2 Mambo 18

2 Mambo 18

Yosafati na Ahabu wanampelekea mfalme wa Ushami vita.

(Taz. 1 Fal. 22.)

1Ikawa, Yosafati alipopata mali na macheo mengi akamwoza mwanawe binti Ahabu.[#2 Mambo 17:5.]

2Miaka ilipopita michache, akashuka kwenda Samaria kwake Ahabu; Ahabu akamchinjia yeye na watu wake, aliokuwa naye, mbuzi na kondoo na ng'ombe wengi, akamchochea kupanda Ramoti wa Gileadi.

3Ahabu, mfalme wa Waisiraeli, akamwuliza Yosafati, mfalme wa Wayuda: Utakwenda pamoja na mimi Ramoti wa Gileadi? Akamwambia: Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, tutakwenda pamoja na wewe vitani.

4Kisha Yosafati akamwambia mfalme wa Waisiraeli: Uliza leo hivi, Bwana atakavyosema![#2 Fal. 3:11.]

5Ndipo, mfalme wa Waisiraeli alipowakusanya wafumbuaji, watu 400, akawauliza: Twende Ramoti wa Gileadi kupga vita au niache? Wakasema: Panda tu! Mungu atautia mkononi mwa mfalme.

6Yosafati akauliza: Huku hakuna tena mfumbuaji wa Bwana, tumwulize naye?

7Mfalme wa Waisiraeli akamwambia Yosafati: Yuko bado mtu mmoja wa kumwuliza neno la Bwana, lakini mimi ninamchukia, kwani hanifumbulii yatakayokuwa mema, ila siku zote husema yatakayokuwa mabaya, naye ndiye Mikaya, mwana wa Imula. Yosafati akasema: Mfalme asiseme hivyo!

8Ndipo, mfalme wa Waisiraeli alipomwita mtumishi mmoja wa nyumbani, akamwambia: Piga mbio kumwita Mikaya, mwana wa Imula!

9Mfalme wa Waisiraeli na Yosafati, mfalme wa Wayuda, walikuwa wamekaa kila mmoja katika kiti chake cha kifalme na kuvaa mavazi, wakawa wakikaa hapo pa kupuria ngano penye lango la kuuingilia mji wa Samaria, nao wafumbuaji wote wakawa wakifumbua mbele yao.

10Ndipo, Sedekia, mwana wa Kenaana, alipojifanyizia pembe za chuma, akasema: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa pembe kama hizi utawakumba Washami, mpaka uwamalize.

11Nao wafumbuaji wote wakafumbua hivyo kwamba: Upandie Ramoti wa Gileadi! Utafanikiwa, naye Bwana atautia mkononi mwake mfalme.

12Yule mjumbe aliyekwenda kumwita Mikaya akamwambia kwamba: Tazama, maneno ya wafumbuaji ni kinywa kimoja tu cha kufumbua mema yatakayomjia mfalme, Basi, neno lako nalo na liwe kama neno la mmoja wao hao, useme mema yatakayokuwa.

13Mikaya akasema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, nitasema hayo tu, Mungu wangu atakayoniambia.

Mfumbuaji Mikaya anamkataza Yosafati kwenda vitani.

14Alipofika kwake mfalme, mfalme akamwuliza: Mika, twende Ramoti wa Gileadi kupiga vita au niache? Akasema: Pandeni! Mtafanikiwa, maana watatiwa mikononi mwenu.

15Mfalme akamwambia: Nimekuapisha mara nyingi, usiniambie mengine katika Jina la Bwana, isipokuwa iliyo ya kweli.

16Ndipo, aliposema: Nimewaona Waisiraeli, nao walikuwa wametawanyika milimani kama kondoo wasio na mchungaji, naye Bwana akasema: Hawa hawana bwana, na warudi na kutengemana kila mtu nyumbani kwake.

17Mfalme wa Waisiraeli akamwambia Yosafati: Sikukuambia: Hanifumbulii yatakayokuwa mema, ila yatakayokuwa mabaya tu?

18Mikaya akasema: Lakini lisikieni neno la Bwana! Nimemwona Bwana, akikaa katika kiti chake kitukufu, navyo vikosi vyote vya mbinguni vikasimama kuumeni na kushotoni kwake.

19Bwana akauliza: Yuko nani atakayemponza Ahabu, mfalme wa Waisiraeli, aje kuupandia Ramoti wa Gileadi, aangushwe huko? Wakajibu, mmoja akisema hivi, mmoja hivi.

20Kisha akatokea roho, akasimama mbele ya Bwana, akasema: Mimi nitamponza. Bwana akamwuliza: Kwa nini?

21Akasema: Nitatoka kuwa roho ya uwongo vinywani mwa wafumbuaji wake wote. Bwana akasema: Utamponza kweli, utaweza hivyo, toka kufanya hivyo!

22Sasa tazama! Bwana ametia roho ya uwongo vinywani mwa hawa wafumbuaji wako, maana yeye Bwana amekwisha kukutakia mabaya.

23Ndipo, Sedekia, mwana wa Kenaana, alipomkaribia Mikaya, akampiga makofi na kumwuliza: Roho ya Mungu imeshika njia gani, inipite mimi, ije kusema na wewe?[#2 Mambo 18:10.]

24Mikaya akasema: Jiangalie! Utaviona siku hiyo, utakapoingia chumba kwa chumba, upate kujificha.

25Mfalme wa Waisiraeli akasema: Mchukueni Mikaya, mmrudishe kwa Amoni, mkuu wa mji, na kwa Yoasi, mwana wa mfalme,

26mseme: Hivi ndivyo, mfalme anavyosema: Mwekeni huyu kifungoni, mmpe chakula cha mahangaiko na maji ya mahangaiko, hata nitakaporudi salama.[#2 Mambo 16:10.]

27Mikaya akasema: kama utarudi salama, Bwana hakusema kinywani mwangu. Kisha akasema: Lisikieni hili, ninyi makabila yote!

Kufa kwake Ahabu.

28Kisha mfalme wa Waisiraeli na Yosafati, mfalme wa Wayuda, wakapanda kwenda Ramoti wa Gileadi.

29Mfalme wa Waisiraeli akamwambia Yosafati: nitavaa nguo nyingine, niingie penye mapigano, lakini wewe zivae nguo zako! Ndipo, mfalme wa Waisiraeli alipovaa nguo nyingine, kisha wakafika penye mapigano.

30Naye mfalme wa Ushami alikuwa amewaagiza wakuu wa magari, aliokuwa nao, kwamba: Msipigane na mtu ye yote, mdogo kwa mkubwa, ila mpigane na mfalme wa Waisiraeli peke yake tu!

31Ikawa, wakuu wa magari walipomwona Yosafati wakamwazia yeye kuwa mfalme wa Waisiraeli, wakamzunguka kupigana naye. Ndipo, Yosafati alipopiga yowe, Bwana akamsaidia, yeye Mungu akawaondoa hapo, alipokuwa, na kuwadanganyadanganya.

32Ikawa, wakuu wa magari walipoona, ya kuwa siye mfalme wa Waisiraeli, wakarudi na kuacha kumfuata.

33Kulikuwa na mtu, akauvuta upindi wake kwa kubahatisha tu, akampiga mfalme wa Waisiraeli hapo, vyuma vya kisibau chake vilipounganishwa. Ndipo, alipomwambia mwendeshaji wa gari: ligeuze kwa mkono wako, unitoe hapa, wanapopigana, kwani nimeumia.

34Mapigano yakazidi siku hiyo, kwa sababu hii mfalme wa Waisiraeli alikuwa amejisimamisha garini ng'ambo ya huku kuwaelekea Washami hata jioni, akafa, jua lilipokuchwa.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania