1 Petero 1

1 Petero 1

Anwani.

1Mimi Petero niliye mtumwa wa Yesu Kristo nawaandikia ninyi wateule mkaao ugenini na kutawanyika kule Ponto na Galatia na Kapadokia na Asia na Bitinia.[#Yak. 1:1.]

2Kwa hivyo, Mungu Baba alivyowatambua kale, aliwatakasa kwa Roho yake, mpate kutii kwa kunyunyizwa damu yake Yesu Kristo. Upole uwafurikie na utengemano![#Rom. 8:29.]

Fungu letu lililoko mbinguni.

3*Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa sababu alituonea huruma nyingi, akatuzaa mara ya pili, tupate kingojeo chenye uzima kwamba: Yesu kristo amefufuka katika wafu![#1 Petr. 1:23.]

4Ndipo, alipotupatia fungu lisiloozeka, lisilochafuka, lisilonyauka; hilo mmelimbikiwa mbinguni ninyi.[#Kol. 1:12.]

5Tena mkikaa na kumtegemea mnalindwa kwa nguvu za Mungu, mpate wokovu uliotengenezwa wa kutokea waziwazi siku za mwisho.[#Yoh. 10:28; 17:11.]

6Hapo mtashangilia, hata ikiwapasa sasa kusikitika siku kidogo, mkijaribiwa na mambo menginemengine,[#Rom. 5:2; 2 Kor. 4:17; 1 Petr. 5:10.]

7kwamba: Kumtegemea Mungu kujulike kwenu kuwa kwa kweli, kisha kuonekane kuwa kwenye kima sana kuliko dhahabu iangamikayo, nayo uzuri wake hujulikana motoni. Mkiwa hivyo mtapata sifa na utukufu na macheo hapo, Yesu Kristo atakapotokea waziwazi.[#Fano. 17:3; Mal. 3:3.]

8Naye mmempenda pasipo kumwona, mkamtegemea pasipo kumwona kamwe; kwa hiyo mtashangilia kwa furaha isiyosemeka kwa utukufu wake;[#Yoh. 20:29; 2 Kor. 5:7.]

9itakuwa hapo, mtakapoutwaa mwisho wa kumtegemea, ndio wokovu wa roho zenu.*[#Rom. 6:22.]

Kazi ya wafumbuaji.

10Nao wafumbuaji walioyafumbua hayo mema, mliyogawiwa, waliutafuta sana wokovu huo na kuuchunguza; wakayafuatafuata, wapate kujua,[#Luk. 10:24.]

11kama ni siku za wakati gani zile, ambazo Roho ya Kristo, waliyokuwa nayo, inazivumbua na kuyashuhudia hapo kale mateso yatakayompata Kristo nao utukufu utakaokuwa mwishoni.[#Sh. 22; Yes. 53.]

12Wao walikuwa wamefunuliwa, ya kama mafumbuo yao hayakuwa ya kuwatumikia wao wenyewe, ila ninyi. Nako kwenu yanatangazwa sasa nao wawapigiao hiyo mbiu njema kwa nguvu ya Roho takatifu iliyotumwa toka mbinguni. Basi, mambo hayo hata malaika huyatunukia kuyachungulia.[#Ef. 3:10.]

Makombozi yetu.

13*Kwa hiyo jifungeni kiroho viuno vyenu, mlevuke! Mtimilike na kuyangojea yale mema, mnayoletewa, mgawiwe, Yesu Kristo atakapotokea waziwazi![#Luk. 12:35-36.]

14Kwa sababu m watoto wanaotii, msijielekeze penye tamaa zenu, mlizozifuata hapo kale, mlipokuwa hamjajua maana![#Rom. 12:2.]

15Ila kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, vivyo hivyo nanyi mwe watakatifu katika mwenendo wenu wote!

16Kwani imeandikwa:

Mwe watakatifu! Kwani mimi ni mtakatifu.*

17*Tena ninyi humwita Baba yeye anayemhukumu kila mtu kwa kazi yake pasipo kupendelea; kwa hiyo mwendelee miaka yenu ya kukaa ugenini na kuogopa![#Rom. 2:11; Fil. 2:12.]

18Jueni: vyenye kuoza, vingawa fedha au dhahabu, sivyo, ambavyo mlikombolewa navyo katika mwenendo wenu wa kikale uliokuwa hauna maana;[#1 Petr. 4:3; 1 Kor. 6:20; 7:23.]

19ila mmekombolewa kwa damu ya Kristo iliyo yenye kima kikuu, maana alikuwa mwana kondoo asiye na kilema wala doadoa.[#Yes. 53:7; Yoh. 1:29; Ebr. 9:14.]

20Alitambulika kale, ulimwengu ulipokuwa haujaumbwa, lakini kutokea alitokea waziwazi siku hizi za nyuma kwa ajili yenu ninyi.[#Rom. 16:25-26; Ef. 1:4.]

21Kwake yeye mmepata kumtegemea Mungu aliyemfufua katika wafu na kumpa utukufu kwamba: Awe Mungu tu, mnayemtegemea na kumngojea.[#Yoh. 14:6.]

22Kwa kuwa mmezitakasa roho zenu na kuyatii yaliyo ya kweli, pendaneni kindugu pasipo ujanja mkijikaza kupendana kila mtu na mwenziwe kwa moyo!

23Kwani mkiwa mmezaliwa mara ya pili, siyo nguvu ya mbegu iozayo, ila ni nguvu ya mbegu isiyoozeka, ndiyo Neno la Mungu lililo lenye uzima, nalo ndilo likaalo.[#Yoh. 1:13; 3:5; Yak. 1:18.]

24Kwani

kila mwenye mwili ni kama majani,

nao uzuri wake wote ni kama ua la majani.

Majani hunyauka, nayo maua yake hupukutika.

25Lakini neno lake Bwana hukaa kale na kale.

Basi, hilo ndilo neno la mbiu njema, mpigiwayo ninyi.*

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania