2 Mambo 10

2 Mambo 10

Rehabeamu anaupata ufalme.

(Taz. 1 Fal. 12:1-19.)

1Rehabeamu akaenda Sikemu, kwani Waisiraeli wote walifikia Sikemu kumpa ufalme.[#1 Fal. 11:40.]

2Naye Yeroboamu, mwana wa Nebati, alikuwa huko Misri, alikokimbilia alipomkimbia mfalme Salomo; lakini alipopashwa hizo habari akarudi toka Misri.

3Wakamwita, naye akaja na Waisiraeli wote, wakamwambia Rehabeamu kwamba:

4Baba yako alitutwisha mzigo mzito, sasa wewe utupunguzie ule utumwa mgumu wa baba yako nao mzigo wake mzito, aliotutwisha! Kisha tutakutumikia.

5Akawaambia: Kwanza nendeni siku tatu, kisha rudini kwangu! Watu walipokwenda zao,

6mfalme Rehabeamu akafanya shauri na wazee waliomtumikia baba yake Salomo, alipokuwa mzima bado, akawauliza: Ninyi shauri lenu ni nini? Watu hawa tuwape majibu gani?

7Wakamwambia hivi: Ukijulikana kwao watu hawa kuwa mwema, ukiwapendeza na kuwaambia maneno mema, ndipo, watakapokuwa watumishi wako siku zote.

8Lakini akaliacha shauri la wazee, walilompa, akafanya shauri na vijana waliokua naye na kumtumikia,

9akawauliza: Ninyi shauri lenu ni nini? Tuwape majibu gani watu hawa walioniambia: Tupunguzie mzigo, aliotutwisha baba yako?

10Vijana hawa waliokuwa naye wakasemezana naye kwamba: Haya ndiyo, uwaambie watu waliokuambia kwamba: Baba yako aliukuza mzigo wetu kuwa mzito, wewe utupunguzie huu mzigo wetu, basi, uwaambie hivyo: Kidole changu kidogo na kinenepe kuliko viuno vya baba yangu;

11sasa vitakuwa hivi: kama baba yangu aliwatwisha mzigo mzito, mimi nitauzidisha mzigo wenu; kama baba yangu aliwapiga fimbo, mimi nitawapiga viboko vyenye miiba.

Ufalme wa Dawidi unagawanyika.

12Yeroboamu na watu wote wakaja kwake Rehabeamu siku ya tatu, kama mfalme alivyosema kwamba: Rudini siku ya tatu!

13Ndipo, mfalme alipowapa majibu magumu, yeye Rehabeamu akiliacha shauri la wazee,

14akasema nao na kulifuata shauri la vijana, akawaambia: kama baba yangu aliwatwisha mzigo mzito, mimi nitauzidisha; kama baba yangu aliwapiga fimbo, mimi nitawapiga viboko vyenye miiba.

15Mfalme hakuwasikia wale watu, kwani Mungu aliyageuza kuwa hivyo, yeye Bwana apate kulitimiza neno lake, alilomwambia Yeroboamu, mwana wa Nebati, kinywani mwa Ahia wa Silo.[#1 Fal. 11:29,31.]

16Waisiraeli wote walipoona, ya kuwa mfalme hakuwasikia, ndipo, watu walipomjibu mfalme kwamba: Sisi tuna bia gani na Dawidi? Hatuna fungu lo lote kwake mwana wa Isai. Waisiraeli, haya! Rudini sasa mahemani kwenu, kila mtu kwake! Nawe Dawidi, na uuangalie mwenyewe mlango wako! Ndipo, Waisiraeli wote walipokwenda mahemani kwao.

17Ni wana wa Isiraeli waliokaa katika miji ya Yuda tu, Rehabeamu aliowapata, awe mfalme wao.

18Mfalme Rehabeamu alipomtuma Hadoramu aliyekuwa msimamizi wa kazi za nguvu, wana wa Isiraeli wakampiga mawe, hata akafa. Kisha mfalme Rehabeamu akajihimiza kupanda garini na kukimbilia Yerusalemu.

19Ndivyo, Waisiraeli walivyojitenga na mlango wa Dawidi mpaka siku ya leo.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania