga nyumba yake ya kukaa humo katika ua wa pili upande wa ndani wa ukumbi huo, nayo ikajengwa vivyo hivyo. Tena akajenga nyumba ya binti Farao, Salomo aliyemwoa, ikawa vivyo hivyo kama ule ukumbi.[#1 Fal. 3:1.]
9Majengo haya yote yalikuwa yamejengwa kwa mawe mazuri yaliyochongwa kwa kipimo na kukatwa kwa misumeno upande wa nyumbani na wa nje, kutoka kwenye msingi mpaka juu kwenye mawe yanayotokea kidogo toka nje kufikia ua mkubwa.
10Nayo misingi ilikuwa imewekewa mawe mazuri makubwa mno, mengine ya mikono kumi, mengine ya mikono minane.
11Juu yao palikuwa na mawe mazuri yaliyochongwa kwa kipimo, tena miangati.
12Ua mkubwa ukazunguka po pote wenye ukuta wa safu tatu za mawe ya kuchonga na safu moja ya boriti za miangati. Ndivyo, vilivyokuwa hata penye ua wa ndani wa nyumba ya Bwana na penye ua wa ukumbi wa nyumba yake.[#1 Fal. 6:36.]
13Kisha mfalme Salomo akatuma kumchukua Hiramu kule Tiro:[#2 Mambo 2:12-13.]
14alikuwa mwana wa mwanamke mjane wa shina la Nafutali, naye baba yake alikuwa mtu wa Tiro aliyefua shaba. Huyu alikuwa mwenye werevu wa kweli na utambuzi na ujuzi wote wa kuzitengeneza kazi zote pia kwa shaba. Huyu akaja kwa mfalme Salomo, akamfanyizia hizo kazi zote.[#1 Mose 4:22; 2 Mose 31:3-4.]
(15-21: 2 Mambo 3:15-17.)15Akatengeneza nguzo mbili za shaba, urefu wake nguzo moja ulikuwa mikono kumi na minane, tena uzi wa mikono kumi na miwili ukaizunguka, nayo nguzo ya pili ilikuwa hivyo.[#2 Fal. 25:17.]
16Akafanya hata vichwa viwili vya kuviweka juu ya hizi nguzo, vilitengenezwa kwa shaba iliyoyeyushwa; kichwa kimoja urefu wake wa kwenda juu ulikuwa mikono mitano, nao wake wa pili mikono mitano.
17Tena misuko iliyotengenezwa kwa nyuzi zilizokuwa kama mikufu ikavifunika vichwa vilivyokuwa juu ya nguzo, kichwa kimoja kikapata saba, nacho cha pili saba.
18Kisha akatengeneza komamanga, mistari miwili ya kuzunguka penye msuko mmoja uliokuwa wa kuvifunika vichwa vilivyokuwa juu ya hizo nguzo, nao wa pili akautengeneza vivyo hivyo.
19Navyo hivyo vichwa vilivyokuwa juu ya nguzo penye ukumbi vilikuwa vimetengenezwa kuwa kama maua ya uwago yenye mikono minne.
20Hivyo vichwa vya juu ya hizo nguzo vilikuwa juu penye ukingo uliokuwa wenye ile misuko. Nazo komamanga zilikuwa 200, zikauzunguka nao msuko wa nguzo ya pili kwa mistari-mistari.
21Kisha akazisimamisha hizo nguzo penye ukumbi wa jumba hili; alipoisimamisha nguzo ya kuumeni akaiita jina lake Yakini (Hushikiza); tena alipoisimamisha nguzo ya kushotoni akaiita jina lake Boazi (Nguvu imo).
22Tena vichwa vya hizo nguzo vilikuwa vimetengenezwa kuwa kama maua ya uwago. Ndivyo, kazi za hizo nguzo zilivyomalizika.
(23-26: 2 Mambo 4:2-5.)23Kisha akaitengeneza ile bahari kwa shaba iliyoyeyushwa; toka ukingo wake wa huku hata ukingo wa huko ilikuwa mikono kumi; iliviringana pande zote, urefu wake wa kwenda juu ulikuwa mikono mitano, nayo kamba ya kuizunguka pande zote ilikuwa ya mikono thelathini.
24Chini ya ukingo wake kuizunguka pande zote palikuwa na mifano ya matango, kumi kwa mkono mmoja, ikaizunguka hiyo bahari pande zote, hiyo mifano ya matango ilikuwa mistari miwili, nayo ilikuwa imeyeyushiwa mumo, bahari ilipoyeyushwa.
25Ikakaa juu ya ng'ombe kumi na mbili, tatu zilielekea kaskazini, tatu zilielekea baharini, tatu zilielekea kusini, tatu zilielekea maawioni kwa jua, nayo bahari ilikuwa juu yao, nayo mapaja yao yote yalikuwa yameelekea ndani.
26Unene wake ulikuwa upana wa shibiri, nao ukingo wake wa juu ulikuwa kama wa kikombe au kama wa ua la uwago. Ndani yake zilienea bati 2000, ndip pishi 18000.
(27-39: 2 Mambo 3:6,10.)27Kisha akatengeneza vilingo kumi vya shaba. Urefu wa kwenda mbele wa kila kilingo kimoja kilikuwa mikono minane nao upana wake ulikuwa mikono minne, nao urefu wake wa kwenda juu ulikuwa mikono mitatu.
28Hivi vilingo vilikuwa vimetengenezwa hivyo: vilikuwa na vibao vya kufungia, hivi vibao vilikuwa katikati ya vilingo.
29Namo katika hivi vibao vilivyokuwa katikati ya vilingo mlikuwa na simba na ng'ombe na Makerubi, vilevile katika vilingo juu na chini ya hizo simba na ng'ombe palikuwa pametengenezwa kata za maua zilizoning'inia.
30Kila kilingo kimoja kilikuwa na magurudumu manne ya shaba, navyo vyuma vya kuyashikia vilikuwa vya shaba; tena miguu yao minne ilikuwa yenye vishikio, navyo hivi vishikio vilikuwa vimetiwa kwa kuyeyushwa chini ya bakuli, tena kando yao kila mmoja pametiwa kata zilizoelekeana.
31Kinywa chake kilikuwa ndani ya kilemba, kikatokea juu kipande cha mkono; hicho kinywa chake kikaviringana, maana kilitengenezwa kuwa hivyo, upana wake ukawa mkono mmoja na nusu. Napo penye kinywa chake palikuwa na machoro; lakini vile vibao vya kufungia vilikuwa vyenye miraba, havikuviringana.
32Yale magurudumu manne yalikuwa chini ya vibao vya kufungia, navyo vyuma vya kuyashikia magurudumu vilikuwa vimeungwa na kilingo, nao urefu wa kwenda juu wa gurudumu moja ulikuwa mkono mmoja na nusu.
33Hayo magurudumu yalikuwa yametengenezwa kama magurudumu ya magari, lakini vyuma vyao vya kuyashikia na miviringo yao ya nje na vijiti vyao na vichwa vyao vya kati vyote pia vilikuwa vya shaba iliyoyeyushwa.
34Penye pembe zote nne za kila kilingo palikuwa na vishikio vinne; hivi vishikio vilikuwa vimeunganika na kilingo chao chenyewe.
35Juu ya kilingo palikuwa kama kilingo kidogo kilichoviringana pande zote, urefu wa kwenda juu ulikuwa nusu ya mkono tu; hapo juu ya kilingo palikuwa navyo vyuma vya kushikia bakuli na vibao vyake vya kufungia, vyote vilikuwa vimeunganika nacho.
36Katika mabamba ya vyuma vyake vya kushikia na katika vibao vyake vya kufungia akachora Makerubi na simba na mitende, po pote kama palivyokuwa na nafasi, kisha akachora kata za maua za kuyazungusha yale machoro.
37Hivyo ndivyo, alivyovitengeneza vile vilingo kumi, vyote pia viliyeyushwa kwa njia moja, nacho kipimo chao kilikuwa kimoja, nao mfano wao ulikuwa mmoja.
38Kisha akatengeneza mitungi kumi ya shaba, katika mtungi mmoja zilienea bati 40, ndio pishi 360, nao upana wa kila mtungi mmoja ulikuwa mikono minne, akaweka katika vilingo vile kumi mtungi mmoja katika kila kilingo kimoja.
39Akaweka vilingo vitano kuumeni kwa ile nyumba na vitano kushotoni kwake ile nyumba, nayo ile bahari akaiweka kuumeni kwa ile nyumba kunakoelekea maawioni kwa jua, lakini kusini kidogo.
(40-47: 2 Mambo 4:11-18.)40Kisha Hiramu akatengeneza mitungi na majembe na vyano. Hiramu akazimaliza kazi zote, alizomfanyizia mfalme Salomo nyumbani mwa Bwana:
41nguzo mbili zenye vilemba vya vile vichwa viwili vilivyoko juu ya hizo nguzo na misuko miwili kama ya mkeka ya kuvifunika vile vilemba viwili vya vichwa vilivyoko juu ya hizo nguzo;
42tena komamanga 400 zilizotiwa katika ile misuko, kila msuko mmoja ukipata mistari miwili ya komamanga ya kuvifunika vile vilemba viwili vya vichwa vilivyoko juu ya hizo nguzo;
43tena vile vilingo kumi na mitungi kumi iliyowekwa juu ya hivyo vilingo;
44tena ile bahari moja na zile ng'ombe kumi na mbili zilizokuwa chini ya ile bahari;
45nayo masufuria na majembe na vyano. Vyombo hivi vyote, Hiramu alivyomtengenezea mfalme Salomo, avitie nyumbani mwa Bwana, vilikuwa vya shaba iliyong'aa.
46Naye mfalme alikuwa ameagiza kuviyeyusha katika bwawa la Yordani penye udongo mgumu katikati ya miji ya Sukoti na Sartani.
47Salomo akaviweka tu vyombo hivi vyote; kwa kuwa vingi sanasana shaba zilizotumiwa hazikupimwa, wala hazikuulizwa, kama ni ngapi.
(48-51: 2 Mambo 4:19-5:1.)48Ndivyo, Salomo alivyovitengeneza vyombo vyote vya kutumiwa nyumbani mwa Bwana. Lakini meza ya kutambikia ilikuwa ya dhahabu, nayo meza ya kumwekea Bwana mikate ilikuwa ya dhahabu;
49navyo vile vinara, vitano vya kuviweka kuumeni, na vitano vya kuviweka kushotoni mbele ya Patakatifu Penyewe, vilikuwa vya dhahabu zilizong'azwa, nayo maua na taa na koleo zao zilikuwa za dhahabu;
50tena mabakuli na makato ya kusafishia mishumaa na vyano na kata na sinia zilikuwa za dhahabu zilizong'azwa. Nazo bawaba za milango ya chumba cha ndani pa kupaingilia Patakatifu Penyewe nazo za milango ya chumba kikubwa cha Patakatifu zilikuwa za dhahabu.
51Kazi zote, ambazo mfalme Salomo aliifanyia nyumba ya Bwana, zilipomalizika, Salomo akavipeleka vipaji vitakatifu vyote vya baba yake Dawidi, zile fedha na dhahabu na vile vyombo, akaviweka penye vilimbiko vya nyumba ya Bwana.