2 Mambo 20

2 Mambo 20

Yosafati anawashinda Waamoni na Wamoabu.

1Ikawa baada ya hayo, wakaja wana wa Moabu na wana wa Amoni pamoja na Waamoni wengine kumpelekea Yosafati vita.

2Watu wakaja kumpasha Yosafati habari kwamba: Uvumi wa watu wengi unakujia, unatoka ng'ambo ya huko ya bahari upande wa Ushami, nao wamekwisha kufika Hasesoni-Tamari, ndio Engedi.

3Yosafati akaogopa, akamwelekezea Bwana uso wake na kulitafuta shauri lake, akatangaza katika nchi yote ya Yuda, watu wafunge.

4Wayuda wakakusanyika kutafuta msaada kwa Bwana; walipokwisha kufika na kutoka katika miji yote ya Yuda, wamtafute Bwana,[#2 Mambo 15:9-15.]

5Yosafati akaja kusimama katika huo mkutano wa Wayuda na Wayerusalemu Nyumbani mwa Bwana mbele ya ua mpya,

6akasema: Bwana Mungu wa baba zetu, wewe siwe Mungu akaaye mbinguni na kuzitawala nchi zote za wamizimu zenye wafalme? Mkononi mwako zimo nguvu na uwezo mwingi, hakuna awezaye kujisimamisha kwako.[#1 Mambo 29:12; 2 Mambo 14:11.]

7Wewe hukuwafukuza wenyeji wa nchi hii mbele yao walio ukoo wako wa Waisiraeli, ukaitoa na kuwapa wao wa uzao wa mpenzi wako Aburahamu, iwe yao kale na kale?

8Wakakaa huku, wakakujengea huku Patakatifu pa Jina lako kwa kwamba:

9Mabaya yatakapotujia, kama panga za kutupatiliza au magonjwa ya kuambukiza au njaa, tuje kusimama mbele ya Nyumba hii na kukulalamikia usoni pako kwa kusongeka kwetu, kwani Jina lako linakaa humu Nyumbani; ndipo, utakapotusikia, utuokoe.[#2 Mambo 6:28-30.]

10Sasa watazame hawa wana wa Amoni na wa Moabu na wa milima ya Seiri! Hapo, Waisiraeli walipotoka katika nchi ya Misri, hukuwapa ruhusa kuingia kwao hawa; kwa hiyo waliondoka kwao pasipo kuwaangamiza.[#5 Mose 2:4-5,9,19.]

11Sasa unawaona, wanavyotufanyizia wakija kutufukuza katika nchi hii, uliyotupatia, utupe sisi, iwe fungu letu.

12Mungu wetu, hutaki kuwapatiliza? Kwani kwetu sisi hakuna nguvu za kuushinda huu uvumi ya watu wengi mno waliotujia. Sisi hatujui la kufanya, kwa hiyo macho yetu yanakuelekea.

13Nao Wayuda wote walikuwa wamesimama mbele ya Bwana pamoja na watoto wao wachanga na wanawake na wana wao.

14Ndipo, Yahazieli, mwana wa Zakaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yieli, mwana wa Matania, aliyekuwa Mlawi wa mlango wa Asafu, alipoingiwa na Roho ya Bwana pale katikati ya mkutano,

15akasema: Ninyi Wayuda wote nanyi wenyeji wa Yerusalemu na wewe mfalme Yosafati, sikilizeni: Haya ndiyo, Bwana anayowaambia: Msiogope, wala msiingiwe na vituko mkiuona uvumi huu wa watu wengi! Kwani vita hivi si vyenu, ila vya Mungu.[#2 Mose 14:14.]

16Kesho shukeni kwenda kwao! Ndipo, mtakapowaona, wakipanda pa kupandia kwenda Sisi, nanyi mtawakuta kwenye mwisho wa bonde lililoko mbele ya nyika ya Yerueli.

17Lakini ninyi hamtapigana huko, jipangeni tu na kusimama, mwone, Bwana atakavyowapatia wokovu, ninyi Wayuda na Wayerusalemu! Msiogope, wala msiingiwe na vituko! Kesho watokeeni tu! Naye Bwana atakuwa nanyi.

18Ndipo, Yosafati alipouinamisha uso wake hata chini, hata Wayuda wote pamoja na wenyeji wa Yerusalemu wakamwangukia Bwana na kumwomba.

19Kisha wakainuka Walawi waliokuwa wa mlango wa Kehati na wa Kora kumshangilia Bwana Mungu wa Isiraeli, wakizipaza kabisa sauti zao ziwe kuu.

20Kesho yake wakaondoka na mapema kwenda nyikani kwa Tekoa; hapo, walipotoka, Yosafati akasimama hapo akisema: Nisikilizeni, ninyi Wayuda na wenyeji wa Yerusalemu! Mtegemeeni Bwana Mungu wenu, ndipo, mtakaposhupazwa! Wategemeeni nao wafumbuaji wake, ndipo, mtakapofanikiwa![#Yes. 28:16.]

21Alipokwisha kuwapa watu shauri hili akaweka watakaomwimbia Bwana nao watakaoutukuza urembo wa Patakatifu, watoke na kuwatangulia wenye mata na kusema: Mshukuruni Bwana, ya kuwa upole wake ni wa kale na kale![#Sh. 106:1.]

22Papo hapo, walipoanza kupiga yowe na shangwe, ndipo, Bwana alipoleta watu wa kuwavizia wana wa Amoni na wa Moabu nao wa milima ya Seiri walioingia katika nchi ya Yuda.

23Maana wana wa Amoni na wa Moabu wakawainukia wenyeji wa milimani kwa Seiri na kuwaua na kuwaangamiza, walipokwisha kuwamaliza wenyeji wa Seiri, wakasaidiana kila mtu na mwenzake kuuana.[#1 Sam. 14:20.]

24Wayuda walipofika hapo pa kuchungulia nyikani, wakiugeukia ule uvumi wa watu, wakaona mizoga tu iliyolala chini, hakuwako aliyepona.

25Ndipo, Yosafati na watu wake walipokuja kujichukulia nyara, wakaona kwao mali nyingi penye hiyo mizoga na vyombo vyenye kima, wakawavua vingi mno, wasiweze kuvichikua vyote; wakawako siku tatu wakipokonya nyara, kwani zilikuwa nyingi.

26Siku ya nne wakakusanyika katika Bonde la Tukuzo, kwani huko ndiko, walikomtukuzia Bwana; kwa sababu hii mahali pale wakapaita Bonde la Tukuzo hata leo.

27Kisha watu wote wa Yuda na wa Yerusalemu wakarudi, naye Yosafati akawatangulia kurudi Yerusalemu na kufurahi, kwani Bwana aliwapa kuwafurahia adui zao.

28Wakaingia Yerusalemu na kupiga mapango na mazeze na matarumbeta, wakaingia Nyumbani mwa Bwana.

29Tisho la Bwana likaziguia hizo nchi zote zenye wafalme, waliposikia, ya kama Bwana amepigana na adui za Waisiraeli.

30Kwa hiyo ufalme wa Yosafati ukapata kutengemana, Mungu wake akimpatia utulivu pande zote.[#2 Mambo 15:15.]

Kutawala kwake Yosafati.

(20:31—21:1: 1 Fal. 22:41-51.)

31Yosafati akawa mfalme wa Wayuda, naye alikuwa mwenye miaka 35 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 25. Jina la mama yake ni Azuba, binti Silihi.

32Akaendelea kuishika njia ya baba yake Asa, hakuiacha kabisa, akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana.

33Matambiko ya vilimani tu hayakukoma, kwani watu hawajamwelekezea Mungu wa baba zao mioyo yao.

34Mambo mengine ya Yosafati, ya kwanza na ya mwisho, tunayaona, yameandikwa katika mambo ya Yehu, mwana wa Hanani, yaliyotiwa katika kitabu cha wafalme wa Waisiraeli.

Yosafati anafanya maagano na Ahazia.

35Baada ya hayo Yosafati, mfalme wa Wayuda, akajiunga na Ahazia, mfalme wa Waisiraeli; lakini huyu matendo yake, aliyoyafanya, yalikuwa maovu.[#1 Fal. 22:52-54.]

36Akajiunga naye kwa kutengeneza merikebu za kwenda Tarsisi; wakatengeneza merikebu hata huko Esioni-Geberi.

37Eliezeri, mwana wa Dodawa wa Maresa, akamfumbulia Yosafati kwamba: Kwa kuwa umejiunga na Ahazia, Bwana atazivunja hizi kazi zako. Kwa hiyo vyombo vikavunjika, havikuweza kwenda Tarsisi.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania