The chat will start when you send the first message.
1Aliye mzee usimkaripie, ila umbembeleze, kama ni baba yako! Walio waume wazima useme nao, kama ni ndugu zako![#3 Mose 19:32.]
2Wanawake wazee nao uwabembeleze, kama ni mama zako! Walio wake wazima useme nao na kuyaangalia yote yenye soni, kama ni dada zako!
3Wanawake wajane walio wajane kweli uwaheshimu![#1 Tim. 5:5.]
4Lakini mwanamke mjane akiwa na watoto au wajukuu, basi, hao wajifunze kwanza kuwaheshimu walio nao nyumbani mwao wenyewe, wakiwalipa wamama na wabibi mema, walioyapata kwao! Kwani hivi vinapendezeka mbele ya Mungu.
5Lakini aliye mjane wa kweli ni yule aliyeachwa peke yake tu; yeye humngojea Mungu akifuliza kumwomba Mungu na kuwaombea wengine usiku na mchana.[#Luk. 2:37.]
6Lakini anayezifuata tamaa zake huyo amekwisha kufa akingali yupo bado.
7Mambo haya uyaagize, watu wasione neno la kuwaonya!
8Lakini mtu asipowatunza walio ndugu zake, kupita wengine wale waliomo nyumbani mwake, basi, huyo amekwisha kumkana, aliyemtegemea, naye ni mwovu kuliko wale wasiomtegemea Mungu.
9Mwanamke mjane apaswaye na kuandikiwa ujane ni yule aliyemaliza miaka 60, aliyekuwa mke wa mume mmoja;
10nayo matendo yake sharti yajulikane kuwa mazuri, kama kukuza watoto au kupenda wageni au kuosha watakatifu miguu au kusaidia wenye maumivu au kufuata matendo mema yawayo yote.[#Ebr. 13:2.]
11Lakini wajane, wasiomaliza bado ile miaka, uwakatae! Kwani hao wangawa wamtumikia Kristo, watakapoingiwa na tamaa ya mume, wanataka kuolewa,
12ijapo wajiumbue kwamba: Hivyo, walivyomtegemea Mungu kwanza, wamevitangua.[#Ufu. 2:4.]
13Vilevile hujizoeza kuwa wavivu na kutangatanga nyumba kwa nyumba. Nao si wavivu tu, ila wanao upuzi mwingi, hunyatia wengine, husema yasiyopasa.
14Kwa hiyo nataka, wasio wazee waolewe, wazae watoto, wayaangalie mambo ya nyumbani mwao, mpingani wasimsengenyeshe,[#1 Kor. 7:9.]
15kwani hivyo wako waliogeuka wakimfuata Satani.
16Lakini mwanamke mwenye kumtegemea Mungu akiwa na wajane mwake, na awatunze, wateule wasilemewe, wapate kuwatunza walio wajane kweli.[#Tume. 6:1.]
17Wazee wanaosimamia vizuri sharti wapewe heshima mara mbili, kupita wengine ni wale wanaojisumbua kulitumikia lile Neno kwa kulifundisha.[#Tume. 14:23; Rom. 12:8.]
18Kwani Maandiko yasema:
Ng'ombe mwenye kupura ngano usimfunge kinywa!
Na tena:
Mtenda kazi hupaswa na kupewa mshahara wake.
19Mzee akisutwa, ukatae, wasipokuwapo mashahidi wawili au watatu![#5 Mose 19:15; Mat. 18:16-17; 2 Kor. 13:1.]
20Wakosao uwaonye mbele yao wote, wale wengine nao wapate kuogopa![#Gal. 2:14.]
21Namtaja Mungu na Kristo Yesu nao malaika waliochaguliwa kuwa mashahidi nikikuagiza sasa, uyashike maneno haya, nalo utakalolifanya lo lote, ulifanye pasipo kuchukizwa wala pasipo kupendezwa na mtu!
22Usimbandikie mtu mikono upesi! Wala usijitie katika makosa ya wengine! Jiangalie, uwe mng'avu![#1 Tim. 4:14.]
23Usifulize kunywa maji tu, ila utumie mvinyo kidogo kwa ajili ya tumbo lako, likipatwa na manyonge mara kwa mara!
24Watu wengine makosa yao yako waziwazi, huwaongoza na kuwapeleka penye hukumu; lakini wengine makosa yao hutokea nyuma yao.
25Vivyo hivyo nayo matendo mazuri mengine yako waziwazi; nayo yasiyo waziwazi hayafichiki.