2 Mambo 16

2 Mambo 16

Asa anatafuta msaada kwa mfalme wa Ushami.

(1-6: 1 Fal. 15:16-22.)

1Katika mwaka wa 36 wa ufalme wa Asa ndipo, Basa, mfalme wa Waisiraeli, alipopanda kuijia nchi ya Yuda, akajenga Rama, asipatikane mtu anayeweza kutoka wala kuingia kwa Asa, mfalme wa Wayuda.

2Ndipo, Asa alipochukua fedha na dhahabu katika vilimbiko vya Nyumba ya Bwana na vya nyumba ya mfalme, akazituma kwake Benihadadi, mfalme wa Ushami, aliyekaa Damasko, kumwambia:

3Liko agano, tuliloliagana mimi na wewe, naye baba yangu na baba yako; kwa hiyo ninatuma kwako fedha na dhahabu. Nenda, ulivunje agano, uliloliagana na Basa, mfalme wa Waisiraeli, aondoke kwangu!

4Benihadadi akamwitikia mfalme Asa, akawatuma wakuu wa vikosi vyake, alivyokuwa navyo, kwenda kupigana na miji ya Waisiraeli, wakaiingia miji ya Iyoni na Dani na Abeli-Maimu na miji yote ya Nafutali iliyokuwa yenye vilimbiko.

5Basa alipoyasikia haya akaacha kuujenga Rama na kuzikomesha kazi zake.

6Kisha mfalme Asa akawatwaa Wayuda wote, wakayachukua mawe ya huko Rama nayo miti yake, Basa aliyoitumia ya kujenga Rama, naye akaitumia ya kujenga Geba na Misipa.

Mfumbuaji Hanani anamwonya Asa.

7Siku hizo mtazamaji Hanani akaja kwa Asa, mfalme wa Wayuda, akamwambia: Kwa kuwa umemwegemea mfalme wa Ushami, usimwegemee Bwana Mungu wako, kwa hiyo vikosi vya mfalme wa Ushami vimeponyoka mkononi mwako.[#Yer. 17:5.]

8Wale Wanubi na Walibia hawakuwa vikosi vingi vyenye magari na wapanda farasi wengi mno? Lakini kwa kuwa ulimwegemea Bwana, akawatia mkononi mwako.[#2 Mambo 14:9-13.]

9Kwani macho ya Bwana huzunguka katika nchi zote, ajitokeze kuwa mwenye nguvu kwao waliomwelekezea mioyo yao yote mizima. Katika jambo hili umefanya upumbavu, kwa hiyo tangu sasa huna budi kupiga vita.

10Asa akamkasirikia mtazamaji, akamfunga nyumbani mwenye mikatale, kwani alimchafukia kwa ajili ya hayo. Nao watu wengine Asa akawakorofisha siku zile.[#2 Mambo 18:26; Mat. 14:3.]

Kufa kwake Asa.

(11-14: 1 Fal. 15:23-24.)

11Mambo ya Asa, ya kwanza na ya mwisho, tukitaka kuyatazama, tunayaona, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Wayuda na wa Waisiraeli.

12Katika mwaka wa 39 wa ufalme wake Asa akaugua miguu, huu ugonjwa wake ukazidi sana; namo katika huu ugonjwa wake hakumtafuta Bwana, ila waganga.

13Kisha Asa akaja kulala na baba zake, akafa katika mwaka wa 41 wa ufalme wake.

14Wakamzika penye makaburi yake, aliyojichimbia mjini mwa Dawidi; wakamlaza katika kilalo walichokijaza uvumba wa namna nyingi na manukato yaliyotengenezwa na mafundi, wakamvukizia mavukizo makubwa sana.[#2 Mambo 21:19; Yer. 34:5.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania