The chat will start when you send the first message.
1Yosafati, mfalme wa Wayuda, aliporudi nyumbani kwake kutengemania Yerusalemu,
2Yehu, mwana wa Hanani, aliyekuwa mchunguzaji akamtokea, akamwambia mfalme Yosafati: Inakuwaje, ukipenda kumsaidia asiyemcha Mungu, nao wanaomchukia Bwana? Kwa sababu hii makali yatokayo kwake Bwana yanakukalia.
3Lakini tena yako mema yaliyoonekana kwako, kwani umevitowesha vinyago vya Ashera katika nchi hii, ukauelekeza moyo wako kumtafuta Mungu.[#2 Mambo 17:3-6.]
4Yosafati alipokaa Yerusalemu kidogo, akatoka tena kwenda kwa watu, akawaanzia wa Beri-Seba, hata awafikie wa milimani kwa Efuraimu, akawarudisha kwake Bwana Mungu wa baba zao.
5Akaweka waamuzi katika nchi hii katika miji yote ya Yuda iliyokuwa yenye maboma, mji kwa mji,
6akawaambia waamuzi: yaangalieni mtakayoyafanya! Kwani sio watu, mnaowafanyia kazi ya uamuzi, ila Bwana, naye yuko pamoja nanyi, mnapokata mashauri.
7Kwa sababu hii tisho la Bwana na liwakalie, mzifanye kazi zenu na kujiangalia! Kwani kwake Bwana hakuna wala upotovu, wala upendeleo, wala upenyezi.[#2 Mose 18:21; 5 Mose 10:17.]
8Namo Yerusalemu Yosafati akaweka Walawi wengine na watambikaji, hata wakuu wengine wa milango ya Isiraeli kumfanyizia Bwana kazi ya uamuzi na kuwagombea watu. Waliporudi Yerusalemu,[#5 Mose 17:8-9; 19:17.]
9akawaagiza kwamba: Haya myafanye kwa kumwogopa Bwana na kwa welekevu na kwa mioyo yote!
10Katika magomvi yote yatakayoletwa kwenu na ndugu zenu wanaokaa katika miji yao, kama ni kugombeana damu zilizomwagwa au maonyo na maagizo au maongozi na maamuzi, mtawafundisha, wasimkosee Bwana, makali yakawajia ninyi nao walio ndugu zenu. Fanyeni hivyo, msikore manza!
11Tazameni, mtambikaji mkuu Amaria atawaongoza katika mambo yote ya Bwana, naye Zebadia, mwana wa Isimaeli, mwenye amri wa mlango wa Yuda, atawaongoza katika mambo yote ya mfalme, nao Walawi wako mbele yenu kuwasimamia watu. Jipeni mioyo, kafanyeni hivyo! Ndipo, Bwana atakapokuwa nao wale walio wema.