1 Petero 4

1 Petero 4

Hata wafu walipigiwa mbiu njema.

1Kwa sababu Kristo aliteswa mwilini kwa ajili yetu, jipeni nanyi mioyo iliyo hivyo, iwashindishe! Kwani atesekaye mwilini huacha kukosa,

2nazo siku zake zilizosalia za kuwapo mwilini hatazimaliza na kuzifuata tamaa za watu, ila atafanya, Mungu ayatakayo.

3Kwani inatosha, ya kuwa siku zilizopita mmeyafanya, wamizimu wayatakayo, mkifuata uasherati na tamaa na ulevi na ulafi na unywaji na matambiko ya vinyago yamchukizayo Mungu.[#Ef. 2:2-3; Tit. 3:3.]

4Wale wanayastukia, ya kuwa sasa hamfuatani nao na kujipujua pasipo kiasi; kwa hiyo wanawatukana.

5Lakini atakayewalipiza ni yeye aliye tayari kuwahukumu wanaoishi nao waliokufa.[#Tume. 10:42; 2 Tim. 4:1.]

6Kwani kwa hiyo hata wafu walipigiwa mbiu njema, wahukumiwe kimwili, kama iwapasavyo watu, kisha wapate kuwapo kiroho, kama Mungu anavyokuwapo.[#1 Petr. 3:19.]

Maonyo menginemengine.

7Mwisho wa vitu vyote uko karibu. Kwa hiyo mjiangalie, mlevuke, mpate kuomba![#1 Kor. 10:11; 1 Yoh. 2:18.]

8*Lakini kupita yote: jikazeni kupendana wenyewe! Kwani upendano hufunika makosa mengi.[#Fano. 10:12; Yak. 5:20.]

9Mkaribishane pasipo kunung'unika![#Ebr. 13:2.]

10Mtumikiane ninyi kwa ninyi, kila mtu akikitumia chema chake, alichogawiwa! Hivyo mtakuwa watunzaji wazuri wa yale mema mengi ya Mungu.

11Mtu akisema na ayaseme, kama ni kusema maneno ya Mungu! Mtu akitumika na atumike kwa kuwa mtu aliyepewa nguvu na Mungu kwamba: Katika mambo yote Mungu atukuzwe kwa ajili ya Yesu Kristo! Wake yeye ni utukufu na uwezo kale na kale pasipo mwisho! Amin.*[#Rom. 12:7.]

Mateso kwa ajili ya Kristo.

12*Wapendwa, msistuke kama wenye kuona neno geni mkipatwa na mambo yenye moto! Maana mtajaribiwa tu.[#1 Petr. 1:6-7.]

13Ila mkiwa wenzake Kristo wa kuteseka changamkeni! Maana hapo, utukufu wake utakapotokea waziwazi, ndipo, mtakapochangamka na kushangilia.[#Tume. 5:41; Rom. 8:17; Yak. 1:2.]

14M wenye shangwe mkitukanwa kwa kuwa mnalo Jina lake Kristo. Kwani Roho wa utukufu na na wa Mungu anawakalia.[#1 Petr. 2:20; Mat. 5:11.]

15Lakini kwenu asioneke ateswaye kwa kuwa mwuaji au mwizi au mtenda maovu au mkaguzi wa mambo yasiyo yake!

16Lakini mtu akiteseka kwa kuwa Mkristo, asione soni, ila amtukuze Mungu kwa kuwamo katika Jina hili![#Fil. 1:20.]

17Kwani siku zimetimia, hukumu ianze kwao walio wa Nyumba ya Mungu. Basi, ikianza kwetu itakuwaje mwishoni kwao waliokataa kutii Utume mwema wa Mungu?[#Yer. 25:29; Ez. 9:6.]

18Tena mwongofu akiona: kuokoka ni kugumu, asiyemcha Mungu na mkosaji atapona wapi?[#Fano. 11:31; Luk. 23:31.]

19Kwa hiyo nasema: Wenye kuteseka kwa hayo, Mungu aliyoyataka, watende mema! Hivyo wataweza kumwagizia yeye roho zao, maana ni muumbaji mwelekevu.*[#Sh. 31:6; Luk. 23:46.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania