2 Mambo 2

2 Mambo 2

Maagano ya Salomo na mfalme Hiramu.

(Taz. 1 Fal. 5:1-16.)

1Salomo akawaza kulijengea Jina la Bwana nyumba, tena kujijengea mwenyewe nyumba ya kifalme.

2Ndipo, Salomo alipohesabu wachukuzi 70000 na mafundi wa kuchonga mawe 80000, akawapeleka milimani pamoja na wasimamizi wao 3600.

3Kisha Salomo akatuma watu kwa Huramu, mfalme wa Tiro, kwamba: Kwa hivyo, ulivyopatana na baba yangu Dawidi, ukampelekea miti ya miangati ya kujijengea nyumba ya kukaa humo,[#1 Mambo 14:1.]

4tazama, mimi ninataka kulijengea Jina la Bwana Mungu wangu nyumba, niitakase kuwa yake, wavukizie mle mbele yake mavukizo yanukayo vizuri, tena wamwekee mikate siku zote, tena wamtolee ng'ombe za tambiko za asubuhi na za jioni na za siku za mapumziko na za miandamo ya mwezi na za sikukuu za Bwana Mungu wetu, maana hayo ndiyo mazoeo ya Waisiraeli ya kale na kale.

5Nayo nyumba, nitakayoijenga, sharti iwe kubwa, kwani Mungu wetu ni mkubwa kuliko miungu yote.[#Sh. 86:8.]

6Lakini yuko nani anayejipatia nguvu ya kumjengea nyumba? Kwani haenei mbinguni, wala mbinguni palipo juu ya mbingu. Mimi nami ni mtu gani nikimjengea nyumba, isipokuwa ya kuvukizia tu mbele yake?[#2 Mambo 6:18; 1 Fal. 8:27.]

7Kwa hiyo tuma sasa kwangu mtu aliye fundi kweli wa kutengeneza vyombo kwa dhahabu na kwa fedha na kwa shaba na kwa chuma na kwa nguo za kifalme nyekundu na nyeusi na kwa nguo za rangi, ajuaye hata kuchora machoro pamoja na mafundi walioko kwangu huku Yuda namo Yerusalemu, baba yangu Dawidi aliowaweka.

8Tena niletee miti ya miangati na mivinje na mininga toka Libanoni, kwani mimi ninajua, ya kuwa watumishi wako hujua kuichonga miti ya Libanoni; nao watu wangu utawaona wa kusaidiana na watu wako,

9wanitengenezee miti mingi, kwani nyumba, mimi nitakayoijenga, itakuwa kubwa ya ajabu.

10Tazama, maseremala wanaoichonga miti walio watu wako nitawapa kori 20000, ndio frasila 200000 za ngano na kori 20000, ndio frasila 200000 za mawele na bati 20000, ndio vibaba 700000 vya mvinyo na bati 20000, ndio vibaba 700000 vya mafuta.

11Huramu, mfalme wa Tiro, akamjibu kwa barua, aliyoituma kwake Salomo kwamba: Kwa hivyo, Bwana anavyoupenda ukoo wake, amekupa kuwa mfalme wao.

12Huramu akaendelea akisema: Bwana Mungu wa Isiraeli aliyeziumba mbingu na nchi na atukuzwe, kwa kuwa amempa mfalme Dawidi mwana aliye mwerevu wa kweli ajuaye kuzitumia akili na utambuzi, amjengee Bwana nyumba, ajijengee naye nyumba ya kifalme!

13Sasa natuma kwako mtu aliye fundi kweli, mwenye ujuzi na utambuzi, aliyemfanyia baba yangu Huramu kazi.

14Ni mwana wa mwanamke wa wana wa kike wa Dani, naye baba yake ni mtu wa Tiro; yeye anajua kutengeneza vyombo kwa dhahabu na kwa fedha na kwa shaba na kwa chuma, kwa mawe na kwa miti, kwa nguo za kifalme nyekundu na nyeusi na kwa nguo za bafta na za rangi, tena anajua kuchora machoro na kutengeneza kazi zote za kifundi, akisaidiwa na mafundi wako na mafundi wa bwana wangu Dawidi.[#2 Mose 31:2-6.]

15Sasa bwana wangu na awapelekee watumishi wake ngano na mawele, mvinyo na mafuta, aliyoyasema.

16Nasi tutakata miti huko Libanoni yote, utakayoitaka ya kutumia, kisha tutaipeleka kwako kwa kuieleza baharini hata Yafo (Yope), huko utaichukua kuipeleka Yerusalemu.

17Ndipo, Salomo alipowahesabu waume wageni wote waliokaa katika nchi, akiifuata njia ya kuhesabu, baba yake Dawidi aliyoishika alipowahesabu, wakaonekana watu 153600.

18Kwao hao akatoa 70000 kuwa wachukuzi, 80000 kuchonga mawe milimani, 3600 kuwa wasimamizi wa kuwafanyisha watu kazi.[#Yos. 9:27.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania