The chat will start when you send the first message.
1Siku zile Samweli akafa; ndipo, Waisiraeli wote walipokusanyika kumwombolezea na kumzika nyumbani kwake huko Rama. Kisha Dawidi akaondoka, akatelemka kwenda nyikani kwa Parani.[#1 Sam. 28:3.]
2Kule Maoni kulikuwa na mtu, nako, alikopatia mali, ni Karmeli; mtu huyo alikuwa mkuu kabisa mwenye kondoo 3000 na mbuzi 1000. Naye siku hizo alikuwa huko Karmeli akiwakata kondoo wake manyoya.
3Huyo mtu jina lake Nabali, naye mkewe jina lake Abigaili; huyu mkewe alikuwa mwenye akili njema na mwenye umbo zuri, lakini yule mume alikuwa mkorofi mwenye matendo mabaya tu, naye ni wa mlango wa Kalebu.
4Dawidi aliposikia kule nyikani, ya kuwa Nabali yumo katika kukata manyoya ya kondoo wake,
5Dawidi akatuma vijana kumi; Dawidi akawaambia hao vijana: Pandeni Karmeli, mwende kwa Nabali kunisalimia kwake!
6Mmwambieni huyu ndugu yangu: Hujambo wewe? Nao wa mlango wako hawajambo? Nao wote walio wako hawajambo?
7Sasa nimesikia, ya kuwa wanakukatia manyoya ya kondoo wako; basi, hao wachungaji wako walikuwa kwetu sisi, nasi hatukuwafanyizia kibaya cho chote, wala hakikupotea cho chote kwao siku zote, walipokuwa huku Karmeli.
8Waulize vijana wako, nao watakuambia, kwa hiyo hawa vijana na waone upendeleo machoni pako! Kwani tumekuja siku iliyo njema; mkono wako utakayoyaona, tupe sisi watumishi wako naye mtumishi wako Dawidi!
9Vijana wa Dawidi walipofika kwake wakamwambia Nabali hayo maneno yote katika jina la Dawidi, kisha wakanyamaza.
10Lakini Nabali akawajibu vijana wa Dawidi kwamba: Dawidi ni nani? Mwana wa Isai ni nani? Leo watumwa waliotoroka kwa bwana zao ni wengi.
11Sasa je? Vilaji vyangu na vinyaji vyangu na vinono vyangu, nilivyowachinjia wanaokata manyoya ya kondoo wangu, nivichukue, niwape watu, nisiowajua, wanakotoka?
12Ndipo, vijana wa Dawidi walipogeuka kurudi kwao; walipofika wakampasha habari hizo zote.
13Ndipo, Dawidi alipowaambia watu wake: Jifungeni kila mtu upanga wake! Nao wakajifunga kila mtu upanga wake, hata Dawidi akajifunga upanga wake; wakamfuata Dawidi watu kama 400 kwenda naye, wengine 200 wakasalia kwenye mizigo yao.
14Kijana mmoja miongoni mwao wale vijana akamsimulia Abigaili, mkewe Nabali, kwamba: Tazama! Dawidi ametuma wajumbe toka nyikani, waje kumsalimia bwana wetu, lakini akawafokea.
15Nao wale watu wametufanyizia mema sana, hawakutufanyizia kibaya cho chote, wala hakikupotea kwetu cho chote siku zote, tulizotembea nao tulipokuwa porini.
16Walikuwa kwetu kama boma usiku na mchana siku zote, tulizokuwa kwao tukichunga kondoo.
17Sasa yajue hayo, uone utakayoyafanya! Kwani yako mabaya yaliyokwisha kutengenezwa ya kumpata bwana wetu na mlango wake wote; lakini yeye ni mtu asiyefaa, hatuwezi kusema naye.
18Ndipo, Abigaili alipojihimiza, akachukua mikate 200 na mitungi 2 ya mvinyo na kondoo 5 waliokwisha kutengenezwa na pishi 5 za bisi na maandazi 100 ya zabibu na 200 ya kuyu, yote pia akapagaza punda.
19Kisha akawaambia vijana wake: Nitangulieni! Mimi nitawafuata nyuma. Lakini mumewe Nabali hakumwambia neno.
20Ikawa, alipokuwa amepanda punda wake na kutelemka mahali palipofichwa na mlima, naye Dawidi na watu wake walikuwa wakitelemka papo hapo upande wa huko; ndivyo, alivyokutana nao.
21Dawidi akawa akiwaza moyoni kwamba: Kumbe mali zote za mtu huyu nimezilinda nyikani bure tu, yote pia yaliyokuwa yake hayakupotea hata moja, naye hayo mema akayalipa kwa kunifanyizia mabaya.
22Mungu na awafanyizie wachukivu wote wa Dawidi hivi na hivi, nikisaza mpaka mapambazuko ya kesho mtu mmoja tu wa kiume kwao wote walio watu wake![#1 Fal. 14:10.]
23Abigaili alipomwona Dawidi akashuka upesi katika punda wake, akajiangusha kifudifudi mbele ya Dawidi kumwangukia hapo chini.
24Kisha akasema na kumpigia magoti: Unilipishe mimi tu huo uovu, bwana wangu! Acha, kijakazi wako aseme masikioni pako, uyasikilize maneno ya kijakazi wako!
25Naomba sana, bwana wangu asiyaweke moyoni mwake mambo ya mtu huyu asiyefaa, huyu Nabali, kwani kama jina lake lilivyo, ndivyo, alivyo kweli: jina lake ni Nabali (Mjinga), nao ujinga anao kabisa. Lakini mimi kijakazi wako sikuwaona wale vijana, wewe bwana wangu uliowatuma.
26Sasa bwana wangu, kwa hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, tena kwa hivyo, mwenyewe ulivyo mzima, Bwana amekuzuia, usije kumwaga damu, ukijilipiza kwa mkono wako mwenyewe. Sasa wachukivu wako nao wote wanaomtakia bwana wangu mabaya na wawe kama Nabali!
27Sasa matunzo haya, kijakazi wako anayomletea bwana wangu, na wapewe vijana wanaozifuata nyayo za bwana wangu.
28Mwondolee kijakazi wako, kama amefanya kipotovu! Kwani Bwana atamtengenezea bwana wangu nyumba yenye nguvu, kwani bwana wangu anampigia Bwana vita, nayo mabaya hayaoneki kwako siku zako zote.
29Mtu atakapoondokea akukimbize na kutafuta njia ya kukuua, ndipo, roho ya bwana wangu itakapokuwa imefungwa vema kifungoni kwao wanaoishi kwake Bwana Mungu wako. Lakini roho za wachukivu wako na azitupe, kama kombeo linavyotupa vijiwe, vikitiwa hapo kati.
30Hapo, Bwana atakapomfanyizia bwana wangu hayo mema yote, aliyokuambia, na kukuweka kuwa mkuu wa kuwatawala Waisiraeli,[#2 Sam. 5:2.]
31hapo halitakutonesha, halitaukwaza moyo wa bwana wangu hilo la kwamba: ulimwaga damu bure tu, upate kujiponya mwenyewe, wewe bwana wangu. Kwa hiyo mkumbuke kijakazi wako hapo, Bwana atakapomfanyizia mema bwana wangu.
32Dawidi akamwambia Abigaili: Na atukuzwe Bwana Mungu wa Isiraeli aliyekutuma siku hii ya leo kukutana na mimi!
33Na yatukuzwe nayo mawazo yako! Na utukuzwe wewe nawe! Kwani umenizuia leo kukora manza za damu, nikitaka kujiponya kwa nguvu za mkono wangu.
34Kwa hivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli aliyenizuia, nisikufanyizie kibaya, alivyo Mwenye uzima, kama usingalipiga mbio kuja kukutana na mimi, kweli kwao walio wa Nabali asingesazwa mpaka mapambazuko ya kesho mtu wa kiume hata mmoja tu.
35Kisha Dawidi akapokea mkononi mwake aliyomletea akimwambia: Nenda na kutengemana nyumbani kwako! Tazama, nimekusikia sauti yako, nikaukweza uso wako!
36Abigaili alipofika kwa Nabali akamkuta, akinywa na wenzake nyumbani mwake, kama mfalme anavyokunywa na wageni wake, nao moyo wake Nabali ukawa ukichangamka kwa kulewa kabisa. Kwa hiyo hakumwambia neno kubwa wala dogo mpaka mapambazuko ya kesho.
37Ikawa asubuhi, Nabali alipolevuka kwa zile mvinyo, alizozinywa, mkewe akamsimulia mambo hayo; ndipo, moyo wake ulipozimia kifuani mwake, naye akawa kama jiwe.
38Siku kumi zilipopita, Bwana akampiga Nabali, akafa
39Dawidi aliposikia, ya kuwa Nabali amekufa, akasema: Na atukuzwe Bwana, kwa kuwa amenigombea huo ugomvi wenye soni, Nabali alionipatia, akamzuia mtumishi wake, asifanye mabaya, nayo mabaya ya Nabali Bwana akayarudisha kumjia kichwani pake. Kisha Dawidi akatuma watu kusema na Abigaili, apate kumchukua, awe mkewe.
40Watumishi wa Dawidi walipofika kwake Abigaili huko Karmeli wakasema naye kwamba: Dawidi ametutuma kwako, akuchukue, uwe mkewe.
41Naye akainuka, akawaangukia hapo chini mara mbili, akasema: Tazameni, kijakazi wenu yuko tayari kuwatumikia watumishi wa bwana wangu na kuwaogesha miguu.
42Kisha Abigaili akaondoka upesi, akapanda punda, vijana wa kike watano wakimfuata nyayo zake, naye akawafuata wajumbe wa Dawidi, akawa mkewe.[#1 Sam. 27:3; 30:5.]
43Naye Ahinoamu wa Izireeli Dawidi akamchukua, wote wawili wakawa wakeze.
44Naye Sauli akamwoza mwanawe Mikali aliyekuwa mkewe Dawidi kuwa mkewe Palti, mwana na Laisi wa Galimu.[#2 Sam. 3:15.]