2 Mambo 15

2 Mambo 15

Mfumbuaji Azaria anamshikiza Asa.

1Roho ya Mungu ikaja kumkalia Azaria, mwana wa Odedi,

2akamtokea Asa, akamwambia: Nisikilizeni, wewe Asa nanyi nyote Wayuda na Wabenyamini: Bwana yuko pamoja nanyi, mkiwa naye; mkimtafuta, atawaonekea ninyi, lakini mkimwacha, atawaacha nanyi.

3Siku nyingi Waisiraeli walikuwa pasipo Mungu wa kweli, pasipo mtambikaji aliyewafundisha Maonyo.[#Hos. 3:4.]

4Waliposongeka wakamrudia Bwana Mungu wa Isiraeli, wakamtafuta, naye akawaonekea.[#Yer. 29:13-14.]

5Siku zile hawakupata kutengemana, wala aliyetoka, wala aliyeingia, kwani wenyeji wote wa nchi hizi walikuwa na mahangaiko mengi.

6Ikasukumana, kabila na kabila nyingine, hata mji na mji mwingine, kwani Mungu aliwatisha na kuwasonga po pote.[#Luk. 21:10.]

7Lakini ninyi jitieni nguvu, wala msiilegeze mikono yenu! Kwani matendo yenu yatapata mshahara wao.[#1 Kor. 15:58.]

Sikukuu ya kumshukuru Mungu.

8Asa alipoyasikia hayo maneno ya ufumbuaji wa mfumbuaji Odedi akajishupaza, akayatowesha matapisho katika nchi yote ya Yuda na ya Benyamini, hata katika miji, aliyoiteka milimani kwa Efuraimu, nayo meza ya kumtambikia Bwana iliyokuwa mbele ya ukumbi wa Bwana akairudishia upya.

9Kisha akawakusanya Wayuda na Wabenyamini wote nao waliokaa ugenini kwake, Waefuraimu na Wamanase na Wasimeoni, kwani wengi waliokuwa Waisiraeli walirudi upande wake walipoona, ya kuwa Bwana Mungu wake yuko pamoja naye.

10Wakakusanyika Yerusalemu katika mwezi wa tatu wa mwaka wa kumi na tano wa Ufalme wa Asa,

11wakamtolea Bwana siku hiyo ng'ombe za tambiko, walizozitoa katika mateka: ng'ombe 700 na kondoo 7000.

12Wakaagana, wamtafute Bwana Mungu wa baba zao kwa mioyo yao yote na kwa roho zao zote,[#Yos. 24:25.]

13kwamba: Kila asiyemtafuta Bwana Mungu wa Isiraeli auawe, mdogo kwa mkubwa, mume kwa mke.

14Wakamwapia Bwana kuyafanya hayo wakipaza sauti za kumshangilia na kupiga matarumbeta na mabaragumu.

15Wayuda wote wakakifurahia hicho kiapo, kwani waliapa kwa mioyo yao yote; kwa kuwa walimtafuta Bwana kwa kupendezwa kabisa, akawaonekea, akawapatia kutulia pande zote.[#2 Mambo 14:6-7; 20:30.]

(16-18: 1 Fal. 15:13-15.)

16Mfalme Asa akamwondoa naye mama yake Maka katika ukuu wake, kwa kuwa alitengeneza kinyago cha Ashera, nacho kinyago chake Asa akakikatakata na kukipondaponda, kisha akakiteketeza penye kijito cha Kidoroni.

17Lakini matambiko ya vilimani hayakutoweka kwao Waisiraeli, lakini moyo wake Asa ulikuwa mtimilifu siku zake zote.

18Navyo, baba yake alivyovitakasa, pamoja navyo alivyovitakasa mwenyewe, fedha na dhahabu na vyombo, akavipeleka Nyumbani mwa Mungu.

19Vita havikuwako hata mwaka wa 35 wa ufalme wa Asa.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania