The chat will start when you send the first message.
1Watu wakamsimulia Dawidi kwamba: Wafilisti wanapiga vita huko Keila, nao hunyang'anya yaliyopo penye kupuria.[#Yos. 15:44.]
2Dawidi akamwuliza Bwana kwamba: Niende, niwapige hao Wafilisti? Bwana akamwambia Dawidi. Nenda, uwapige hao Wafilisti, uuokoe mji wa Keila!
3Lakini watu wa Dawidi wakamwambia: Tazama, huku katika nchi ya Yuda tunakaa na kuogopa; basi, tutakwendaje Keila, Wafilisti walikojipanga?
4Ndipo, Dawidi alipomwuliza Bwana mara ya pili; naye Bwana akamjibu na kusema: Ondoka, ushukie Keila! Kwani mimi nitawatia Wafilisti mkononi mwako.
5Kisha Dawidi akaenda Keila na watu wake, akapigana na Wafilisti, akateka mbuzi na kondoo wao, akawapiga pigo kubwa; ndivyo, Dawidi alivyowaokoa wenyeji wa Keila.[#1 Sam. 19:8.]
6Ikawa, Abiatari, mwana na Ahimeleki, alipomkimbilia Dawidi kule Keila alishuka na kukishika kisibau cha mtambikaji mkononi.[#1 Sam. 22:20.]
7Sauli alipopashwa habari, ya kuwa Dawidi ameingia Keila, Sauli akasema: Mungu amemwumbua na kumtia mkononi mwangu, kwani alipoingia mji wenye milango na makomeo amekwisha kufungiwa humo.
8Kisha Sauli akawaita watu wote kuja vitani, waushukie Keila kumsonga Dawidi na watu wake kwa kuwazinga.
9Dawidi alipojua, ya kuwa Sauli amewaza kumfanyizia mabaya, akamwambia mtambikaji Abiatari: Kilete kisibau cha mtambikaji![#1 Sam. 30:7.]
10Kisha Dawidi akaomba: Bwana Mungu wa Isiraeli, msikilize vema mtumishi wako! Kwani Sauli anatafuta njia ya kuingia Keila, auangamize mji huu kwa ajili yangu mimi.
11Sasa je? Wenyeji wa Keila watanitoa na kunitia mkononi mwake Sauli, atakaposhuka, kama mtumishi wako alivyosikia? Bwana Mungu wa Isiraeli, hili mwambie mtumishi wako! Bwana akasema: Atashuka.
12Dawidi akauliza tena: Wenyeji wa Keila watanitoa mimi na watu wangu na kututia mkononi mwa Sauli? Bwana akasema: Watawatoa.
13Ndipo, Dawidi alipoondoka na watu wake waliokuwa kama 600, wakatoka Keila, wakajiendea kwa kujiendea tu. Sauli alipopashwa habari, ya kuwa Dawidi amejiponya na kutoka Keila akaacha kuuendea.
14Kisha Dawidi akakaa nyikani magengeni, zaidi akakaa milimani katika nyika ya Zifu. Sauli akamtafuta siku zote, lakini Mungu hakumtia mkononi mwake.[#1 Sam. 23:19; 24:1.]
15Dawidi alipoona, ya kuwa Sauli ametoka, apate kuizimisha roho yake, alikuwa mwituni katika nyika ya Zifu.
16Ndipo, Yonatani, mwana wa Sauli, alipoondoka kwenda kwake Dawidi kule mwituni, akaushupaza mkono wake kwa nguvu za Mungu.
17Akamwambia: Usiogope! Kwani mkono wa baba yangu Sauli hautakupata, ila wewe utakuwa mfalme wao Waisiraeli, nami nitakuwa wa pili akufuataye; hata baba yangu Sauli anayajua haya.[#1 Sam. 20:30-31; 24:21.]
18Kisha wote wawili wakafanya agano machoni pa Bwana; Dawidi akakaa kule mwituni, naye Yonatani akaenda nyumbani kwake.[#1 Sam. 18:3.]
19Kulikuwako Wazifu waliopanda Gibea kwa Sauli kumwambia: Je? Dawidi hajifichi kwetu magengeni mwituni katika kilima cha Hakila kilichoko kusini kwenye jangwa?[#1 Sam. 26:1; Sh. 54:2.]
20Sasa wewe mfalme, shuka tu kwa hivyo, roho yako inavyotamani kabisa kushuka! Nasi tutamtoa, tumtie mkononi mwa mfalme.
21Sauli akasema: Na mbarikiwe na Bwana, kwa kuwa mmenihurumia!
22Nendeni kumvumbua tena, mpate kujua na kupaona mahali pake panapo nyayo zake, mmjue naye aliyemwona. Kwani watu huniambia, ya kuwa ni mwerevu sanasana.
23Tazameni, myajue maficho yote pia, anamojificha! Kisha rudini kwangu kwa hayo, mliyoyavumbua, nipate kwenda nanyi! Kama yuko katika nchi hii, nitamtafuta, nimpate katika maelfu yote ya Yuda.
24Kisha wakaondoka, wakaenda Zifu mbele ya Sauli; lakini Dawidi na watu wake walikuwa porini katika nyika ya Maoni upande wa kusini kwenye jangwa.
25Sauli alipokwenda na watu wake kumtafuta, watu wakampasha Dawidi habari; ndipo, aliposhuka mwambani, akakaa katika nyika ya Maoni. Sauli aliposikia, akaja upesi kumfuata kule nyikani kwa Maoni.
26Sauli akashika njia ya upande wa huku wa mlima ule, naye Dawidi na watu wake wakashika njia ya upande wa huko wa mlima uleule, lakini Dawidi akajihimiza kumkimbia Sauli. Hapo, Sauli na watu wake walipomfikia Dawidi na watu wake na kuwazunguka, wawakamate,
27ndipo, mjumbe alipofika kwa Sauli kwamba: Uje mbiombio, kwani Wafilisti wanaiteka nchi hii!
28Ndipo, Sauli alipoacha kumkimbiza Dawidi, akawageukia Wafilisti, kwa hiyo wakapaita mahali pale Mwamba wa Matengano.
29Kisha Dawidi akaondoka hapo, akakaa magengeni huko Engedi.