2 Mambo 23

2 Mambo 23

Yoasi anapata ufalme.

(Taz. 2 Fal. 11:4-20.)

1Katika mwaka wa saba Yoyada akajishupaza, akawachukua wakuu wa mamia, Azaria, mwana wa Yerohamu, na Isimaeli, mwana wa Yohana, na Azaria, mwana wa Obedi, na Masea, mwana wa Adaya, na Elisafati, mwana wa Zikiri, akafanya maagano nao.

2Wakazunguka katika nchi ya Yuda, wakawakusanya Walawi na kuwatoa katika miji yote ya Yuda pamoja na wakuu wa milango ya Isiraeli, wakaja Yerusalemu.

3Huu mkutano wote ukafanya agano na mfalme Nyumbani mwa Mungu, Yoyada akawaambia: Mtazameni huyu mwana wa mfalme! Atakuwa mfalme, kama Bwana alivyosema kwa ajili ya wana wa Dawidi.

4Hili ndilo neno, mtakalolifanya: fungu lenu la tatu, ninyi watambikaji na Walawi, watakaoingia kazi siku ya mapumziko, sharti walinde malangoni;

5fungu jingine la tatu sharti walinde nyumbani mwa mfalme, fungu jingine la tatu walinde langoni penye msingi. Kisha watu wote waje nyuani penye Nyumba ya Bwana.

6Lakini Nyumbani mwa Bwana mtu asiingie, wasipokuwa watambikaji nao Walawi wanaotumikia. Hao wataingia, kwani ndio watakatifu. Nao watu wote sharti walinde ulinzi wa Bwana,

7nao Walawi sharti wamzunguke mfalme pande zote, kila mtu akiyashika mata yake, kisha kila atakayeingia Nyumbani mwa Bwana na auawe! Hivyo sharti mwe na mfalme, akiingia, hata akitoka.

8Walawi na Wayuda wote wakayafanya yote, kama mtambikaji Yoyada alivyowaagiza, kila mtu akawachukua wate wake walioingia kazi siku ya mapumziko nao waliotoka kazi siku ya mapumziko, kwani mtambikaji Yoyada hakuwapa ruhusa waliozimaliza zamu.

9Kisha mtambikaji Yoyada akawapa wakuu wa mamia mikuki na ngao ndogo na kubwa za mfalme Dawidi zilizokuwa Nyumbani mwa Mungu.

10Akawapanga watu wote, kila mtu na mkuki wake mkononi mwake kuanzia upande wa kuume wa Nyumba kuufikia upande wa kushoto wa Nyumba, kuifikia meza ya kutambikia na tena kuifikia Nyumba yenyewe, wamzunguke mfalme pande zote.

11Kisha wakamtoa mwana wa mfalme, wakamvika kilemba cha kifalme, wakampa nacho kizingo cha Ushahidi, wakamfanya kuwa mfalme, Yoyada na wanawe wakimpaka mafuta na kusema: pongezi, mfalme!

Atalia anauawa.

12Atalia alipozisikia sauti za watu waliomkimbilia mfalme na kumshangilia, akaja naye hapo, watu walipo, penye Nyumba ya Bwana.

13Alipotazama, akamwona mfalme, akisimama katika ulingo wake pa kuingilia, nao wakuu na wapiga matarumbeta wakisimama kwake mfalme, nao watu wote wa nchi yao wakawa wenye furaha na kupiga matarumbeta, nao waimbaji wakavipiga vyombo vya kuimbia, wakawaongoza watu kushangilia. Ndipo, Atalia alipoyararua mavazi yake na kupiga kelele kwamba: Mmedanganyika! Mmedanganyika!

14Ndipo, mtambikaji Yoyada alipowatoa wakuu wa mamia waliovisimamia vikosi, akawaambia: Mtoeni hapa penye mipango ya watu! Naye atakayemfuata na auawe kwa upanga! Kwani mtambikaji alisema: Msimwue Nyumbani mwa Bwana!

15Wakamkamata kwa mikono, naye alipofika pa kuliingilia lango la farasi penye nyumba ya mfalme, wakamwua huko.

Matambiko ya Baali yanatoweshwa.

16Kisha Yoyada akafanya agano, yeye na watu wote na mfalme, wawe ukoo wake Bwana.[#2 Mambo 15:12.]

17Ndipo, watu wote walipoiingia nyumba ya Baali, wakaibomoa; nazo meza za kumtambikia na vinyago vyake wakavivunjavunja kabisa, naye Matani, mtambikaji wa Baali, wakamwua mbele ya meza za kutambikia.

18Kisha Yoyada akaweka watambikaji na Walawi kuwa wakaguzi wa Nyumba ya Bwana, kwani Dawidi aliwapatia hao kazi ya kuiangalia Nyumba ya Bwana, wamteketezee Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, kama ilivyoandikwa katika Maonyo ya Mose, pamoja na kuimba nyimbo za furaha, kama Dawidi alivyowaongoza.[#2 Mambo 29:30.]

19Akaweka nao walinda malango ya Nyumba ya Bwana, mtu asiingie akiwa mwenye uchafu kwa jambo lo lote.

20Kisha akawachukua wakuu wa mamia na watukufu na watawalaji wa watu nao watu wote wa nchi hii, akamtoa mfalme Nyumbani mwa Bwana, wakaingia nyumbani mwa mfalme na kupita katikati katika lango la juu, wakamketisha mfalme katika kiti cha kifalme.

21Wakafurahi watu wote wa nchi hii, nao mji ukatulia. Lakini Atalia walikuwa wamemwua kwa upanga.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania