The chat will start when you send the first message.
1Kulikuwa na mtu wa Benyamini, jina lake Kisi, mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorati, mwana wa Afia, mwana wa mtu wa Benyamini, naye alikuwa fundi wa vita mwenye nguvu.
2Alikuwa na mwana wa kiume, jina lake Sauli, naye alikuwa kijana mzuri mno, kwa Waisireli hakuwako mtu mzuri zaidi kuliko yeye, naye aliwapita watu wote kwa urefu wa kichwa kimoja, kikianza kupimwa mabegani.
3Punda wa kike wa Kisi, babake Sauli, walipopotea, Kisi akamwambia mwanawe Sauli: Chukua mmoja wao vijana, uondoke kwenda kuwatafuta hao punda!
4Basi, akapitia milimani kwa Efuraimu, kisha akapitia hata katika nchi ya Salisa, lakini hakuwaona. Kisha akapitia katika nchi ya Saalimu, nako walikuwa hawako. Kisha akapitia katika nchi ya Benyamini, lakini hawakuwaona.[#Yoh. 3:23.]
5Kisha wakaingia katika nchi ya Sufu; ndipo, Sauli alipomwambia yule kijana, aliyekuwa naye: Haya! Na turudi, baba asiwaache wale punda, akatuhangaikia sisi.[#1 Sam. 10:2.]
6Naye akamwambia: Tazama! Humu mjini yumo mtu wa Mungu, naye ni mwenye macheo, kwani yote, anayoyasema, hutimia; sasa twende huko, labda atatuonyesha njia, tutakayoishika.
7Sauli akamwambia huyo kijana wake: Tazama! Tukienda, tutampelekea nini yule mtu? Kwani pamba zetu zimekwisha katika vyombo vyetu, hata tunzo hatunalo la kumpelekea yule mtu wa Mungu. Kiko nini, tulicho hacho?
8Yule kijana akamjibu Sauli tena akisema: Tazama, mkononi mwangu imeonekana thumuni! Hii nitampa yule mtu wa Mungu, atuonyeshe njia yetu.
9Hapo kale kwao Waisiraeli mtu alipokwenda kumwuliza Mungu husema: Haya! Twende kwa mtazamaji! Kwani mfumbuaji wa leo kale huitwa mtazamaji.[#4 Mose 21:3; 2 Fal. 17:13; 1 Mambo 9:22.]
10Sauli akamwambia kijana wake: Neno lako ni jema; haya! Twende! Wakaja mle mjini, yule mtu wa Mungu alimokuwa.
11Wao walipokwea hapo pa kupandia kwenda mjini wakaona vijana wa kike waliotoka kuchota maji, wakawauliza hao: Mtazamaji yuko wapi humu?
12Wakawajibu na kuwaambia: Tazama, yuko mbele yako! Piga mbio sana! Kwani ameingia leo humu mjini, kwa kuwa leo watu wanatambika huko kilimani pa kutambikia.
13Mtakapoingia mjini, mtamkuta, hajapanda kilimani kula, kwani watu hawali, mpaka aje, kwani yeye kwanza sharti aibariki ng'ombe ya tambiko, kisha waalikwao hula. Sasa pandeni! Kwani siku kama hii ya leo mtamwona.
14Walipopanda mjini na kuingia humo mjini kati, mara Samweli akatokea, akakutana nao akitaka kupanda kilimani pa kutambikia.
15Nayo siku hiyo iliyotangulia kufika kwake Sauli Bwana alikuwa amemfumbulia Samweli masikioni mwake kwamba:
16Kesho wakati huu nitatuma kwako mtu wa nchi ya Benyamini; yeye ndiye, utakayempaka mafuta, awe mkuu wao walio ukoo wangu wa Waisiraeli. Naye ndiye atakayewaokoa walio ukoo wangu mikononi mwa Wafilisti, kwani nimewaona walio ukoo wangu, navyo vilio vyao vimefika kwangu.
17Samweli alipomwona Sauli, Bwana akamwambia: Tazama, yule mtu, niliyekuambia, anakuja kwako! Yeye ndiye atayewatawala walio ukoo wangu.
18Sauli akamkaribia Samweli langoni katikati na kumwambia: Niambie, nyumba ya mtazamaji iliko!
19Samweli akamjibu Sauli kwamba: Mtazamaji ni mimi; unitangulie kwenda huko kilimani pa kutambikia! Leo mtakula pamoja nami, kesho nitakuaga nikiisha kukuambia yote yaliyomo moyoni mwako.
20Nao wale punda wa kike waliokupotelea leo siku ya tatu usiwahangaikie moyoni mwako! kwani wameonekana. Kumbe mema yote ya Waisiraeli siyo yako na ya mlango wote wa baba yako?
21Sauli akajibu kwamba: Mimi si mwana wa Benyamini, nalo silo shina lililo dogo kuliko mengine ya Waisiraeli? Nao ukoo wangu ni mdogo kuliko koo zote za shina la Benyamini, mbona unaniambia maneno kama hayo?[#1 Sam. 15:17.]
22Kisha Samweli akamchukua Sauli na kijana wake, akawapeleka chumbani, walimolia ng'ombe ya tambiko, akawaketisha juu kwao walioalikwa, nao walikuwa kama watu 30.
23Samweli akamwambia mpishi: Lete hicho kipande, nilichokupa na kukuambia: Kiweke kwako!
24Mpishi akachukua paja pamoja na nyama zilizoshikana nalo, akamwandalia Sauli. Samweli akamwambia Sauli: Tazama iliyosazwa! Jiandalie, ule! Kwani niliposema: Nimewaalika watu, umewekewa nyama hii kuwa ya saa hiihii. Basi, siku hiyo Sauli akala pamoja na Samweli.
25Kisha wakatelemka wakitoka kilimani pa kutambikia kwenda mjini, naye Samweli akaja kuongea na Sauli darini.
26Walipoamka asubuhi, mapambazuko yalipotokea, Samweli akamwita Sauli huko darini kwamba: Inuka, nikusindikize! Ndipo, Sauli alipoinuka, wakatoka wote wawili, yeye na Samweli, kwenda nje.
27Walipotelemka, wafike mwishoni kwa mji, Samweli akamwambia Sauli: Mwambie kijana huyu, apite kwenda mbele yetu! Alipopita kwenda mbele, akasema: Lakini wewe simama sasa, nikuambie neno la Mungu!