The chat will start when you send the first message.
1Ndipo, Samweli alipokitwaa kichupa cha mafuta, akayamiminia kichwa chake, akamnonea midomo na kumwambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyokupaka mafuta, uwe mkuu wao walio fungu lake.
2Utakapotoka kwangu leo, utaona watu wawili penye kaburi la Raheli mpakani mwa Benyamini huko Selsa, nao watakuambia: Wale punda wa kike, uliokwenda kuwatafuta, wameonekana. Tazama, baba yako ameyaacha mambo ya punda kwa kuwahangaikia ninyi akisema: Mwanangu nimfanyie nini?[#1 Mose 35:19.]
3Utakapoondoka huko kwenda zako na kufika penye mvule wa Tabori, huko watu watatu watakutana na wewe, nao wanapanda kwenda Beteli kwa Mungu, mmoja anachukua wana mbuzi watatu, mmoja mikate mitatu, mmoja kiriba cha mvinyo.
4Nao watakuamkia na kukupa mikate miwili, nawe utaipokea mikononi mwao.
5Baadaye utafika kwenye kilima cha Mungu, ngome ya Wafilisti iliko. Utakapofika huko penye mji huo utakuta kikosi cha wafumbuaji wanaoshuka kilimani pa kutambikia wakitanguliwa na mapango na matoazi na mazomari na mazeze, nao wanakwenda wakifumbua maneno.
6Ndipo, roho ya Bwana itakapokujia, ufumbue pamoja nao; ndivyo, utakavyogeuzwa kuwa mtu mwingine.[#1 Sam. 10:10.]
7Hapo, hivyo vielekezo vitakapokutukia, fanya, mkono wako utakayoyaona! kwani Mungu yuko na wewe.
8Kisha shuka kunitangulia kwenda Gilgali! Nami utaniona, nikishuka kuja kwako kutoa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na kuchinja ng'ombe za tambiko za shukrani. Utangoja siku saba, hata nitakapokuja kwako, nikujulishe utakayoyafanya.[#1 Sam. 13:8.]
9Ikawa, Sauli alipogeuka, atoke kwake Samweli, ndipo, Mungu alipougeuza moyo wake kuwa mwingine. Navyo vielekezo vile vyote vikatukia siku ile.
10Walipofika kule Gibea, wakaona kikosi cha wafumbuaji kilichokuja kukutana naye; ndipo, roho ya Mungu ilipomjia, naye akafumbua mambo katikati yao.[#1 Sam. 19:20-24.]
11Ikawa, wote waliomjua zamani zote walipomwona, ya kuwa anafumbua mambo pamoja na wafumbuaji, ndipo, watu hao waliposemezana kila mtu na mwenzake: Hivi vya mwana wa Kisi vinakuwaje? Kumbe Sauli naye yumo katika wafumbuaji?
12Mtu wa huko akajibu: Je? Baba yao ni nani? Kwa hiyo likawa fumbo la kwamba: Kumbe Sauli naye yumo katika wafumbuaji!
13Alipokwisha kufumbua mambo akaja kilimani pa kutambikia.
14Mjomba wake Sauli akamwuliza yeye na kijana wake: Mlikwenda wapi? Akajibu: Kuwatatufa wale punda wa kike; lakini tusipowaona tukaenda kwa Samweli.
15Mjomba wake Sauli akasema: Nisimulie, Samweli aliyowaambia!
16Sauli akamwambia mjomba wake: Ametupasha habari, ya kuwa wale punda wa kike wameonekana; lakini lile neno la ufalme, Samweli alilolisema, hakumsimulia.
17Kisha Samweli akawaita watu kuja kwake Bwana huko Misipa.
18Akawaambia wana wa Isiraeli: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mungu wa Isiraeli: Mimi niliwatoa Waisiraeli Misri, nikawaponya mikononi mwa Wamisri namo mikononi mwa wafalme wote waliowasumbua ninyi.
19Nanyi siku hii ya leo mmemkataa Mungu wenu aliyewaokoa katika mabaya na katika masongano yenu yote mkimwambia: Tuwekee mfalme, atutawale! Sasa jipangeni hapa machoni pake Bwana kwa mashina yenu na kwa maelfu yenu![#1 Sam. 8:7.]
20Samweli alipokwisha kuyafikisha mashina yote, wakipiga kura, likashikwa shina la Benyamini.[#1 Sam. 14:41-42.]
21Kisha alipolifikisha shina la Benyamini milango kwa milango, ukashikwa mlango wa Matiri, kisha akashikwa Sauli, mwana wa Kisi. Lakini walipomtafuta hawakumwona.
22Ndipo, walipomwuliza Bwana tena: Mtu huyu amefika kweli huku? Bwana akajibu: Mtazameni, amejificha kwenye mizigo!
23Wakapiga mbio kwenda kumchukua huko. Alipokuja kusimama katikati ya watu aliwapita watu wote kwa urefu wa kichwa, kikianza kupimwa mabegani.
24Samweli akawaambia watu wote: Mmemwona, Bwana aliyemchagua? Kwani kwao watu wote hakuna afananaye naye. Ndipo, wote walipopiga yowe za kumshangilia kwamba: Pongezi, mfalme![#1 Fal. 1:25.]
25Kisha Samweli akawaambia watu haki yake mfalme, akaiandika katika kitabu, akakiweka hapo pake Bwana; kisha Samweli akawaaga watu wote, waende zao kila mtu nyumbani kwake.[#1 Sam. 8:11; 5 Mose 17:14-20.]
26Naye Sauli akaenda zake nyumbani kwake huko Gibea, nao vijana wenye nguvu, Mungu aliowahimiza mioyoni, wakamsindikiza.
27Lakini watu wasiofaa kitu wakasema: Huyu atatuokoaje? Wakambeza, hawakumletea matunzo. Lakini yeye akawa, kama hakuyasikia, waliyoyasema.[#1 Sam. 11:12.]