The chat will start when you send the first message.
1*Pamesalia, ndugu, tuwahimize na kuwabembeleza, kwa hivyo, mlivyo wake Bwana Yesu, mfanye mwenendo uwapasao wa kumpendeza Mungu ulivyo.
2Kwani mwayajua maagizo, tuliyowaagiza, kama tulivyoyapata kwake Bwana Yesu.
3Kwani haya ndiyo, Mungu ayatakayo: mtakaswe, mwuepuke ugoni.
4Kila mmoja wenu ajue kuuangalia mwili wake, uwepo ukitakata na kupata heshima iupasayo,[#1 Kor. 6:13,15.]
5usivurugikane na tamaa na kijicho, kama wamizimu walivyofanya, wasiomjua Mungu!
6Katika jambo hili mtu asiupite mpaka akimdanganya ndugu yake, kwani Bwana ndiye atakayeyalipizia hayo yote, kama tulivyowaambia kale na kuwashuhudia.
7Kwani Mungu hakutuitia kuwa wenye uchafu, ila tuje, tutakaswe.
8Basi, kwa hiyo mtu akiyatangua haya, hatangui ya mtu, ila yake Mungu aliyewapa ninyi Roho wake Mtakatifu, awakalie.[#Luk. 10:16.]
9Kwa ajili ya upendano ninyi hampaswi na kuandikiwa neno, kwani ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana.[#Yer. 31:33-34; Yoh. 13:34.]
10Nanyi mnawafanyia hivi ndugu wote katika nchi yote ya Makedonia. Lakini twawaonya ninyi, ndugu, lifulizieni jambo hili!
11Uchuchumieni utulivu, mpate kuyafuata mambo yenu wenyewe na kufanya kazi kwa mikono yenu, kama tulivyowaagiza![#Ef. 4:28; 2 Tes. 3:8,12.]
12Sharti mfanye mwenendo uwafaliao wale watu wa nje, kwao msitake mtu wo wote wa kuwasaidia.*[#Kol. 4:5.]
13*Lakini, ndugu, hatutaki, ninyi mkose kujua, mambo yao waliolala yalivyo, msione masikitiko kama wale wengine wasio na kingojeo.[#1 Kor. 15:20; Ef. 2:12.]
14Kwani tukiyategemea, ya kuwa Yesu alikufa, kisha akafufuka tena, vivyo hivyo Mungu nao waliolala katika Yesu atawapeleka, wawe pamoja naye.[#Rom. 14:9; 1 Kor. 15:3-4,12.]
15Kwani neno hili, tunalowaambia, ni neno lake Bwana kwamba: Sisi tunaoishi, tuliosazwa, mpaka Bwana atakapokuja, hatutawatangulia wale waliolala.[#Mat. 16:28; 24:30-31; 1 Kor. 15:51.]
16Kwani Bwana mwenyewe atashuka toka mbinguni papo hapo, wito utakapovumika, nayo sauti ya malaika mkuu itasikilika, hata baragumu la Mungu litalia. Ndipo, waliokufa katika Kristo watakapofufuka kwanza;[#1 Kor. 15:23,52.]
17kisha sisi tuliosazwa, tutakaokuwa tu hai, tutapokonywa katika mawingu pamoja nao hao, tupate kukutana na Bwana angani. Hivyo tutakuwa pamoja na Bwana siku zote.[#Yoh. 12:26; 17:24.]
18Tulizaneni mioyo ninyi kwa ninyi na kisimuliana maneno haya!*