1 Timoteo 4

1 Timoteo 4

Ujanja wao wenye kukataza kuoa.

1Lakini Roho anasema waziwazi: Siku za mwisho watakuwako watakaoacha kumtegemea Mungu, wakifuata rohoroho za upotevu na mafundisho ya mapepo:[#Mat. 24:24; 2 Tim. 3:1; 2 Petr. 3:3; 1 Yoh. 2:18; Yuda 18.]

2ndio watu waliodanganywa nao wanaojitendekeza kwa kusema uwongo na kwa kuficha, ya kuwa wenyewe wamechomwa moto mioyoni kwa kufanya hivyo.

3Ndio wanaokataza watu kuoa, tena hutangaza miiko ya vyakula, Mungu alivyoviumba, wavile na kushukuru, wakiwa wenye kumtegemea na kuyatambua yaliyo ya kweli.[#1 Mose 9:3-4; 1 Kor. 10:30-31.]

Upato wa kumcha Mungu.

4*Kwani kila kilichoumbwa na Mungu ni kizuri, wala hakuna chenye mwiko kinacholiwa, watu wakimshukuru.[#1 Mose 1:31; Tume. 10:15.]

5Kwani kinatakaswa kwa neno lake Mungu, watu wanapokiombea.

6Ukiwafundisha ndugu mambo hayo utakuwa mtumishi mzuri wa Kristo Yesu, nawe utajilisha maneno, tuyategemeayo, tunayoyafundisha kwamba: Ni mazuri; ni hayo, uliyoyafuata nawe.

7Lakini yale masimulio yasiyo na maana, yapendezayo wazee wa kike tu, yakatae! Jizoeze kumcha Mungu![#1 Tim. 1:4; 6:20; 2 Tim. 2:16,23; Tit. 1:14; 3:9.]

8Kwani mazoezo ya mwili hufalia mambo machache tu; lakini kumcha Mungu hufalia mambo yote, tena kunacho kiago cha uzima wa sasa na cha ule utakaokuwapo.[#1 Tim. 6:6.]

9Neno hili ni la kweli, nalo linapasa kushikwa na watu wote.[#1 Tim. 2:3-4.]

10Kwani kwa sababu hii twasumbuka tukigombezwa, ya kuwa tumemngojea Mungu Mwenye uzima aliye mwokozi wa watu wote, kwanza wao wamtegemeao.

11Mambo haya uyaagize na kuyafundisha!*

12Mtu asikubeze kwamba: U kijana bado! Ila wenye kumtegemea Mungu uwe kielezo chao cha kujifundishia kusema na kuendelea na kupendana na kumtegemea Mungu na kujitakasa.[#Tit. 2:15.]

13Mpaka nitakapofika, ufulize kuwasomea na kuwaonya na kuwafundisha![#Kol. 4:16; 1 Tes. 5:27.]

14Usiache kuyatunza yale mema, uliyogawiwa kwa kufumbuliwa kwanza, kisha ukayapata kwa kubandikiwa mikono ya wazee.[#1 Tim. 1:18; 5:22; Tume. 6:6; 8:17.]

15Mambo hayo uyatunze, ushikamane nayo, wote wapate kuona, unavyoendelea!

16Jiangalie mwenyewe, uyaangalie nayo, unayoyafundisha, ujikaze yayo hayo! Kwani ukiyafanya hayo utajiokoa mwenyewe, hata wanaokusikia.[#Rom. 11:14.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania